Na Mwandishi Wetu
RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka waandishi wa Habari na vyombo vya Habari kwa ujumla kuutumia Uhuru wa vyombo vya Habari kuhabarisha Umma lakini kuweka na Uzalendo wakati wakifanya kazi zao.
Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji Tuzo za Samia Kalamu Awards, Rais Samia amesema, jambo ambalo ameahidi mara kwa mara kwa wanahabari ni kukuza Uhuru wa vyombo vya Habari na linaonekana wazi.
Rais Samia amesema, Uhuru wa Habari uliopo uendelee kuwa chachu kwa wanahabari lakini lazima Uhuru huo uendane na Uzalendo wanapotoa Habari kwa jamii.

Amewataka Waandishi wa Habari, kutumia Takwimu kutoa taarifa zao kwani uandishi wa kutumia takwimu una manufaa makubwa kwa jamii na unatoa nafasi kubwa kwa jamii kuona maendeleo yanayofanywa na Serikali.
Kuhusu matumizi ya Lugha sanifu ya Kiswahili, Rais Samia amewataka waandishi wa Habari kutumia lugha vizuri ili taarifa wanazozitoa zieleweke na pia kukuza lugha hiyo hapa nchini na ulimwenguni kwa ujumla.
Awali Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi amewaambia waandishi wa Habari kuwa uhuru wa kuandika na kutangaza Habari unapewa nguvu na Katiba ya 18 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini pia Ibara ya 30 katiba hiyo inaweka mipaka ya uhuru huo.

Amesema Ibara ya 30 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano Tanzania imeweka mipaka ya uhuru wa Habari kwa kuzingatia Usalama wa Taifa na Maadili ya Tanzania.
Amewataka waandishi wa Habari kufanya kazi zao kwa uhuru huku wakiongozwa na mipaka ya Uhuru huo ili kuendelea kulinda Maadili, Utamaduni na Usalama wa Taifa.