Shivji kawaanika wasomi wa sasa

HIVI karibuni nilipata fursa ya kusoma kitabu cha Edward Moringe Sokoine: Maisha na Uongozi wake. Huyu ni Waziri Mkuu wa zamani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT). Kitabu hiki kimejaa mambo mengi ambayo yanashikamanishwa na uongozi wa Sokoine akiwa Mbunge, Naibu Waziri, Waziri wa Ulinzi na baadaye Waziri Mkuu wa JMT. Ndani ya kitabu hicho ipo sura iliyobeba kichwa kisemacho: Hitimisho Fikirishi- Tafakuri Tunduizi Juu ya Uongozi wa Edward Sokoine, sura hii imeandikwa na Mwanazuoni mbobezi, Profesa Issa Shivji.

Katika sura hiyo, Profesa Shivji ananukuu hotuba nyingi za Sokoine, lakini nukuu ambayo imevuta hisia zangu na kunisukuma kuandika safu hii wiki hii ni hii: “Kwa mujibu wa nadharia kuhusu maendeleo, nchi yoyote haiwezi kuendelea bila kuwa na mijadala juu ya mielekeo mbalimbali ya maendeleo. Jukumu mojawapo la wasomi wa Kitanzania ni kuchochea na kuongoza mijadala hii.” Shivji anamnukuu Sokoine wakati alipohutubia wanazuoni katika Chuo Kiku cha Dar es Salaam wakati wa kuadhimisha miaka 10 ya Taasisi ya Taaluma na Maendeleo (Institute of Development Studies- IDS) chuoni hapo Oktoba 12, 1993. Hata hivyo, Shivji aliongeza maelezo yake akifafanua juu ya umuhimu wa mijadala hasa katika taasisi za elimu ya juu. Anasema umuhimu wake unabaki palepale. Hata hivyo, anasema katika miongo miwili hivi, siyo mijadala tu imedidimia chuoni hapo, bali imeisha kabisa. Anasema hajui kama Sokoine angelifufuka angesema nini. Labda angesusia kabisa kwenda chuoni hapo.

Profesa Shivji ni mwanazuoni wa kweli. Anakijua Chuo Kikuu cha Da es Salaam, tangu zama za harakati za mapambano ya kudai uhuru kwa nchi za Afrika, harakati za siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na sera ya Azimio la Arusha; harakati za mageuzi ya kiuchumi na hata sasa siasa za sera za mfumo wa uchumi huria. Ameshiriki katika mijadala mingi na mizito ya kitaifa na kimataifa ikilenga sera za maendeleo na haki za wananchi kujitawala katika nchi yao. Profesa Shivji ni mwanazuoni wa viwango vya juu kabisa vya kimataifa.

Mtu wa viwango vya Profesa Shivji anaposema kwamba mijadala Chuo Kikuu cha Dar es Salaam imekwisha kabisa, huwezi tu kupinga hivi hivi. Kwanza, yeye ni tunda la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, maisha yake ya kitaaluma takribani miaka 50, ameitumia kwenye chuo hicho, anakijua, amelelewa hapo. Sasa suala la kujiuliza ni hili, hivi kama chuo kikuu hakina tena mijadala, kinageuka kuwa nini sasa? Je, ni nini hasa kimeua mijadala hiyo? Je, Ipo sera mahususi ya serikali ya kuzuia uhuru wa kitaaluma katika vyuo vya elimu ya juu?

Kwa hakika, ili chuo kikuu kipate hadhi ya kuitwa chuo kikuu jambo la umuhimu wa kipekee ni uhuru wa kitaaluma. Kwamba wanafunzi na wahadhiri wao wote wana uhuru wa mawazo kitaaluma, hawapangiwi wawaze vipi, lini, wapi na kwa nini? Wana uhuru kamili wa mawazo. Chuo Kikuu ni jamii yenye uhuru wa mawazo mijadala, tena ya moto. Mijadala chuo kikuu chochote ni  ni mambo yasiyoepukika.

Katika mazingira tunayoishi nchini kwetu sasa hivi mtu anapaswa kujiuliza swali moja la kimsingi, hivi jamii yetu imeamka kwa kiwango gani? Je, jamii yetu inajisumbua kwa lolote? Inajali lolote? Kama majibu ni hapana, je, katika taifa la namna hiyo kunaweza kupatikana taasisi za elimu ya juu zinazojali? Labda nipanue zaidi goli, hivi jamii ya ovyo isiyojali lolote inaweza kudai mambo ya maana yoyote? Tumeelezwa kwamba jamii yoyote ile hupata viongozi wanaostahili kwa sababu nao ni sehemu ya jamii hiyo. Hivyo hivyo, wasomi wa vyuo vya elimu ya juu nao wanatokana na jamii yake, yamkini watafanana na jamii yake. Pengine haya ndiyo mambo ya kujiuliza. Kwamba je, sisi tumekuwa jamii ya ovyo kiasi kwamba hata taasisi zetu, iwe ni za elimu, za afya, za kilimo, za haki, za kutunga sheria, za kila kitu nazo zimekuwa ni za ovyo? Ni vigumu kupata jibu la moja kwa moja, lakini upo uwezekano kwamba kwa kadri tunavyojiruhusu kama jamii kuachia mambo ya ovyo kutokea au kuendeshwa katika nchi yetu, ndivyo tunazidi kujididimiza katika matatizo mengi kwa kila nyanja.

Wakati Profesa Shivji akibashiri kwamba kama Sokoine angelifufuka leo asingekanyaga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa sababu ya kuwa ‘butu’ kabisa katika mijadala, yafaa pia kujiuliza kwa kina, hivi Tanzania kama taifa, katika eneo hili la demokrasia ambayo kwa hakika watu wako huru kushiriki katika mambo ya taifa lao kwa uhuru bila hofu, tunasimamia wapi? Hivi kama taifa ni kwa kiwango gani tunaheshimu, kulinda na kutetea uhuru wa kila raia katika kushiriki mambo yanayohusu nchi yake kwa haki?

Profesa Shivji ameamua kuwa muungwana bila kutaka kufunguka zaidi juu ya kisa cha vuguvugu la mijadala kupotea kabisa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, chuo kikongwe kuliko vyote nchini Tanzania. Ukweli uliopo ni kwamba wanataaluma wameamua kwamba taaluma haina tena thamani kama nafasi za kisiasa za kuchaguliwa au kuteuliwa. Wengi wameamini kwamba maisha ni mepesi na ya mafanikio zaidi katika uteuzi kuliko katika taaluma. Mfumo huu wa kuachia nafasi za uteuzi, hasa za kisiasa, kuwa ndizo zenye kuwahakikishia waliozikalia unafuu mkubwa wa maisha- malipo manono- umeathiri mno jamii yetu. Kila kitu sasa kinadharauliwa, na kila mmoja sasa anatamani kukimbilia kwenye siasa.

Ingawa siasa siyo jambo la haramu likiwa linatambuliwa kisheria kabisa kuwa ni halali, hata hivyo, kwa jinsi ambavyo katika miaka ya hivi karibuni imekuwa inaendeshwa, imefanya taifa letu kuingia katika mtihani mbaya. Mtihani wa kunyang’anya watu uhuru wa kufikiri, uhuru wa kukosoa, uhuru wa kuja na mawazo mbadala ya kujenga. Matokeo yake tumejenga jamii ya watu wanaojipendekeza, wanaojiondoa ufahamu, wanaoamini kwamba akili zao haziwezi kuwasaidia kwa kusimama kwa miguu yao, kuendeleza uchawa ndiko kumeonekana kuwa kunalipa.

Ugonjwa huu haujakamata jamii ya huku nje tu, umetambaa na kutamalaki katika vyuo vya elimu ya juu kiasi kwamba ile mijadala ya moto ambayo hata Sokoine aliitamani, haipo tena. Hakuna anayetaka kuonekana kuwa na fikra tunduizi. Hakuna. Kisa? Anaogopa kuudhi au kupoteza nafasi yake ya uwezekano wa kukumbukwa katika uteuzi.

Taifa lote linaugua ugonjwa wa uteuzi. Wasomi wanaogopa kutumia taaluma zao, kuhoji na kujadili kuhusu mustakabali wa taifa lao, kwa sababu wanawaza uteuzi. Wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nao wameingia kwenye mkondo huo huo, kuwaza uteuzi. Katika mazingira haya, nani anatamani mijadala ya maana kuhusu maendeleo ya taifa? Ugonjwa huu usipodhibitiwa, itafika mahali tutakuja kutumbukia katika shimo refu la maangamizi. Tafakari.

spot_img

Latest articles

Luhemeja ashuhudia zoezi la usafirishaji Ziwa Victoria

KATIBU Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mha. Cyprian Luhemeja akifuatilia...

Mfalme Zumaridi ashikiliwa na Polisi

Na Mwandishi Wetu Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limesema linamshikilia na kumhoji Diana Bundala...

More like this