Jengo makao makuu ya mahakama liongeze kasi, ari ya upatinakaji haki

JUMAMOSI ya wiki iliyopita, yaani Aprili 5, 2025 kuna jambo kubwa lilitokea jijini Dodoma. Hili ni la uzinduzi wa Makao Makuu ya Mahakama Tanzania. Kwa mara ya kwanza katika historia ya uhuru wa taifa hili, Mahakama ilipata jengo la makao yake makuu. Uzinduzi wa jengo hilo linalobeba sifa nyingi za kipekee, ulifanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Siku chache kabla ya uzinduzi huo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Profesa Elisante Ole Gabriel alikuwa ameweka hadharani sifa za jengo hilo ambazo alisema ni pamoja na ukubwa wake ambao unaelezwa kuwa litakuwa ni jengo la kwanza la makao makuu ya mahakama kwa ukubwa barani Afrika na la sita duniani. Alieleza kuwa jengo la kwanza kwa ukubwa la makao makuu ya mahakama liko barani Asia likiwa na ukubwa wa mita za mraba 147,000, hakutaja liko nchi gani.

Sifa zaidi za jengo hilo la kisasa kabisa lenye sakafu (floor) tisa kila moja ikiwa na mita za mraba 8,100, zikiunganishwa zinakamilisha ukubwa wa mita za mraba 63,244; kuwa lina eneo la kutua helikopta juu yake; likiwa limeunganishwa na mahakama zote nchini kwa mfumo wa tekinolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) na linakadiriwa kuwa litadumu kwa miaka 100 ijayo. Gharama ya ujenzi wa jengo hili ni Sh bilioni 185, fedha ambazo zinatokana na kodi ya wananchi. Hakuna mkopo katika ujenzi huo. Jengo hili linaelezwa kuwa na miundombinu ya kisasa kabisa ya TEHAMA ambayo inawezesha kutumika kwa akili mnemba au akili unde (AI) katika kufanikisha utendaji kazi wa mahakama Tanzania.

Hata hivyo, taarifa za mitandao zinaonyesha kuwa ​jengo kubwa kuliko yote duniani la makao makuu ya mahakama ni New Palace of Justice lililoko Kuwait, likiwa limekalia eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 356,189 kwenye jengo lenye sakafu 25.

Katika kuonyesha mafanikio ya Mahakama Tanzania, Profesa Ole Gabriel alisema kuanzia mwaka 2021 Rais Samia alipoingia madarakani idadi ya vituo jumuishi vya mahakama nchini ambavyo vina ngazi tano za mahakama, yaani kuanzia mahakama ya mwanzo, mahakama za wilaya, mahakama ya hakimu mkazi, mahakama kuu na mahakama ya rufani, vimeongezeka sana. Alitaja kuwa sasa kuna mahakama za mwanzo 960, mahakama za wilaya ziko 136 kwa maana kwamba ni wilaya tatu ambazo mahakama hizo hazijakamilika katika wilaya zote 139 za Tanzania na ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi. Aidha, mahakama za hakimu mkazi ziko 30 zaidi ya idadi ya mikoa ya Tanzania Bara ambayo ipo 26, mahakama kuu 20 na mahakama ya rufani moja.  

Huwezi kupuuza ukweli kwamba kupatikana kwa makao makuu ya mahakama katika jengo moja kubwa jipya ni hatua kubwa kwa nchi. Aidha, ni hatua ambayo ilichelewa sana kufikiwa kwa nchi inayojiendesha kwa mfumo wa mgawanyo wa madaraka baina ya mihimili ya dola, yaani serikali, bunge na mahakama. Ingawa jengo lililoko barabara ya kivukoni Dar es Salaam, lilikuwa linatumika kama makao makuu ya mahakama, halikutosheleza mahitaji pamoja na hadhi ya muhimili huo wa dola, hasa inapolinganishwa na makao makuu ya mihimili mingine kama ikulu ya Dar es Salaam au ya Chamwino, Dodoma; au na jengo la Bunge jijini Dodoma. Ni dhahiri, mahakama ilihitaji jengo hili muda mrefu sana uliopita. Hatua hii ni ya kupongeza.

Katika uzinduzi huo pia zilizinduliwa nyumba za makazi ya majaji jijini Dodoma. Taarifa zinaeleza kwamba nazo ni nyumba za kisasa ambazo zitasaidia kuwapatia majaji makazi mazuri na utulivu. Mambo haya ni ya kupongeza kwani ni matumizi mazuri ya fedha za umma. Majengo haya iwe ni makazi au ofisi za mahakama ni mali ya umma, hakuna atakayeondoka nazo. Yatatumiwa na Watanzania walioko leo na watakaozaliwa baadaye. Yatawabeba majaji walioko sasa na watakaokuja baadaye. Ujenzi wa nyumba hizi za makazi ya majaji unaondoa kero ya ukosefu wa makazi ya hadhi ya majaji nchini, hasa ikikumbukwa kwamba miaka ya mwanzoni mwa 2000 nyumba nyingi za serikali kati ya chache zilizokuwako ziliuzwa kwa watumishi wake nchini kote.

Wakati Watanzania wakifurahia matunda haya ya makao makuu ya mahakama, wanapaswa pia kuwa na mawazo je, baada ya kupatikana kwa ofisi hizi na makazi, ni kwa kiasi gani yatasaidia kupatikana kwa huduma bora za mahakama nchini yaani upatikanaji wa haki mbele ya vyombo vya sheria?

Kwa miaka mingi nchini kumekuwako na kilio cha haki za raia kutokupatikana itakiwavyo. Mosi, haki hazipatikani kwa wakati. Hii inatokana na kesi nyingi, hasa za jinai, kuchukuwa muda mrefu kusikilizwa kwa sababu mbalimbali. Mojawapo, ni uhaba wa mahakimu na majaji. Lakini pia, kutokana na urasimu tu ambao kimsingi hauna maaana sana mahakamani.

Kuna tatizo kubwa pia la haki za watu kukanyagwa. Yapo malalamiko mengi ya wananchi kupokwa haki zao mahakamani kwa visinzio mabalimbali. Kwa mfano, juzi akizindua jengo hilo, Rais Samia alisema kuwa siyo sawasawa kwa wananchi kupoteza haki kwa sababu ya makosa ya kiufundi.

Ni matarajio ya Watanzania kwamba wakati miundombinu ya mahakama inaimarishwa, vivyo hivyo kiwango cha kupatikana kwa haki kwa wananchi nacho kinapaswa kuongezeka. Ikiwezekana habari ya watu kukaa mahabusu kwa miaka na miaka iwe historia nchini au kesi kusikilizwa kwa miaka na miaka iwe historia pia.

Kwa mfano Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani mtu anakamatwa na kuwekwa mahabusu na hata kufikishwa mahakamani kwa makosa ambayo upelelezi wake haujakamilika. Maelezo ya waendesha mashitaka mahakamani kwamba eti upelelezi wa kesi haujakamilika huku watu wakisota rumande, ni visingizio vya kawaida kabisa vya kukanyanga haki za raia.

Mfumo huu wa kuendesha kesi za jinai umekuwa chanzo kikubwa cha watu kuteseka na kuumizwa kwa kuwa tu wametuhumiwa kwa makosa ambayo hawakutenda. Ingeliwezekana kabisa mashitaka yakafunguliwa kwa wale tu ambao kwa uhakika upelelezi dhidi ya tuhuma zao umekamilika na kuna uwezekano wa washukiwa kutiwa hatiani.

Kwa mujibu wa taarifa ya haki za binadamu nchini kwa mwaka 2023 iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) katika utafiti uliofanywa kwenye mikoa 20 ya Tanzania Bara kuhusiana na upatikanaji wa haki, asilimia 78 ya wananchi walieleza kuwa rushwa ni kikwazo kikubwa cha kupatikana kwa haki. Vyombo vya dola, hasa polisi na maofisa wa mahakama walitajwa kuwa miongoni mwa watumishi wa umma wanaodai rushwa ili kutoa haki kwa raia au kupindisha utoaji wa haki hiyo. Kadhalika, asilimia 49 ya wananchi waliohojiwa pia walisema kikwazo kingine cha haki ni kesi kuchukuwa muda mrefu kukamilika mahakamani; uelewa mdogo wa sheria kwa asilimia 48 na asilimia 39 ilielezwa ni kikwazo cha gharama kubwa za kuweka mawakili katika kesi zao. Yote haya yanachangia kukanyagwa kwa haki za raia katika kufikia haki zao mahakamani. Katika vikwazo hivi mahakama imo!

Wakati Watanzania wakifurahia na kusherehekea ufunguzi wa jengo kubwa la makao makuu ya mahakama Tanzania, pia ijulikane kuwa ujumbe kwa mashangilio haya ni lazima sasa uakisi kupatikana kwa haki za wananchi. Ndiyo kusema kwamba jengo jipya la makao makuu ya mahakama ni vema ukaakisi shida na mahitaji ya jamii katika kupata haki zao kwa wakati bila vikwazo.

spot_img

Latest articles

Luhemeja ashuhudia zoezi la usafirishaji Ziwa Victoria

KATIBU Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mha. Cyprian Luhemeja akifuatilia...

Mfalme Zumaridi ashikiliwa na Polisi

Na Mwandishi Wetu Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limesema linamshikilia na kumhoji Diana Bundala...

More like this