Na Mwandishi Wetu
UTOAJI wa huduma za afya nchini Tanzania kwa kipindi cha 2020/25 umeendelea kuimarika kutokana na jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanywa na serikali ya awamu ya sita kwa kushirikiana na wadau wa sekta binafsi, ambapo vituo vya huduma za afya nchini kutoka Vituo 8,458 mwaka 2020 hadi vituo 9, 826, Februari 2025.
Akitoa Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Bunge leo Aprili 09, 2025, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameliambia Bunge kwamba Hospitali zinazotoa huduma za magonjwa ya dharura nazo zimeongezeka kutoka saba mwaka 2020 hadi 116 mwaka 2025 huku pia vituo vya afya vyenye majengo ya Mama na Mtoto vikiongezeka kutoka 6,081 mwaka 2020 hadi 7,397 Februari mwaka huu.

“Kutokana na jitihada hizo vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2020 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000 Februari, 2025 na vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano vimepungua kutoka 67 mwaka 2020 hadi 43 Februari, 2025,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Ameeleza kuwa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi zimeendelea kuimarika ambapo kwasasa zinapatikana kwenye hospitali za rufaa za Mikoa zinazotoa huduma nane za kibingwa ambapo hapo awali zilikuwa zinapatikana katika ngazi ya Kanda.

“Huduma hizo za matibabu ni pamoja na afya ya uzazi na magonjwa ya wanawake, afya ya watoto, magonjwa ya ndani, upasuaji, upasuaji wa mifupa na ajali, huduma za dharura, huduma za mionzi, huduma za ganzi na dawa za Usingizi,” ameeleza Majaliwa.

Aidha amesema kuwa upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya kisasa na bidhaa za afya nchini vimeimarika kutoka asilimia 73 mwaka 2020 hadi asilimia 89.3 Februari mwaka huu, mafanikio ambayo yameendelea kuvutia wagonjwa kutoka nje ya nchi na kuimarisha tiba utalii ambapo hadi Februari 2025, wagonjwa 7, 843 kutoka nje ya nchi wametibiwa ikilinganishwa na wagonjwa 5,705 wa mwaka 2020.