ASKOFU wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dk. Benson Bagonza, katika moja ya maandishi yake wiki hii amesema kuna mambo 10 hayako sawa nchini. Miongoni mwa mambo hayo 10 ametaja mojawapo kuwa ni “Mbuzi akipotea anapatikana, lakini mtu akipotea hapatikani.” Kauli ya Askofu Bagonza inabeba ujumbe mzito juu ya usalama na haki za wananchi wa Tanzania.
Kauli ya Askofu Bagonza inatoka wakati ambao bado taifa hili linaendelea kushuhudia wimbi la watu kupotea katika mazingira ya kutatanisha. Matukio haya awali yalionekana kuwa ni halali kwa wale wote walioonekana kufungamana na siasa za vyama vya siasa ambavyo haviko madarakani. Hata hivyo, mawanda ya wanaopotea sasa yamepanuka na kuwagusa hata wale wa chama tawala, CCM.
Kwa mfano, Machi 23, 2025 takribani siku 10 zilizopita Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, Daniel Chonchorio Nyamhanga (46) anadaiwa ‘kutekwa’ na watu wasiojulikana. Taarifa kutoka kwa wanafamilia zinasema kuwa ndugu yao alifuatwa nyumbani kwake jijini Mwanza na watu wanne walikuwa na gari na kisha kuondoka naye. Tangu siku hiyo hadi sasa haijulikani aliko.
Tukio la Nyamhanga linatokea siku chache tu baada ya kupotea kwa Katibu wa Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Mwanza, Amani Manongelo. Kada huyo anadaiwa kupotea tangu siku ya wapendao Februari 14, 2025. Hadi sasa hakuna mwenye taarifa za aliko kada huyo.
Matukio haya yanatokea miezi saba baada ya kupotea kwa makada wengine wa Chadema jijini Dar es Salaam. Makada hao, Jacob Mlay wa Chadema Katibu Temeke; Deusdedit Soko, Katibu Bavicha Temeke na mwanachama wa Chadema, Frank Mbise, wanadaiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha. Hata hivyo, chama hicho kimekuwa kikilituhumu Jeshi la Polisi kuwa na mikono katika kupotea kwa viongozi hao. Viongozi hao walipotea kipindi kimoja na tukio la kutekwa na kisha kuuawa kikatili kwa aliyekuwa mjumbe wa sektretariati ya Chadema, Ally Kibao. Kibao alitekwa akiwa kwenye basi akisafiri kwenda Tanga. Inadaiwa kwamba watekaji waliosimamisha basi hilo kwa kulizuia kwa magari mawili mbele na nyuma, ni wanausalama ambao walikuwa na silaha zinazotumiwa na vyombo vya ulinzi vya ndani ya nchi. Walimfunga pingu Kibao na kisha kuondoka naye. Baada ya siku moja mwili wake ulikutwa Ununio Dar es Salaam, ukiwa umeharibiwa sana uso kwa tindikali.
Matukio haya yanaogofya. Siyo mazuri. Hayaleti picha nzuri kuhusu uhuru na usalama wa wananchi kwa ujumla wake. Ni mambo ambayo kwa asili siyo utamaduni wa Kitanzania. Yaani kuteka watu, kupoteza watu na hata kuua siyo mambo ya kawaida katika jamii ya Kitanzania. Baya zaidi, kwamba kuna watu wenye uwezo wa kuteka, kupoteza na kuua watu, lakini hawajulikani, siyo jambo linaloingia kwa urahisi katika akili za wengi.
Polisi mara nyingi wamenukuliwa wakisema kuwa uchunguzi wa matukio hayo unaendelea na kuomba ushirikiano wa wananchi kubaini wanaofanya matukio haya.
Wiki iliyopita kulikuwa na taarifa kutoka Haiti kwamba mmoja wa askari wa kikosi cha Kenya ambao wamepelekwa huko kusaidia kurejesha amani, hajulikani aliko. Baada ya kukamatwa na magenge ya wahalifu ambayo yamefanya Haiti isitawalike. Hata hivyo, taarifa za baadaye zilithibitisha kwamba askari huyo, alikuwa amekwisha kuuawa. Magenge ya wahalifu huko Haiti yamekuwa ni tatizo kubwa linalosumbua nchi hiyo kiasi cha kuomba jamii ya kimataifa msaada wa vikosi vya ulinzi kutoka Umoja wa Mataifa ili kusaidia juhudi za kurejesha amani nchini humo.
Nimefanya rejea ya magenge haya ya Haiti siyo kwa sababu Tanzania imefikia kiwango hicho cha uhalifu, ila kuonyesha kwamba iko hatari kubwa kwa usalama wa nchi kama watu wanaoendesha uovu kama huu wa kuteka watu na hata kuua, kama hakuna hata mmoja ambaye amewahi kukamatwa na kushitakiwa.
Ni bahati mbaya kama taifa pamoja na kauli za polisi kwamba wanawasaka wahusika wa matendo haya maovu ya kinyama dhidi ya binadamu wengine, kwamba matukio haya yanataka kuzoeleka. Kwamba sasa akitekwa mtu siyo jambo la kushitua sana tena, labda wanafamilia tu ambao ndugu yao ama amepotea au ametekwa au kuuawa ndiyo wanaonekana kusumbuka zaidi. Kuna hatari ya kuzoea hali hii ya watu kutekwa, kupotea au kuuawa. Hali hii ikifikia kiwango hicho, ni dhahiri amani ya taifa hili inamomonyolewa.
Kwa kawaida uhalifu hauchagui itikadi, dini, kabila, jinsia au umri. Tabia ya uhalifu ikishakomaa na kuota mizizi katika jamii, huathiri kila mmoja. Hii ni sawa na ule usemi kwamba ‘mtego hukamata waliomo na wasiokuwamo’ kwa maana hiyo, kuacha uovu na uhalifu uendelee kutokea nchini ni kutoa fursa kwa hali hiyo kuota mizizi na kukomaa. Uhalifu ukishakomaa kwa kiwango hicho kazi ya kuutokomeza inakuwa ni ngumu na nzito.
Wakati vitendo hivi vya kuteka watu na kuwapoteza na wengine kukutwa wamekwisha kuuawa vilipoanza kushika kasi tangu mwanzoni mwa mwaka 2016, ilidhaniwa ni mambo ya kupita tu. Ilionekana kama ni upepo tu. Kwamba utapita. Leo ni mwaka 2025 vitendo hivyo vinazidi kujitokeza.
Mwaka jana Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kiliweka hadharani orodha ya watu 83, kikisema ama wamekamatwa, kutekwa na kuteswa kiholela na kueleza wasiwasi wao huenda Jeshi la Polisi linahusika na vitendo hivyo. Mbali ya kusikitishwa na kulaani vitendo hivyo ambavyo kwa maoni yao vyombo husika vya dola vimeshindwa kuwajibika ipasavyo, walimshauri Rais Samia Suluhu Hassan kuunda Tume maalumu ya kuchunguza matukio yote ya kupotea kwa watu, kutekwa na kuteswa.
Aidha, TLS walimshauri Rais Samia kuunda Tume Maalum ya kuchunguza ushiriki wa Jeshi la Polisi kwenye masuala ya Utekaji kwa kuwa limekuwa likituhumiwa kushiriki katika
vitendo hivyo; na pia walipendekeza kuundwa kwa chombo maalumu cha kudumu cha kuangalia utendaji wa vyombo vya dola (oversight body) ili kuhakikisha vinafanya kazi kwa mujibu wa Katiba na Sheria.
Mapendekezo haya tangu yatolewe ni zaidi ya miezi saba sasa, ni vigumu kusema kuwa kuna hatua zimechukuliwa kutekeleza lolote kati ya hayo. Hata hivyo, kwa matukio ya Mwanza ya hivi karibuni ni kielelezo kingine kwamba bado kile ambacho kwa muda sasa kimekuwa kikilalamikiwa na watu kuhusu utekaji na kupotea/kupotezwa kwa watu ni matukio ambayo yanaendelea kutokea nchini. Bahati mbaya sana ni kwamba waendesha matendo haya, hawajawahi kukamatwa. Hawajulikani. Hawajaacha. Polisi ni kama wameingia baridi kuwakabili.
Watanzania wanajua kwamba Jeshi la Polisi ni chombo madhubuti, lina mbinu, maarifa na uwezo mkubwa wa kuchunguza uhalifu wowote na kuwatia mbaroni wahusika wote. Lina zana za kuwawezesha kufanya hivyo, lina mtandao wa ndani na wa kimataifa wa kushirikishana katika kufanya kazi hiyo, hata kama uhalifu huo utakuwa umevuka mipaka ya nchi hii. Kwa nini hatua hazionekani zikichukuliwa kukabili uhalifu huu kama ambavyo ni matamanio ya wengi, ni swali ambalo wenye majibu ni polisi wenyewe.