YAMEKUWAPO mapendekezo mengi ya kuboresha mfumo wa kuendesha siasa za Tanzania kwa kitambo sasa. Mapendekezo haya ni pamoja na matamanio ya kuruhusiwa kwa mgombea binafsi katika uchaguzi. Pendekezo la kuruhusiwa kwa mgombea binafsi limekabiliwa na upinzani mkali sana kutoka kwa watawala wa nchi hii kwa miongo kadhaa sasa.
Harakati za kutaka nchi iwe na mgombea binafsi siyo tu imehusu harakati za ndani ya nchi, bali pia vyombo vya kimataifa kama Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu ambayo ilitoa hukumu ya kuitaka Tanzania kuruhusu uwepo wake. Hukumu hiyo ilitokana na maombi yaliyopelekwa kwenye mahakama hiyo yakiwasilishwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) pamoja na Marehemu Mchungaji Christopher Mtikila mwaka 2013.
Mbali na hukumu ya Mahakama ya Afrika, pia kumekuwako maoni ya kutaka iwepo fursa ya mgombea binafsi katika mfumo wa uchaguzi nchini. Mapendekezo haya yamekuwapo tangu kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 pamoja na tume nyingine zilizoundwa ikiwapo ya Jaji Joseph Warioba ya Katiba Mpya ya mwaka 2012. Licha ya kuwapo kwa maoni haya kwa kitambo sasa, bado suala la mgombea binafsi limeendelea kuwa gumu kutekelezwa katika mfumo wa uchaguzi nchini.
Wapinzani wa hoja ya mgombea binafsi kwa muda sasa wamekuwa na hoja yao dhidi ya mfumo huo. Kwamba mgombea binafsi siyo taasisi, kwa maana hiyo hawezi kudhibitiwa kama ilivyo mfumo wa wagombea kupitia vyama vya siasa.
Mvutano ambao umetanda katika hoja ya mgombea binafsi umejengwa kwenye dhana kuwa haki ya kushiriki shughuli za kisiasa, hasa kwa kuchaguliwa, ni miongoni mwa haki za binadamu ambayo kuimilikisha haki hiyo taasisi inayoitwa chama cha siasa ni kuvunja haki za binadamu. Hukumu ya Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika ambayo ilitoa ushindi kwa LHRC na Marehemu Mtikila, ilikuwa ni mwendelezo tu wa kiu ya kutakiwa mgombea binafsi nchini. Awali ilikuwapo kwa hukumu nyingine ya mahakama kuu iliyokuwa imehalalisha mgombea binafsi. Hii ni baada ya mwaka 1993 Mchunguaji Mtikila kufungua shauri la kikatiba katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma lililosikilizwa na Jaji Kahwa Lugakingira, akitaka mahakama hiyo itamke kwamba mgombea bnafsi ni haki ya kila raia wa Tanzania kwa mujibu wa katiba. Kwamba haki hiyo ni pamoja na kuchagua na kuchaguliwa na kuifungamanisha na chama cha siasa ni uvunjaji wa haki yenyewe. Jaji Lugakingira alikubaliana na madai ya Mtikila.
Hata hivyo, kwa kuwa mgombea binafsi imekuwa ni hoja isiyopendwa na watawala, mwaka 1994 serikali iliwasilisha bungeni mabadiliko ya 11 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na katika ibara ya 39 na 67 waliweka sharti ya kugombea nafasi za kuchaguliwa (urais na ubunge) kwamba ni lazima mgombea atokane na chama cha siasa. Mtikila alipinga mabadiliko hayo Mahakama Kuu kwa kufungua kesi iliyosikilizwa na jopo la majaji watatu, Amir Manento, Salumu Massati na Thomas Mihayo. Kimsingi ukisoma hoja za majaji baada ya kusikiliza pande mbili, Jamhuri na Mtikila, waliona mantiki ya hoja za mleta shauri, lakini waliepa njia ya kutamka kuwa mabadiliko hayo yanakiuka katiba. Walishikilia kuwa mabadiliko ya katiba ni mchakato wa kisiasa, ambayo ni mamlaka ya bunge, wakishauri njia hiyo itumike kurekebisha lolote alilokuwa anaomba mleta shauri.
Ukisikiliza hata kile walichosema wajumbe wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2022 na 2024, ni mapendekezo ya kufanyika kwa marekebisho madogo ya katiba. Marekebisho hayo ni ya kuwapo kwa Tume Huru ya Uchaguzi na mgombea binafsi. Mambo hayo yafanyike kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu wa 2025.
Madai ya kutaka kuwapo kwa mfumo wa kisiasa unaoruhusu mgombea binafsi yamekuwako kwa miongo mitatu na ushei sasa, lakini ni dhahiri siyo jambo ambalo wenye mamlaka wanalipenda au kuliunga mkono. Ndiyo maana kila vyombo vya kulinda haki za raia vinapotoa uamuzi wa jambo hilo, serikali imetafuta upenyo wa kutokutekeleza maamuzi ya mahakama, za ndani na nje.
Hata hivyo, hofu ya mgombea binafsi inatokana na nini hasa tunapotafakari mabadiliko makubwa ya uendeshaji wa shughuli za kisiasa nchini kwa sasa? Kwa mfano, ukitafakari jinsi kampeni za mwaka 2015 za Chama Cha Mapinduzi (CCM) zilivyokuwa zinaendeshwa chini ya mgombea wao wa urais, Marehemu John Magufuli. Kwamba mabango yake kwa kiwango kikubwa hayakuakisi chama chake, yalijitokeza kama yeye ni yeye. Ni kweli kwa kiwango kikubwa kampeni zilikuwa zinaratibiwa na chama; ni kweli alikuwa anavaa sare za chama chake; ni kweli pia alikuwa amebeba ilani ya chama chake. Lakini kwa kiasi kikubwa alikuwa anajizungumzia yeye. Alikuwa anatamka kuwa serikali yake atakayoiunda.
Jumatatu ya wiki hii, yaani Machi 17, 2025 Watanzania walikumbuka miaka minne ya kifo cha Magufuli. Wapo waliokwenda makanisani kumkumbuka. Wamefanya jambo jema, huyu alikuwa kiongozi wa nchi, na alikufa angali madarakani. Hata hivyo, yafaa kukumbuka kwamba tangu kuingia madarakani kwa Magufuli mwaka 2015 na aina ya utawala aliokuja kutuonyesha, dhana ya mgombea binafsi imejitokeza katika picha tofauti.
Kwamba tangu mwaka 2015 kila kitu cha serikali kimegeuzwa kuwa cha rais aliyeko madarakani. Kila kitu kinachofanywa na serikali, ni cha rais. Ukisikiliza hotuba za viongozi wote, kuanzia kwa makamu wa rais, nenda kwa waziri mkuu, pita kwa mawaziri, gusa wakuu wa mikoa, chungulia kwa wakuu wa wilaya na kwa watendaji wengine wote, lugha ni moja, fedha ni za rais, miradi ni ya rais kila kitu kinanasabishwa na rais kwa jina. Kwamba mradi wa maji kaleta rais, shule ikijengwa mahali kajenga rais, kituo cha afya kikijengwa mahali kajenga rais. Mwelekeo ni mpya, kufungamanisha kila kitu na rais. Fedha ni za rais, hata wabunge ambao wanajua fika kwamba mchakato wa serikali kupata fedha unakuwaje, nao wanasema fedha ni za rais.
Tunapokuwa na matamanio ya kufungamaisha kila kitu cha umma au cha serikali na mtu mmoja, hivi tunakuwa na hofu gani basi ya kuwa na mgombea binafsi? Kama tangu mwaka 2015 mwelekeo wetu kama taifa ni wa kupambana kukuza ‘mtu’ na siyo taasisi, hofu yetu ya kuwa na mgombea binafsi inakuwa na mashiko gani tena?
2025 ni mwaka wa uchaguzi mkuu ambao Watanzania wanakwenda kuwachagua viongozi wao kisiasa katika vyombo vya dola, madiwani, wabunge na rais. Ni kwa kiasi gani dhana hii ya kubinafsisha vitu vya umma inakwenda kutuathiri katika uchaguzi huu? Inawezekana tunapenda taasisi za umma kama vyama vya siasa kwa nia ya kudhibitiana kwa kitambo kidogo tu, hasa katika mchakato wa kuwania madaraka, lakini baada ya hapo pengine taasisi hizi zinakuwa hazipewi umuhimu mkubwa sana kama unaoelekezwa kwa ‘mtu’ katika nyakati za sasa.
Ni katika kutafakari uhalisia wa mambo ulivyo leo, kama wapinzani wa hoja ya mgombea binafsi bado wanaona mantiki yoyote ya kuendelea na msimamo wao, hata kama kinachoonekana sasa ni kuenzi watu kuliko kujenga taasisi imara ili tuwe na utawala bora ndani ya nchi yetu.