Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi amesema waandishi wa habari watakaothibitishwa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari watalindwa kutokana na manyanyaso ama vitisho wawapo kwenye majukumu yao.
Profesa Kabudi ameyasema hayo leo Machi 3, 2025 mkoani Dar es Salaam, wakati akizindua Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari.
Profesa Kabudi amesema kuwa waandishi wa habari wakitambuliwa pia hakutakuwa na upotoshwaji wa habari, kwani watakuwa wanalindwa na weledi chini ya usimamizi wa Bodi ya Ithibati.
Amesema waandishi watakaothibitishwa watakuwa wanawajibika kwa bodi na pia watalindwa wakati wote watakapotekeleza majukumu yao iwe kwenye mazingira hatarishi ama nyakati za uchaguzi.

Ameongeza kuwa bodi pia itahakikisha inausimamia Mfuko wa Waandishi wa Habari ili waweze kupatiwa mafunzo kwa ajili ya kuandaa maudhuni ya ndani (local Content), yenye mvuto ambayo yatashindanishwa na maudhui mengine ya kimataifa.
Profesa Kabudi amesema utafiti ndio nguzo kuu kwa waandishi wa habari, hivyo Mfuko wa Waandishi wa Habari utawawezesha waandishi hao kupata mafunzo kuhusu kufanya utafiti ili kuwa na maudhui yenye mvuto kwa jamii.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema uwepo wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari hauna lengo la kufanya watu wazuiwe kuingia katika tasnia hiyo bali inalenga kupatikana kwa Huduma bora.

“Utafiti tulioufanya hivi karibuni tulibaini Vyuo vyetu vinazalisha zaidi ya Waandishi wa Habari 500 kila Mwaka. Kusoma ni jambo moja lakini Watu hao wanahitaji kujengewa uwezo ili kuwa na ubora wa kufanya kazi iliyo bora.
“Hiyo inaonesha kuna ongeko la Vijana katika tasnia na wengi wao wana Shahada ya Habari, unadhani watakwenda wapi? Hivyo, uwepo wa Bodi ya Ithibati utasaidia wawe bora na kinachozalishwa kiwe bora pia. Kama Vyuo vinazalisha, unadhani wakitoka hapo watakwenda wapi? Lazima tushirikiane kuwasaidia,” amesema Msigwa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari nchini, Tido Mhando amesema kuanza kazi kwa bodi hiyo sasa ni rasmi kufanya kazi kwa ukanjanja kutakuwa kumekufa.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa vitendea kazi vya kuiongoza bodi hiyo, Tido amesema kumekuwa na kuporomoka kwa maadili ya waandishi wa habari kunatokana na kukosekana kwa usimamizi wa taaluma ya habari.

Tido ameongeza kuwa bodi itazingatia sheria na miongozo iliyopo ili kutekeleza majukumu yake kwa lengo la kutatua changamoto zinazowakabili waandishi wengi wa habari hapa nchini.
Amesema bodi itafanya kila njia kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao na kuleta matokeo chanya kwenye tasnia ya habari.

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile amesema uzinduzi wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari ni mwanzo wa kupatikana kwa Baraza Huru la Habari hapa nchini.

Balile amesema kukiwa na Baraza Huru la Habari usimamizi wa kazi za wanahabari utakuwa rahisi, na hata kesi zinazohusu taaluma hiyo zitaamuliwa na Baraza na sio mahakamani tena.
Amesema Baraza Huru la Habari litarahisisha usimamizi wa sekta ya habari na litalinda maslahi ya waandishi wa habari dhidi ya watu wenye nia ovu na sekta hiyo.