Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali imedhamiria kumaliza matatizo ya kiafya wanayokabiliana nayo Wananchi wanaoishi katika Visiwa Vidogovidogo kwa kufikishwa katika matibabu kwa wakati ili kupunguza vifo vinavyoweza kuepukika ikiwemo vya akinamama na watoto.
Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo baada ya kuzindua Boti za kubeba Wagonjwa wakati wa dharura hafla iliofanyika Verde Mtoni , Wilaya ya Mjini , Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amesema kuwa, Boti hizo ni sehemu ya uimarishaji wa huduma za dharura na mfumo wa wa Rufaa kwa Wagonjwa wanaotoka kwenye Visiwa wanaopewa Rufaa kutoka Vituo vya Afya kwenda Hospitali za Wilaya, Mkoa na Taifa.
Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa Serikali imeamua kuzipeleka Boti hizo katika maeneo yenye changamoto kubwa zaidi na kwengine kutafanyiwa utaratibu wa Haraka baadae.

Aidha, Dkt. Mwinyi ameishukuru Benki ya Dunia kwa kusaidia gharama za Ununuzi wa Boti Tano ambazo tatu tayari zimekamilika na mbili zitakamilika muda mfupi Ujao.

Naye Waziri wa Afya Nassor Ahmed Mazrui amewahakikishia Wananchi wanaoishi katika Visiwa huduma za ihakika zitakazoanza hivi karibuni na kuwa tayari kuzitumia huduma hizo hususan akina Mama na watoto.Boti hizo zimegharimu takribani Shilingi Bilioni 2 na zimetengenezwa na Kampuni ya QIRO GROUP LIMITED.
