Na Mwandishi Wetu
WATOTO pacha Hassan na Hussein Jummane (3) wakazi wa Igunga mkoani Tabora, waliozaliwa Agosti 2021 wakiwa wameungana wameruhusiwa rasmi leo wameruhusiwa rasmi kurudi nyumbani kwao.
Watoto hao kwa walikuwa wameungana kwa kiasi kikubwa kwenye nyonga, kifua, tumbo, miguu mitatu, kibofu cha mkojo, utumbo na sehemu ya maumbile na Oktoba 5, 2023 kufanyiwa upasuaji wa kutenganishwa nchini Saudi Arabia na kurejea nchini Disemba 2024 kisha kupokelewa Hospitali ya Taifa Muhimbili,
Akizungumza na vyombo vya habari kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Dkt. Julieth Magandi amesema, watoto hao walipokelewa hospitalini hapo Agosti 2021 kutokea Igunga Tabora wakiwa na umri wa siku 14 na kukaa hospitalini hapo miezi 11 wakipata matibabu mbalimbali ya kuwaimarisha na kisha kuondoka kwenda nchini Saudi Arabia kwa ndege maalum Agosti 23, 2023 ili kufanyiwa upasuaji mkubwa wa kuwatenganisha.

Dkt. Magandi ameishukuru Serikali ya Saudi Arabia kwa msaada huo ambao umewarejesha watoto hao katika maisha ya kawaida.
“Baada ya upasuaji walipokelewa Hospitalini hapa tangu Disemba, 2024 kwa ajili ya uangalizi na kufanya maandalizi ya kina kupitia Serikali ya Mkoa wa Tabora ili kuwapokea na kuwatunza kwani bado wanaendelea na matibabu ya awamu mbalimbali ili kuboresha ustawi wa maisha yao ambapo MNH imewanunulia zawadi mbalimbali za kwenda kuanza maisha,” amesema Dkt. Magandi.

Naye Daktari Bingwa Mbobezi wa Upasuaji Watoto wa MNH, Dkt. Zaituni Bokhary ambaye pia atawasindikiza Igunga amesema, kutokana na namna watoto walivyokuwa wameungana, ilihitaji utaalam wa juu zaidi hivyo Serikali ya Saudi Arabia ilichukua jukumu la kuwasafirisha, kuwafanyia upasuaji kwenye hospitali ya King Abdulaziz iliyopo Riyadh Saudi Arabia, uliodumu kwa saa 16.
Amesema upasuaji huo ulishirikisha jopo la madaktari wabobezi upasuaji wa mishipa ya fahamu, mfumo wa mkojo wa watoto, mfumo wa ini na chakula.
Dkt. Bokhary amesema baada ya upasuaji huo, kila mmoja ana mguu mmoja na wataendelea na matibabu baada ya mwaka mmoja ambapo watarudi nchini Saud Arabia kurekebishiwa baadhi ya viungo na mara tu watakapofikisha miaka mitano kila mmoja atatengenezewa mguu wa bandia ili kuwawezesha kutembea vizuri na kufanya shughuli zako kama kawaida.
Kwa upande wake mama wa watoto hao, Hadija Shabani ameishukuru Serikali ya Saudi Arabia kwa msaada wa matibabu ya kutenganisha watoto hao pamoja na Serikali ya Tanzania kwa jinsi ilivyoratibu zoezi hilo, watoa huduma wote wa MNH, na Serikali mkoani Tabora kwa maandalizi mazuri ya kuwapokea.
