MAHAKAMA ya Kijeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imetoa hati ya kukamatwa kwa kiongozi wa umoja wa makundi ya waasi nchini humo ya Alliance Fleuve Congo (AFC/M23), Corneille Nangaa.
Shirika la Habari la AP limeripoti leo Februari 7, 2025, kuwa mahakama ya kijeshi nchini humo imetoa hati Nangaa akamatwe akituhumiwa kuhusika katika kile ilichotaja kuwa ni uasi na uhalifu wa kivita dhidi ya raia nchini humo.

Televisheni ya Taifa ya DRC nayo iliripoti kuwa hati ya kukamatwa kwa Nangaa imetolewa Jumanne Februari 4, 2025, baada ya kuhusika katika mauaji ya maelfu ya raia katika mapigano yaliyoibuliwa na wapiganaji wake katika Jimbo la Kivu Kaskazini nchini humo.
Mahakama hiyo katika hati yake imesema kutekeleza mauaji ya raia katika mapigano hayo ni kinyume cha sheria za nchi na sheria za kimataifa.Imeamuru Nangaa akamatwe akiwa mahali popote atakapokutwa duniani na kufikishwa katika Mahakama ya kijeshi nchini DRC.