Rwanda, Uganda, M23 watia kiza Jumuiya Afrika Mashariki

TUPO mwezi wa pili tu wa mwaka 2025, lakini kuna kila dalili kwamba unakwenda kuwa mwaka wenye machungu mengi kwa ustawi wa maisha ya watu wengi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwa sasa moto unawaka ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutokana na vita vinavyoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (RDC). Rwanda ambayo imetuhumiwa kwa miongo kadhaa sasa kuwa ndiyo inawaunga mkono ‘waasi’ wa M23 (March 23 Movement) imejikuta katika malumbano makubwa ya kidiplomasia na DRC, Afrika Kusini, Angola na hata Kenya.

Rais Paul Kagame wa Rwanda amekuwa kwenye vyombo vya habari vingi ndani ya wiki moja iliyopita, akijitetea kuwa nchi yake haina jeshi DRC na kwamba M23 siyo Wanyarwanda bali ni raia wa DRC wanaopigana kujitetea dhidi ya maamuzi ya serikali ya nchi hiyo ya kuwakataa kwamba ni raia.

Mapigano ya mwezi uliopita ya mashariki mwa DRC hasa katika mji wa Goma yameacha maafa makubwa baada ya ‘waasi’ wa M23 kupambana na vikosi vya serikali ya nchi hiyo pamoja na majeshi ya kulinda amani kutoka Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Katika mapigano hayo, taarifa zinasema nchi za SADC ambazo zimepeleka wanajeshi huko, zimepoteza askari wake. Tanzania inadaiwa kupoteza askari wawili na wanne wamejeruhiwa, huku Afrika Kusini ikielezwa kupoteza askari wake 14 kati ya 20 waliouawa na ‘waasi’ wa M23 kati ya Januari 24 na 28 katika miji ya Seke na Goma.

Kwa mujibu wa taarifa zilipo kwenye mitandao ya kijamii, mapigano katika mji wa Goma yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 700 huku wengine zaidi ya 2,800 wakijeruhiwa. Maelfu ya watu wamekimbia makazi yao baada ya mji huo sasa kudhibitiwa na M23. Katika janga hili ambalo limezidi kufanya hali ya usalama wa DRC kuwa mbaya, pengine kuibua hofu pia kwa majirani zake kama Burundi na hata Tanzania, Rais Kagame amekuwa akiwashutumu wote ambao wamekuwa wakiendesha mazungumzo ya kutafuta amani ya DRC kuwa wanapenda kutukuza majina yao na siyo kupata ufumbuzi wa vita hivyo ambavyo hadi sasa vimepoteza maisha ya maelfu ya raia. Kagame amemshambulia Rais wa Angola, João Lourenço na Rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta ambao wamekuwa wakiendesha mazungumzo ya kutafuta amani ya mashariki mwa DRC.

Kwa Kagame viongozi hawa wanasumbuliwa zaidi na kutukuza majina yao kuliko kutatua mgogoro halisi wa mashariki ya DRC, lawama za Kagame hazijaishia kwa viongozi hao, bali hata kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo amediriki kuhoji kama ipo, huku akimtuhumu Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa kwa kuitishia nchi yake.

 ‘Waasi’ wa M23 waliibuka mara ya kwanza mwaka 2012 baada ya kundi la wanajeshi wa Jeshi la DRC kuasi na kuunda kundi la wapiganaji wa The National Congress for the Defense of the People (CNDP) na kutwaa maeneo ya Kivu Kaskazini hasa mji wa Goma. Kati ya mwaka 2012 na 2013, M23 waliendesha mapigano mengi ambayo yalisababisha mauaji ya maefu ya raia wa Kongo. M23 walidhibitiwa Novemba 2013, baada ya kupokea kichapo cha Jeshi la DRC likisaidiwa na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa (MONUSCO). Inaelezwa kwamba baada ya kudhibitiwa M23 walikimbilia Rwanda na Uganda.

M23 baada ya kupotea takribani kwa miaka minane hivi, 2021 waliibuka tena safari hii wakishambulia eneo lilelile la Kivu Kaskazini. Walikamata baadhi ya miji na wamekuwa wakiendelea kukamata maeneo ya mashariki ya DRC mpaka hivi karibuni walipoutwaa tena mji wa Goma.

Katika picha hii, M23 waliokimbilia Rwanda na Uganda zote zikiwa ni nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, baada ya kukaa mafichoni kwa miaka minane, walirejea tena kwa kishindo, safari hii wakifanikiwa kutwaa maeneo makubwa zaidi. Ni vigumu kusema kwamba Rwanda na Uganda hawahusiki katika nguvu hii mpya waliyokuja nayo M23. Kikubwa zaidi haielezeki Rwanda na hasa Rais Kagame anakwepa vipi lawama hizi za Umoja wa Mataifa, lakini pia hata za SADC kwamba ana mkono DRC.

DRC na Rwanda zote ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, lakini katika mgogoro wa mashariki ya Kongo umezifanya nchi hizi kuwa ‘paka na mbwa’ ambazo ni vigumu kwa sasa kuona zikielewana.

Wakati taarifa mbalimbali za uchunguzi za Umoja wa Mataifa zinaituhumu Rwanda kama ndiyo ‘kifua’ cha M23 ikidaiwa kuwa na askari wapatao 4,000 ndani ya ardhi ya DRC, Rais Kagame amekuwa akikanusha vikali madai hayo.

Kumekuwa na mfululizo wa vikao vya wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na SADC kutafuta njia ya kuepusha balaa na maafa yanayoendelea mashariki mwa DRC. Kwa sura ya vikao hivi, haiyumkiniki kama shida ya mgogoro wa mashariki ya DRC itapatikana kwa sababu kuu moja, utawala wa DRC unaonekana kwa miaka na miaka sasa kushindwa kabisa kubeba wajibu wa usalama wa eneo la mashariki mwa nchi hiyo mabegani mwao.

DRC ambayo ilipata uhuru mwaka 1960 kutoka kwa wakoloni wa Kibelgiji, serikali zote zilizoundwa tangu utawala wa Joseph Kasa-Vubu (1960–1965); Mobutu Sese Seko (965–1997); Laurent-Désiré Kabila (997–2001); Joseph Kabila (2001–2019) na sasa Félix Tshisekedi, imekuwa na masahibu makubwa ya rushwa, kukosa uwezo wa kulitawala eneo lote la nchi hiyo hali inayotoa mwanya kushamiri kwa vikundi vya waasi wenye silaha hasa upande wa mashariki wa taifa hilo wanaojinufaisha kwa rasilimali za madini na mazao ya misitu.

Leo hii ni vigumu kusema kwa yakini kabisa kwamba wakuu wa DRC walioko Kinshasa wanajali kwa kiwango gani yanayotokea mashariki mwa nchi hii. Wakongoman ambao wamekufa kutokana na mizozo na migogoro ya ndani kwa ndani au ikichochewa na nguvu kutoka nje, ni mamilioni mengi. Aidha, ni vigumu kusema kwa uhakika kwamba raia wa DRC hasa mashariki mwa nchi hiyo wamepata kuonja amani tangu uhuru wa nchi hiyo.

Ni katika kuangalia picha hii hoja inaibuka kwamba wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki au SADC au Umoja wa Afrika au hata Umoja wa Mataifa wanajadili nini hasa kuhusu mzozo wa DRC na majirani wake? Ni nini hasa kinakwamisha kupatikana kwa suluhu ya kudumu ya mgogoro ambao kwa miaka zaidi ya 30 sasa unaziunganisha pamoja Uganda, Rwanda na waasi wa M23 kwa upande mmoja na serikali ya DRC kwa upande mwingine?

Tumeona kule Ulaya mataifa yao yalivyojipanga kuitetea Ukraine ambayo ilivamiwa na Urusi. Tumeona Ukraine ikipewa kila aina ya msaada wa silaha na washirika wa NATO; tumeona mataifa  makubwa yakitenga bajeti kuisaida Ukraine; kikubwa tumeona mataifa makubwa yakipeleka azimio kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kulipitisha kwa kuweka vikwazo dhidi ya Russia.

Ni kwa nini tangu inaitwa Congo, kisha ikawa Zaire na sasa DRC imeachwa kuwa uwanja wa kumwaga damu ya watu wake wasio na hatia kana kwamba uhai wao hauna thamani kama tunavyoona kelele za kuitetea Palestina dhidi ya ukatili wa Israel au Ukraine dhidi ya uvamizi wa Russia? Kwa nini hali hii? Ni kwa nini AU imeshindwa kwa kiasi hiki kuhami mataifa yake?

spot_img

Latest articles

MINZIRO NA PAMBA YAKE NAWAPIGA TU

Na Mwandishi Wetu Timu ya Pamba Jiji chini ya Kocha Felix Minziro (Majeshi, Baba Isaya)...

Majaliwa azitaka Mamlaka za Mikoa, Taasisi za Elimu kusimamia utekelezaji Sera ya elimu

Na Mwandishi Wetu WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amezielekeza mamlaka za mikoa, halmashauri na taasisi za...

Bidhaa ‘feki’ zadidimiza Watanzania lindi la umasikini

Watanzania wanazidi kunasa katika mzunguko wa umasikini unaosababishwa na kushamiri kwa bidhaa duni na...

More like this

MINZIRO NA PAMBA YAKE NAWAPIGA TU

Na Mwandishi Wetu Timu ya Pamba Jiji chini ya Kocha Felix Minziro (Majeshi, Baba Isaya)...

Majaliwa azitaka Mamlaka za Mikoa, Taasisi za Elimu kusimamia utekelezaji Sera ya elimu

Na Mwandishi Wetu WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amezielekeza mamlaka za mikoa, halmashauri na taasisi za...