NI siku nne tu zimebakia kuupa kisogo mwaka 2024. Mwaka huu ulikuwa na mambo mengi. Mambo yalikuwa mengi katika nyanja nyingi. Kiuchumi ni mwaka ambao ulituonyesha makali ya vikwazo vya uchumi ambavyo viliwekewa taifa la Russia ili kuwatia adabu kwa uvamizi wake Ukaraine; vikwazo ambazo vilikata kuwili kama msumeno, kwa waweka vikwazo na wawekewa vikwazo. Mataifa mengi ya magharibi, hasa ya Umoja wa Kujihami Kijeshi wa Nchi za Magharibi kwa kimombo North Atlantic Treaty Organisation -NATO, yalionja makali ya kupanda kwa gharama za maisha kutokana na vikwazo walivyobuni wenyewe dhidi ya Russia!
Vita viliendelea kutamalaki maeneo mengi ya dunia, na vingali vinarindima. Kwa Afrika bado Sudan kunawaka moto katika ugomvi wa madaraka baina ya majeshi ya serikali na Vikosi vya Huduma ya Haraka – Rapid Support Forces (RSF). Zaidi ya watu milioni 10 raia wa Sudan wamekimbia makazi yao kutokana na vita hivyo vilivyoanzia mji mkuu wa Khartoum. Huko Afrika magharibi nako hakujapoa, nchi za Burkina Faso, Mali, Chad, Niger na Guinea – ukanda wa Sahel wanajeshi wameendelea kutawala kwa mkono wa chuma baada ya kuziondoa madarakani serikali zilizochaguliwa kwa kura.
Mashariki ya Kati ulikuwa mwaka wa matukio mabaya zaidi katika historia ya migogoro ya aina hiyo. Tukio la Oktoba 7, mwaka jana ambalo lilisababishwa na uvamizi wa kikundi cha Hamas katika ardhi ya Israel, limesababisha maafa makubwa katika ukanda wa Gaza. Gaza umebomolewa na kubakia magofu kutokana na mabomu ya Jeshi la Israel wakisingizia kuwasaka ‘magaidi’ wa Hamas. Maelfu ya watu wameuawa, kujeruhiwa na kupoteza makazi. Lebanon nayo haikuwa salama, Syria yameibuka mapya baada ya Rais Bashar al-Assad kuikimbia nchi kwenda kuishi Russia baada ya mji wa Damascus kuangukia mikononi mwa waasi.
Nguvu ya maandamano ya umma kwa mwaka wa 2024 ilizidi kuonyesha makali yake pia. Huko Bangladesh Waziri Mkuu Sheikh Hasina alifurushwa madarakani kufuatia mfululizo wa maandamano ya wanafunzi. Hasina amekimbilia uhamishoni India. Kwa majirani wetu Kenya, vijana wa kizazi cha Gen Z waliitikisa vilivyo serikali ya Rais William Ruto kufuatia maadamano makubwa kuwahi kutokea katika nchi hiyo ambayo yalifanyika katika miji yote mikubwa. Maandamano hayo yaliyokuwa yakipinga muswada wa Fedha wa mwaka 2024 yaliwafikisha waandamanaji mpaka bungeni ambako wabunge walikimbia na kuacha Gen Z wakijimilikisha ukumbi wa Bunge kwa muda, huku wakijiburudisha kwa vyakula na vinywaji vilivyokuwa vimeandaliwa kwa ajili ya wabunge.
Mwaka 2024 ulikuwa ni mwaka wa uchaguzi kwa mataifa mengi. Takribani nchi 70 duniani kote zilifanya uchaguzi. Afrika ilishuhudia uchaguzi huko Afrika Kusini ambako ANC kwa mara ya kwanza ilipoteza uhalali wa kuunda serikali wenyewe; Ghana chama tawala kilipoteza uongozi, Rwanda Rais Paul Kagame alizidi kujichimbia madarakani kwa ushindi wa kimbunga wa asilimia 99; Namibia kwa mara ya kwanza chama tawala SWAPO kimempata Rais wa kwanza Mwanamke, Netumbo Nandi-Ndaitwah; huku Msumbuji chama tawala Frelimo kimeingiwa na msukosuko mkubwa baada ya ushindi kwa asilimia 65 ambazo wapinzani wamekataa matokeo, hali ambayo imeliingiza taifa hilo lililotawaliwa na Wareno kuzidi kuzama katika uwezekano wa vita vya wenyewe kwa wenyewe tena.
Marekani Rais Donald Trump amerejea madarakani baada ya kurusha tena karata yake mara ya tatu. Awali aliongoza kipindi kimoja cha urais na kushindwa kutetea kiti chake dhidi ya Joe Baden mwaka 2020. Dunia inasubiri kuona Trump II atakuwa ni rais wa namna gani. Ulaya hakukuwa na utulivu pia. Ufaransa kumekuwa na mshikemshike dhidi ya Serikali ya Rais Emmanuel Macron, ambaye chama chake kimepigwa kwenye uchaguzi, nchini Uingereza utawala wa takribani muongo mmoja na nusu wa chama cha Conservative ulihitimishwa kwa kichapo kikubwa dhidi ya chama cha Labour kwenye uchaguzi mkuu wa Julai mwaka huu. Japan nako chama tawala LPD kilionjeshwa machungu kwa kupoteza viti vingi kuliko ilivyotarajiwa. Kwa kifupi uwanja wa kisiasa na masuala ya uchaguzi kulikuwa na mengi kwa mwaka 2024.
Hapa nyumbani, mambo hayakuwa haba. Ni mwaka ambao uchaguzi wa serikali za mitaa ulifanyika. Kama ilivyokuwa mwaka 2019, uchaguzi huo umeacha tena aibu. Aibu ya usimamizi wa hovyo wa mchakato mzima wa uchaguzi. Uandikishaji uliolalamikiwa na wengi, hasa vyama vya upinzani na wadau wengine wa uchaguzi, uteuzi wa wagombea uliojaa mizengwe na hila nyingi pamoja na upigaji kura ulioshuhudia vihoja vingi vya kura bandia. Ni uchaguzi ambao kwa mara nyingine damu za watu wasio na hatia imemwagwa. Mauaji ya wagombea, wafuasi wa vyama vya siasa kutekwa nyara na kuteswa kwa raia kwa sababu za kisiasa. Ulikuwa ni mwaka ambao Tanzania ilitarajiwa kusafisha makosa ya mwaka 2019, lakini kinyume chake ikazidi kuchafua taswira yake ndani na nje ya uga wa kimataifa.
Matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2024 nchini umeibua upya hisia za kutokuaminiana baina ya vyama vya siasa vya upinzani kwa upande mmoja na chama tawala kwa upande wa pili. Kadhalika, wadau wengine wa kisiasa kama taasisi za dini, wameonyesha wasiwasi wao kuhusu uchaguzi huo kama kweli unakidhi vigezo vya kuwa huru na haki.
Katika muktadha huo, swali kubwa linaibuka. Je, kile alichoahidi Rais Samia Suluhu Hassan juu ya R4 ndicho hicho kimejidhihirisha katika uchaguzi wa serikali za mitaa? Kwamba R4 zilizaliwa kutokana na matukio mabaya ya masuala mbalimbali katika nchi yaliyotamalaki tangu mwaka 2016 hadi 2021. Yakiwamo kukamatwa kwa watu kiholela na kuteswa, kutekwa, kuuawa na kupotezwa kwa upande mmoja, na ukiukaji mkubwa wa misingi ya mchakato huru na haki wa uchaguzi wa kidemokrasia ya vyama vingi kwa upande mwingine.
Tunapofunga mwaka 2024 tukiendea na kuukaribisha mwaka 2025 ambao utakuwa ni mwaka wa uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na rais, tukiwa na mzigo wa uchafuzi wa uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kiwango hiki, tunakwenda kutarajia uchaguzi wa namna gani?
Kama vitendo vya ukiukaji wa mchakato wa uchaguzi unafurahiwa na wale walioaminiwa kuusimamia, ni utamaduni gani tunaujenga nchini kuhusu uchaguzi? Je, ni hisia gani ya kisiasa inajengwa kwa wananchi kwamba uchaguzi ni kiini macho, ni hadaa au ni utashi wa aliyeko madarakani na siyo uamuzi wa wananchi kwa mujibu wa ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Kama taifa tunakubaliana kwamba uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, hazikuwa ni chaguzi huru kwa vigezo vyovyote vinavyokubalika kidemokrasia. Kama hivyo ndivyo, lakini tumeruhusu tena uchafuzi wa mwaka 2019 kujirudia mwaka 2024, hakika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kuwa huru na haki bila uchafuzi utakuwa ni muhali.
Pengine wenye dhima ya kusimamia uchaguzi katika nchi hii wajaribu kutumia vema maarifa waliyojaliwa na Muumba wao kwamba ‘mvunja nchi ni mwananchi’ hasa anapokwepa au kukataa kutimiza wajibu wake sawasawa. Ni kujidanganya kwa kiwango kikubwa kudhani eti vurugu zinazotokea katika mataifa mengine Afrika na hata nje ya bara hili kwa sababu ya hila za uchaguzi, eti haziwezi kutokea Tanzania. Tukumbuke mwisho wa yote binadamu wote ni wanyama.