JANA Jumatano Novemba 27, 2024 Watanzania walipiga kura kuchagua viongozi wao wa serikali za mitaa. Hawa ni wenyeviti wa vijijini na vitongozi kwenye maeneo ya vijijini na wenyeviti wa mitaa kwa maeneo ya mijini.
Uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka huu wa 2024 ingawa siyo wa kwanza katika mfumo wa siasa za vyama nchini, ulikuwa na umuhimu wa kipekee. Umuhimu huu unatokana na historia ya uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019 na uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na urais wa mwaka 2020. Katika chaguzi hizi mbili mambo kadhaa yalijitokeza ambayo yalikuwa ni tofauti kabisa na chaguzi nyingine zote ambazo zilifanyika huko nyuma tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992.
Uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa ni kipimo cha kuona kwa matendo halisi juu ya ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kurejesha hali mpya ya ustawi katika taifa kwa kile alichookita R4 akimaanisha kukuza Maridhiano (Reconciliation), Ustahamilivu (Resilience), Mageuzi (Reforms), na Kujenga upya Taifa (Rebuilding).
Ingawa uchambuzi huu umeandikwa kabla ya matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 kutangazwa, mchakato wa uchaguzi huu umekumbwa na malalamiko mengi. Haya yalikuwa katika sura ambayo inafanana na mambo yaliyotokea kwenye uchaguzi wa 2019 na ule wa 2020. Kikubwa ni kuenguliwa kwa baadhi ya wagombea kwa kile kilichoelezwa ni kukosa sifa za kugombea.
Akizungumza na wahariri katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Novemba 16, 2024 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa alieleza kuridhishwa kwake na mchakato mzima wa uchaguzi huo. Alisema kwa takwimu alizokuwa amepokea kutoka mikoa yote Tanzania, kwamba katika nafasi zote zinazogombewa ambazo ni vijiji 12,280; mitaa 4,264 na vitongoji 63,886 ni Chama Cha Mapinduzi tu kilikuwa kimesimamisha wagombea wake kwenye nafasi zote, huku vyama vya upinzani kwa ujumla wao wakiwa wamesimamisha wagombea kwa asilimia 38.51 tu.
Kwa kauli ya Mchengerwa asilimia 61.49 ni wagombea pekee wa CCM ambao wangepigiwa kura ya ndiyo na hapana katika uchaguzi uliofanyika jana, Novemba 27, 2024. Mchengerwa katika mkutano na wahariri alilaumu baadhi ya viongozi ambao kwa kiwango kikubwa alidai wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kufanya ‘propaganda’ juu ya kukatwa kwa wagombea wa upinzani, huku akidai kwamba ‘propaganda’ hizo zimesababisha hata viongozi wa taasisi za dini wanaoheshimika kutoa matamko ambayo yamesababishwa na alichokisema ni upotoshaji wa mchakato wa uchaguzi huo.
Wakati Mchengerwa akilaumu alichookiita ‘propaganda’ Novemba 19, 2024 Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe, aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza kwa kina madhila ambayo wagombea wa Chadema katika ngazi mbalimbali za serikali za mitaa walikumbana nayo katika mchakato wa uchaguzi huo, ikiwa ni pamoja na kuenguliwa bila kufuata taratibu na sheria. Mbowe alieleza kusikitishwa na takwimu za Mchengerwa akieleza kuwa zinatokana na mkakati wa makusudi wa kuzuia wagombea wa vyama vya upinzani kuwania nafasi katika uchaguzi huo. Kwa ujumla, hakujawa na maelewano juu ya kile kinachoitwa vyama vya siasa vya upinzani kushindwa kusimamisha wagombea kama ambavyo Mchengerwa anaeleza, na kile ambacho viongozi wa vyama vya upinzani wanaeleza wagombea na wanachama wao kufanyiwa ‘figisu’ nyingi ili kuwapoka haki na fursa yao ya kuwania nafasi zinazoshindaniwa katika uchaguzi uliofanyika jana.
Malalamiko haya ya kuenguliwa kwa wingi kwa wagombea wa vyama vya upinzani, pamoja na ‘walakini’ wa uandikishaji wa wapiga kura ulioelezwa kufanyika bila udhibiti wowote wa utambuzi bila kutoa kitambulisho chochote, ndiyo ulisababisha Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kila taasisi kwa nafasi yake kutoa kauli juu ya mwenendo wenye shaka wa uchaguzi wa serikali za mitaa.
Waziri Mchengerwa kwa kauli yake anaamini kwamba mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2024 umefanyika vema, anaamini kwamba Watanzania wamepata fursa ya kutumia haki yao ya kikatiba kushiriki ama kwa kuchaguliwa au kuchagua viongozi wanaowataka.
Wakati Mchengerwa akisimamia msimamo huo ana akisisitiza kuwa suala la uchaguzi siyo la huruma bali la kisheria, yapo maoni mengi kwamba kuna maamuzi yamefanywa na wasimamizi wa uchaguzi huo ambayo yanaacha maswali mengi juu ya Watanzania wa upande mmoja katika mchakato wa uchaguzi huo kuwa werevu wa kufuata taratibu, ilihali wa upande mwingine wakionekana kwamba ndiwo tu hawajui, kwa mfano jinsi ya kujaza fomu.
Malalamiko haya pengine ndiyo yalimfikia Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na kumwagiza Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi, kutoa kauli ya kuwataka wasimamizi wa uchaguzi huo kulegeza kamba katika kushikilia makosa madogomadogo ambayo yamewafanya baadhi ya wagombea kuenguliwa, ili kusaidia kulea ‘demokarasia changa ya Watanzania’. Pengine ni malalamiko hayo hayo ya kuonekana kukosekana kwa uwanja uliosawa baina ya pande mbili zinazowania nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo, ndiyo pia kumewaibua CCT na TEC.
R4 za Rais zimekuwa zikifanyiwa rejea mara nyingi sana na Watanzania. Nia ya kufanya rejea hizi ni kutaka kukumbushana na kuelezana kwamba kama taifa hapo nyuma kuna mahali tulikwama. Kwa mfano ukimsikia Mwenyekiti wa Chadema Mbowe, anasema kwamba baada ya kuvurugwa kwa kiwango kukibwa kwa uwanja wa kufanya siasa nchini kwa takribani miaka saba, wameanza kujenga tena chama chao kwa uhuru tangu Februari mwaka jana. Kwa maana hiyo, ni kweli kuna sehemu ambazo hawajafika kwa sasa na ndiyo maana hawakusimamisha wagombea kwenye nafasi zote maeneo yote. Hata hivyo, analalamika kwamba bado kuna watu hawaamini katika kutenda haki kwenye uchaguzi.
Kwa tathmini ya mapema ya mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 sura ambayo imejitokeza tangu siku ya kwanza ni ya kukosekana kuaminiana baina ya wadau wote wa kisiasa. Kuna kutokuaminiana juu ya chombo chenye sifa ya kusimamia uchaguzi huo. Kuna kutokuaminiana juu ya utararibu wa kuandikisha wapiga kura, lakini pia kuna kutokuaminiana juu ya wenye dhima ya kupitisha wagombea na kutangaza matokeo.
Sura ya uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mwaka wa 2024 ni lazima ifikirishe Watanzania wote kwa kujiuliza maswali muhimu; je, wote tuna nia ya kujenga taifa moja, lenye kulinda haki za kila mmoja? Ni kwa kiasi gani R4 za Rais Samia zimezingatiwa katika kuendesha uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024? Katika uchaguzi wa mwaka huu tumefuzu nini? Ni vema tujikumbushe kama Watanzania hatuna nchi nyingine ya kwenda, tusichukulie haki kwa wepesi. Haki husimamisha taifa imara.