MWAKA 2024 umeendelea kuwa mwaka wenye shughuli nyingi hasa kwenye eneo la uchaguzi. Takribani nchi 70 duniani kote mwaka huu zimefanya uchaguzi au zitafanya katika muda wa miezi miwili iliyosalia kwa mwaka huu kufikia tamati.
Uchaguzi haujawahi kuwa ni habari njema kwa walioko madarakani. Siyo habari njema kwa sababu katika nchi inayoendesha uchaguzi huru ukisimamiwa na vyombo huru vyenye kutekeleza wajibu wake bila kuingiliwa, mara nyingi watawala wanapokwenda kwa wananchi kuomba tena kuruhusiwa kuongoza nchi zao, wanakuwa hawana hakika ya matokeo yatakuwa kwa upande wao au la.
Uchaguzi kutokuwa habari njema katika nchi zenye mifumo huru ya kusimamia kazi hiyo, unaweza kuelezwa katika sura ya uchaguzi kama uliofanyika Ufaransa Julai mwaka huu. Katika uchaguzi huo ushirika wa Rais Emmanuel Macron, umejikuta katika mtihani mkubwa wa kuongoza Bunge na serikali kutokana na uamuzi wa wananchi kwenye sanduku la kura wa kuwaadhibu watawala hao vikali.
Kwa mfano, sheria za Ufaransa zinaweka kigezo kwa chama cha siasa ama chenyewe au kwa ushirika wake kuwa na haki ya kuunda serikali kama watapata walau wabunge 289 katika bunge lenye viti 577, Macron na mshirika wake katika uchaguzi wa Julai mwaka huu walipoteza viti vingi na kujikuta wakishika nafasi ya pili kwa kujikusanyia jumla ya wabunge 161, hali hiyo inamfanya aingie katika kazi nyingine ngumu ya kutafuta jinsi ya kubakia salama madarakani katika siasa za Ufaransa kwa kutafuta kuunganisha nguvu na vyama vingine.
Jumapili ya Oktoba 26, 2024 wananchi wa Japan nao walimuonyesha Waziri mkuu wa nchi hiyo, Shigeru Ishiba, uchaguzi usivyokuwa habari njema kwa watawala. Chama tawala cha Japan, Liberal Democratic Party (LDP) na Mshirika wake chama cha Komeito, wamekosa wingi wa wabunge wa kuwawezesha kuunda serikali wao tu. Ushirika huo ulikuwa na wabunge (viti) 279, lakini matokeo ya uchaguzi huo ambao uliitishwa mapema umeadhibu ushirika wa Waziri Mkuu Ishiba vilivyo kwani wamepoteza wabunge 64 kwa kuibuka na viti 215 tu.
Katika nchi za Afrika mwaka huu tumeshuhudia uchaguzi nyingi kama Afrika Kusini, Rwanda, Tunisia na Msumbiji. Nchini Afrika Kusini chama tawala ANC Mei kilikumbana na hasira ya umma kwani kwa mara ya kwanza tangu kianze kutawala taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi Afrika mwaka 1994, kilishindwa kupata wingi wa viti vya bunge vya kukipa fursa ya kuunda serikali. ANC ilipata asilimia 40.18 ya kura na kupata wabunge 159, huku chama Democratic Alliance (DA) kikiibuka cha pili kwa kura asilimia 21.8 wakijikusanyia wabunge 87. ANC ilishindwa kuunda serikali yenyewe kwa kukosa vigezo vya kisheria, ikaamua kutafuta washirika miongoni mwao ni chama cha DA. Ukiwaeleza wanachama wa ANC kwamba uchaguzi siyo habari njema sana kwa kuwa ni sawa na kwenda kwenye usahili wa kutafuta kazi, wanaweza kukuelewa sasa na hivyo kujihoji hasira ya umma inatoka wapi na wafanye nini wasijekupotea kabisa. Sasa wanajua katika uchaguzi lolote linaweza kutokea.
Wakati baadhi ya watawala wakiona uchaguzi kwamba siyo habari njema kwa kuwa ni usahili wa wananchi kulingana na utendaji wao kwa kipindi kilichopita, labda hofu hiyo haikuwako kwa Rais Paul Kagame wa Rwanda na chama tawala cha RPF ambacho katika uchaguzi mkuu wa Julai mwaka huu kimezoa asilimia 99.18 ya kura zote milioni nane na ushei – ikiwa na idadi ya watu ya milioni 14 na ushei tu; au siyo habari ya kumnyima usingizi Rais wa Tunisia, Kais Saied ambaye katika uchaguzi mkuu wa Julai mwaka huu amezoa kura asilimia 90.7 katika uchaguzi ambao wapigakura wachache asilimia 28.8 tu ndiyo walijitokeza kushiriki.
Pia makali ya uchaguzi yanaweza yasiwasumbue sana chama tawala cha Msumbiji, Frelimo, ambacho mgombea wake, Daniel Chapo, katika uchaguzi wa mapema mwezi wa huu wa Oktoba, alijichotea asilimia 70 ya ushindi wa urais, akiwaacha wapinzani wake mbali. Mgombea wa kujitegemea Vanencio Mondlane aliibuka na asilimia 20 wakati mgombea wa chama cha Renamo, Ossufo Momade, alipata asilimia 5 tu ya kura za urais. Matokeo hayo yameamsha rabsha kubwa ya maandamano nchini Msumbuji.
Tanzania mwezi ujao, Novemba 27, 2024, itaungana na nchi nyingine za Afrika na duniani kote kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa. Uchaguzi huo umekuwa na matukio kadhaa ya ukinzani. Miongoni mwake ni hoja ya uhalali wa Wizara ya Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa (TAMISEMI) kusimamia uchaguzi huo. Wapo waliofungua kesi kupinga TAMISEMI kusimamia uchuguzi huo, Mahakama Kuu imehukumu na kusema ni halali TAMISEMI kusimamia uchaguzi huo.
Mwakani Tanzania itafanya uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa saba tangu mfumo wa vyama vingi ulioporejeshwa tena nchini kisheria mwaka 1992. Katika chaguzi hizo, uchaguzi wa mwaka 2005 ambao Rais Jakaya Kikwete alikuwa mgombea wa Chama cha Mapinduzi ndiye aliweka rekodi ya kuzoa kura nyingi kwa kupata asilimia 80.28 akiwa amekusanya kura milioni 9.123. Rekodi ya Kikwete ilikuja kuvunjwa na Rais John Magufuli wa CCM katika uchaguzi wa mwaka 2020 ambao alipata kura milioni 12.516 sawa na asilimia 84.40. Hata hivyo, uchaguzi wa mwaka 2020 ndiyo unatajwa kujaa vitendo vingi vya ukiukaji wa uchaguzi ikiwa ni pamoja na kuenguliwa kwa wagombea wa vyama vya upinzani kwa hila.
Mwaka 2015 Edward Lowassa akiwania urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiungwa mkono na vyama vingine vitatu vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), alivunja rekodi iliyokuwa inashikiliwa na mgombea wa upinzani, Augustino Mrema aliyewania urais akichuana na Rais Benjamin Mkapa mwaka 1995, Profesa Ibrahimu Lipumba wa CUF na John Cheyo wa UDP. Mkapa alishinda kwa kupata kura milioni 4.02 sawa na asilimia 61.82 huku Mrema akipata kura milioni 1.808 sawa na asilimia 27.77.
Lowassa alivunja rekodi hiyo kwa kupata kura milioni 6.072 sawa na asilimia 39.97 nyuma ya Magufuli aliyepata kura milioni 8.882 sawa na asilimia 58.46.
Kwa maneno mengine, katika chaguzi sita zilizopita tangu mwaka 1995 hadi 2020 upinzani ulipata kufikia walau asilimia 40 ya kura, CCM nayo ilipata kupata kiwango cha chini kabisa cha kura cha asilimia 58.46 mwaka 2015 kwa Magufuli, kikifuatiwa na kile cha Mkapa cha mwaka 1995 cha asilimia 61.82 na cha Kikwete cha asilimia 62.83 mwaka 2010 alipopambana pamoja na wagombesa wengine, Dk Wilbroad Slaa wa Chadema aliyepata asilimia 27.02.
Kiwango hili cha kura kwa watawala nchini kwetu, kinaacha uwanja wazi kwa wenye maswali kama kweli CCM kama chama tawala kimefikishwa hatua ya kuona ‘uchaguzi siyo habari njema?’ Ni vigumu kufikia hitimisho hilo. Hata hivyo, mtu anapaswa kupiga picha mwelekeo wa chaguzi za Tanzania mwaka baada ya mwaka, grafu zinaonyesha kupanda na kushuka kwa pande zote mbili, yaani chama tawala huwa kinapanda na kushuka, wakati hali ikiwa ni hiyo pia kwa vyama vya upinzani. Kwa mfano tafakari ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 inaacha maswali mengi, kwamba ingawa Magufuli alipata ushindi wa kishindo wa asilimia 84.40 na kuweka rekodi ya ushindi wa CCM ndani ya mfumo wa vyama vingi, Mgombea wa Chadema, Tundu Lissu, alipata kura milioni 1.933 sawa na asilimia 13.04 katika mazingira ambayo yalikuwa ni magumu na hatarishi mno kwa mtu kufanya siasa za ushindani hasa kutoka kambi ya upinzani.
Mwelekeo huu wa hali ya uchaguzi barani Afrika na kwingineko duniani inamfanya mtu ajiulize, je, Tanzania imefika hatua ya watawala kuwaza kwamba uchaguzi siyo habari njema sana kwa kuwa wananchi hawatabiriki?