Shamba darasa kutoka Kenya: Hata Rais anatokwa jasho

KUNA kitu kinaitwa ‘shamba darasa’. Hili ni shamba ambalo huandaliwa na kuendeshwa kwa nia ya kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wakulima. Aghalabu, shamba hili husimamiwa na wataalam wa kilimo almaarufu kama maofisa ugani. Shamba hili huwapa wakulima fursa ya kujifunza kwa kuona njia za kitaalam za kuendesha kilimo. Shamba darasa pia laweza kuwapo kwenye uwanja wa kuendesha siasa na utawala.

Kwa mfano kinachoendelea katika nchi jirani ya Kenya tangu mwanzoni mwa mwezi huu katika kile kinachoitwa kumuondoa madarakani Naibu Rais, Rigathi Gachagua, hakika ni shamba darasa la siasa kwa nchi za Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.

Gachagua au kama wengi wanavyomuita Riggy G amekuwa kwenye mtanziko mkali wa kisiasa nchini Kenya. Ametuhumiwa kwa makosa 11 ambayo yaliwasilishwa mbele ya Bunge la nchini hiyo ambako kura ya kumuondoa madarakani ilipigwa dhini yake, kwa wabunge 282 kuridhia kumfurusha madarakani. Mashitaka yake pia yaliwasilishwa mbele ya Bunge la Seneti la nchi hiyo ambalo lilimtia hatiani kwa makosa matano kati ya 11 aliyokuwa anashitakiwa kwayo. Kwa uamuzi wa Seneti Riggy G alitangazwa kupoteza nafasi hiyo ambayo amekuwa akiishikilia tangu mwaka 2022 waliposhinda uchaguzi mkuu akiwa ni mgombea mwenza wa swahiba wake, Rais William Ruto.

Hata hivyo, pamoja na Bunge la Kenya kumpitisha kwa kauli moja Profesa Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais mpya, mchakato wa kumpitisha umeingia mushkeli baada ya Mahakama Kuu nchini humo kutoa zuio la muda la kuendelea kwa mchakato huo kwa kile kinachoelezwa haki za Riggy G kukiukwa. Riggy G amefungua kesi mahakamani kupinga uamuzi wa Seneti kwa kuwa hakupewa fursa ya kujitetea. Riggy G aliugua ghafla Alhamisi iliyopita na kulazwa kwa muda katika hospitali ya Karen akidaiwa kuwa na maumivu makali ya kifua. Juzi Jumapili, Riggy G alitoka hopitalini na hakuficha hisia zake kwamba anayemwandama siyo mtu mwingine isipokuwa Rais Ruto. Amemuomba asimuue yeye wala watoto wake. Maneno haya yanafanana na ambayo Ruto akiwa Naibu Rais alipata kutoa dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta.

Awali ilikuwa inaonekana kama maneno ni ya mtaani kwamba Riggy G na Ruto, washirika wakuu waliounda Muungano wa Kenya Kwanza katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 uliomuweka madarakani Ruto, wamegeuka kuwa maadui wakubwa wasioweza tena kukaa kwenye serikali moja, lakini kwa yanayoendelea Kenya na kwa kauli ya Riggy G mwenyewe wawili hawa sasa ni mahasimu wakuu.

Riggy G ametamka hadharani kwamba kwa mwaka mmoja sasa amekuwa katika mateso makubwa. Amefungamanisha mateso hayo na uamuzi wa Rais Ruto wa kutaka kumuangamiza. Amedai wazi kwamba ameponea mara mbili kuuawa kwa sumu. Mara ya kwanza akiwa Kisumu na baadaye akiwa Meru. Anasema wazi kwamba baada ya njama za kumuua kwa sumu kushindikana ndipo hatua ya kumng’oa kwenye kiti cha Makamu wa Rais zilipangwa. Rais Ruto hajatamka lolote juu ya madai ya Riggy G, isipokuwa tu kasi ya serikali yake kusukuma mchakato wa kumng’oa madarakani Riggy G na kumteua mbadala wake, ndiyo unaweza kuonyesha uhusika wa Rais huyo wa Tano wa Jamhuri ya Kenya.

Katika mchakato wote huu wa kumng’oa Riggy G, kuanzia Bungeni na kisha kwenye Seneti, ni kwa kiasi gani unatoa fursa na somo la kisiasa katika nchi za ukanda huu? Ingawa kila taifa miongoni mwa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ina tamaduni zake na maadili ya kisiasa, sura moja ambayo inajitokeza kwa Kenya na ambayo inaweza kuwa funzo kubwa yaani shamba darasa ni jinsi mahakama ilivyo huru.

Uhuru huu wa mahakama siyo tu unakuwa kiboko cha kila mmoja katika nchi hiyo, bali ni kimbilio la uhakika kwa yeyote anayeona kwamba haki yake imeathirika katika kufikiwa maamuzi fulani dhidi yake.

Kwa mfano, ukitafakari kwa undani kasi ya serikali ya kutaka kumthibitisha Naibu Rais kati ya Alhamisi ya Oktoba 17 na Oktoba 18, mwaka huu utaona wazi kwamba kuna kitu serikali ilikuwa inakimbizana nacho. Uamuzi wa Seneti wa kumng’oa Riggy G ulifikiwa dakika chache kabla ya usiku wa saa sita Alhamisi ya Oktoba 17, 2024, lakini ndani ya dakika hizo zisizozidi nusu saa, Seneti ilifanikisha kutolewa kwa Tangazo la Serikali la Oktoba 17, 2024 la kutangaza kwamba kiti cha Naibu Rais kiko wazi kwani Riggy G alikuwa ameng’olewa kwa kutiwa hatiani kwa makosa matano kati ya 11.

Kasi hiyo hiyo, ilidhihirika kesho yake asubuhi, yaani Oktoba 18, 2024 kwa Rais Ruto kuwasilisha jina la Profesa Kindiki mbele ya Bunge kwa ajili ya kupitishwa kuwa Naibu Rais, ambalo nalo kwa kasi ya umeme walimpitisha kwa kauli moja. Wakati serikali ikikimbia kwa kasi hiyo, upande wa Riggy G nao ulikuwa unakimbizana na mchakato wa kufungua kesi mahakamani, na walifanikiwa kupata hati ya zuio la mahakama dhidi ya uamuzi wa Seneti wa kumng’oa madarakani. Ni amri hii ya mahakama ndiyo imefanya Profesa Kindiki asile kiapo cha kuanza kazi hiyo mpya, ingawa tayari watumishi wote waliokuwa wanafanya kazi na Riggy G wametakiwa kwenda likizo ya lazima. Hatua hii bila shaka inatoa mwanya wa Profesa Kindiki kuingia ofisini na timu ya watu wake.

Kesi iliyofunguliwa na Riggy G itasikilizwa Alhamisi wiki hii, yaani Oktoba 24, 2024, ambayo inasubiriwa na wengi kuona kile ambacho Wakenya kwa asilimia kubwa wanaamini kuwa mahakama zao ziko huru. Kwamba siyo mali ya muhimili wa serikali wala Bunge, na ndiyo maana mihimili hii miwili, Bunge na serikali, walikuwa wanakimbizana na muda kabla mahakama haijatia mguu kwenye mchakato mzima wa kumng’oa Riggy G na kumweka mbadala wake.

Ukitazama na kutafakari mfumo wa mgawanyo wa madaraka miongoni mwa mihimili ya madaraka ya dola kati ya Bunge, Serikali na Mahakama, utaona jinsi ambavyo Mahakama imejitenga dhidi ya kuingia ‘ushirika’ wa kuvunja haki za raia. Mahakama za Kenya kwa mara nyingi zimekuwa zikijiendesha kwa uhuru mkubwa, kiasi kwamba mwaka 2017 Mahakama ya Rufaa (Mahakama ya Upeo) ilifuta matokeo ya uchaguzi wa Rais ambao Uhuru Kenyatta alikuwa anatetea kiti chake. Uamuzi huu wa Mahakama ya Rufaa ya Kenya siyo tu ulitikisa Kenya, Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, bali pia ulionyesha kwa viwango vya juu kabisa jinsi ambavyo Mahakama za Kenya isivyowezekana kuwekwa kwenye mifuko ya wanasiasa wanaotamba kuwa wana ‘mizizi mirefu.’  

Kwa mara nyingine Kenya wametupatia shamba darasa la kisiasa. Kwamba wanaweza kutumia katiba yao kuwajibishana, lakini pia katiba hiyo hiyo inalazimisha kila mmoja aifuate pasi na kisingizio chochote. Ile tu kutoa zuio dhidi ya uamuzi wa Seneti, ni kielelezo kwamba ipo kwa ajili ya kulinda na kutetea haki za yeyote anayeona kuwa haki yake inavunjwa. Haijalishi anayevunja ni mtu mmoja mmoja au taasisi au muhimili wa dola, kwa mahakama za Kenya kila mmoja anastahili kulindwa kwa haki zake. Na hili ni shamba darasa kubwa sana ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ukiona hata Rais anakimbizana na jambo lake kuwahi kabla ya mahakama hajaamua vinginevyo, ni hakika katika mazingira kama hayo, uhuru wa mahakama unaishi na kustawi.

spot_img

Latest articles

Kuporomoka majengo: Tuseme hapana kwa majanga ya kujitakia

TANZANIA ni nchi salama sana dhidi ya majanga ya asili kama vimbunga, matetemeko ya...

Rais Samia avaa viatu vya Mwalimu G20

Rio de Janeiro, Brazil RAIS Samia Suluhu Hassan ameyataka mataifa tajiri duniani ya kundi la...

Nyerere’s Footsteps, Samia Urges G20 to Rethink Global Economic Systems

Rio de Janeiro, Brazil President Samia Suluhu Hassan has rekindled the enduring vision of Tanzania’s...

Mjerumani amrithi Gamondi

Na Winfrida Mtoi Yanga imemtangaza kocha Sead Ramovic raia wa Ujerumani kuchukua nafasi ya...

More like this

Kuporomoka majengo: Tuseme hapana kwa majanga ya kujitakia

TANZANIA ni nchi salama sana dhidi ya majanga ya asili kama vimbunga, matetemeko ya...

Rais Samia avaa viatu vya Mwalimu G20

Rio de Janeiro, Brazil RAIS Samia Suluhu Hassan ameyataka mataifa tajiri duniani ya kundi la...

Nyerere’s Footsteps, Samia Urges G20 to Rethink Global Economic Systems

Rio de Janeiro, Brazil President Samia Suluhu Hassan has rekindled the enduring vision of Tanzania’s...