JUMATATU wiki hii Watanzania walikumbuka kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliyefariki dunia katika hopitali ya Mtakatifu Thomas London, Uingereza Oktoba 14, mwaka 1999. Tangu Mwalimu atangulie mbele ya haki ni robo karne imepita, ni muda mrefu kwa viwango vya ratiba za kazi na uhai wa mwanadamu.
Watanzania wanamkumbuka Mwalimu Nyerere kama kiongozi mwaminifu aliyewaongoza kwa kipindi cha miaka 24, tangu uhuru Desemba 9, mwaka 1961 hadi alipong’atuka madarakani kwa hiari yake mwaka 1985. Muda ambao Mwalimu alikaa madarakani hautafikiwa na Rais mwingine walau kwa sasa, kwa kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka ukomo wa mtu kukaa madarakani. Katiba inaruhusu vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja.
Baada ya kuondoka madarakani na kumkabidhi mikoba ya urais Ali Hassan Mwinyi, kwa kipindi cha miaka mitano alibaki na madaraka ya Uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakati huo kikiwa ni chama pekee cha siasa nchini. Katika kipindi hicho, 1985 – 1990, Mwalimu alianzisha programu aliyoibatiza jina la ‘Kuimarisha Chama’. Alifanya ziara mikoa mbalimbali kuimarisha CCM.
Hatimaye Agosti mwaka 1990 Mwalimu aliachia pia madaraka ya chama, hivyo kutoa fursa kwa Rais Mwinyi kuwa na kofia mbili, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, chama tawala. Ni kama alijiimarisha zaidi madarakani, akiongoza chama na serikali.
Kwa mara ya kwanza Tanzania ikawa na Rais Mstaafu na Mwenyekiti Mstaafu wa chama tawala. Katika mazingira hayo ambayo kwa nchi za Afrika ilikuwa ni nadra sana kuwa na Rais Mstaafu aliye hai huku Rais aliyeko madarakani akiendelea na majukumu yake bila bugudha au kuwa na hofu ya mwenendo wa Rais Mstaafu, ulikuwa ni uzoefu mpya wa kisiasa nchini. Hatukuona vituko vya kutaka kumshitaki Rais mstaafu kwa tuhuma za kutunga au vinginevyo kama ilivyoshuhudiwa kwa nchi nyingi za Afrika. Mwalimu aliishi kwa heshima kubwa, akiwa mtu huru ambaye hakuwahi kuficha hisia zake kwa jambo lolote kuhusu utawala wa nchi, hata kama lilikuwa ni kutokukubaliana na maamuzi yaliyofikiwa.
Leo tunapotazama nyuma na kutafakari mfumo wa utawala wa taifa letu, na tukijaribu kukumbuka hali ya mambo ilivyokuwa wakati wa utawala wa Rais Mwinyi, tunajivuna kwamba kuna msingi mkubwa sana ulijengwa wa kuvumiliana baina ya viongozi wakuu. Huu sasa umekuwa ni utamaduni wa taifa letu.
Hali hii unaweza kuielewa zaidi kama ukisoma kitabu cha Rais Mwinyi – Mzee Rukhsa: Safari ya Maisha Yangu, ambako Rais Mwinyi anasema wazi kwamba hakupata kumjibu Mwalimu Nyerere kwa jambo lolote ambalo alitoa changamoto kuhusu utawala wake, hasa kuhusu safari ya mageuzi ya kiuchumi. Rais Mwinyi anaeleza wazi kwenye kitabu chake kwamba alikuwa anamuheshimu sana Mwalimu na alimsaidia sana katika kipindi cha Urais wake, na walielewana kwa mengi.
Kauli nzito kati ya nyingi ambazo Mwalimu alipata kutoa hadharani akionyesha kutokukubaliana na sera za CCM na serikali ni suala la ubinafsishaji wa mashirika ya umma. Akihutubia katika shehehe za Mei Mosi 1995 mkoani Mbeya, Mwalimu siyo tu alitumia maneno mazito kuonyesha kutokukubaliana na utekelezaji wa sera hizo ulivyokuwa unafanywa kinyume cha maelezo, bali pia alionyesha wazi kwamba utekelezaji wa sera hizo ilikuwa mbinu ya wachache kuwa mabilionea kwa rasilimali za umma huku watu masikini wakiongezeka. Ingawa pia alisema sera hizo zilitokana na shinikizo kutoka nje, bila shaka akilenga Shirika la Fedha Duniani (IMF), lakini akihoji kwa nini viongozi walikubali kila kitu tu.
Mwalimu akisema kwamba kumekuwa na wimbi la kutaka nchi masikini kufunga viwanda vyake, wakati inajulikana wazi kuwa ili nchi iendelee ni lazima kuwa na viwanda vyake. Alitoa mfano kwamba alipoondoka madarakani aliacha viwanda vya nguo vya umma 12 ambavyo vilikuwa vinatumia asilimia 75 ya pamba yote iliyokuwa inazalishwa nchini. Ni katika hotuba ambayo alitoa kauli nzito zifuatazo:
“Mtu mwenye akili akikupa mawazo ya kipumbavu usipoyakataa anakudharau.” Mwalimu aliongeza kwamba sera ya CCM kwa miaka ya 90 kuhusu mashirika ya umma ilikuwa ni kurekebisha mashirika ya umma, kwa kuuza yake yaliyokuwa yanaleta hasara, au kuyafunga au kuyakodisha. Ama kwa yale ambayo ni ya msingi na nyeti kwa uchumi kama Bandari, Posta na Simu; Reli; Mabenki na Nishati yataendelea kuwa ya umma.
Mwalimu alihoji kwa nini sasa mashirika yanayopata faida yanauzwa? Huku akisema uamuzi huo ni “huu ni unyang’anyi tu” na kusisitiza kwamba “hili ni jambo la kipumbavu.” Hakika, hotuba ya Mei Mosi mwaka 1995 siyo tu kwamba ilitikisa utawala wa Rais Mwinyi, bali pia ilionyesha uvumlivu uliopindukia wa Rais Mwinyi wa kutokumjibu Mwalimu kama anavyoeleza kwenye kitabu chake kwamba hakutaka kumjibu Mwalimu katika ukosoaji wake.
Tunapoadhimisha kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Nyerere miaka 25 sasa, tunawiwa kujitafakari kama taifa kama kweli leo hii yupo kiongozi mstaafu anayethubutu kuhoji lolote linalofaywa na serikali hata kama ni dhahiri kwamba kuna kasoro za kimaamuzi na au za utendaji?
Ni kwa kiwango gani leo wastaafu wako huru kutoka hadharani na kusema jambo, kukemea na kushauri hatua mbadala za kuchukuliwa kwa upande mmoja, kwa upande mwingine waliokalia viti nao wawe na uvumilivu na ujasiri kama wa Mzee Rukhsa kuitikia na kumeza bila kuanza kusikia kauli za kutaka kunyamazishana kama za “wastaafu kuwashwawashwa.”
Katika hotuba hiyo ya Mei Mosi 1995 ambayo yamkini ndiyo inayoweza kuchukuliwa kuwa miongoni mwa hotuba nzito alizopata kutoa akiwa amestaafu nafasi zote, urais na uenyekiti wa CCM, pia alizungumzia habari ya mgombea binafsi. Alieleza kushangazwa kwake na uamuzi wa serikali kupinga hukumu ya mahakama ya kuruhusu mgombea binafsi ambayo alisema ni haki ya raia. Alitoa mfano wa mwanachama wa TANU huko Mbulu, Herman Sarwatt ambaye hakukubaliana na mgombea aliyesimamishwa na TANU kuwania ubunge katika jimbo hilo. Akiwa pia ni mwanachama wa TANU, alimpinga mgombea wa TANU akasimama kama mgombea binafsi, alishinda kiti hicho. Mwalimu Nyerere mwenyewe alikiri kwenda Mbulu kumpigia kampeni mgombea wa TANU, lakini walianguswa na Sarwatt.
Wakati huu tunaposheherekea maisha ya Mwalimu Nyerere na kukumbuka urathi aliotuachia, ni kwa kiwango gani tunajifunza kwa uwazi alioujenga katika kufanya kazi kama mtawala? Kubwa la yote ni kwa jinsi ambavyo hakukimbia mijadala, hali ambayo ilimpa fursa ya kuhoji yaliyokuwa yanafanywa na mrithi wake, bila kujificha kwenye kichaka cha kustaafu? Kwamba mrithi wake, hakujiona dhalili kwa kuwa tu sera zake zilichambuliwa hadharani, Rais Mwinyi naye hakujitokeza au kutuma wapambe wa kumshambulia Mwalimu ili kumnyamazisha. Ujasiri huu unaweza vipi kuchukuliwa kama somo chanya kwa wenye mamlaka kukubali wenye fikra tofauti na zao?
Tusheherekee maisha ya Mwalimu Julius Nyerere kwa kutambua urathi aliotuachia, tuutumie kujenga na kuendesha mfumo wa utawala unaokubali na kukumbatia hoja na kupokea mawazo kinzani bila kinyongo. Pengine mrithi wa Mwalimu Nyerere asingelikuwa ni mtu wa haiba ya Mzee Mwinyi kama ambavyo tumekuja kushuhudia yaliyotokea baada ya viongozi hawa, yawezekana msingi na utamaduni ambao umekuwako nchini kwa kitambo sasa kwa wastaafu kuishi nchini bila hofu, usingelikuwa kama ilivyo leo. Tuna kila sababu ya kuwaenzi Mwalimu Nyerere na Mzee Ruksa.