HISTORIA inashuhudia kwamba wapo watumwa walikataa kuwa huru kwa sababu waliamini kwamba pamoja na madhila waliyokuwa wanapata kwa bwana zao, walikuwa wanatendewa mambo mema. Ni vigumu kumwelewa mtumwa wa namna hiyo, lakini wapo. Na wanaona fahari kuendelea kuwa chini ya minyororo ya mabwana zao.
Ingawa mfumo wa utumwa ni kitu cha kale na ambacho haiingi akilini binadamu kukubali utumwa katika nyakati za sasa, bado binadamu wa leo wanaweza kabisa kuishi katika mfumo wa utumwa. Mfumo huu ni ule wa kuamua kushikamana na jambo fulani hata kama kwa akili ya kawaida kabisa limekupoka uhuru wako. Limekunyima haki yako ya kutumia utashi wako katika kuendesha mambo.
Tanzania ni nchi ya kidemokrasia inayoendesha mambo yake katika mfumo wa vyama vingi vya siasa. Mfumo huu umeshikamanisha haki ya kuendesha siasa, ama kufanya shughuli za kisiasa au hata kuchaguliwa kwenye nafasi yoyote ya uongozi, kuwa ni sharti mtu awe mwanachama wa chama cha siasa.
Kumekuwapo na mjadala mrefu, ambao pia ulihusisha kufunguliwa kesi mahakamani wa kuwapo kwa haki ya kisiasa katika nchi hii ambayo haifungamanishwi na chama cha siasa. Kushiriki siasa nchini Tanzania ni haki ambayo imefungamanishwa na chama cha siasa. Ni kwa msingi huo utaratibu wa mgombea huru/binafsi katika nchi hii haukubaliki. Ni dhahiri vyama vya siasa vimepewa haki ambayo kimsingi ni ya raia.
Ni katika kutafakari hali hii wakati Watanzania mwaka huu watashiriki uchaguzi wa serikali za mitaa na mwakani uchaguzi mkuu, lakini kama ilivyokuwa kwenye chaguzi zote zilizopita kila anayetaka kuchaguliwa kwenye nafasi ama mwenyekiti wa vijiji, wajumbe wa vitongoji, au wenyeviti wa serikali za mitaa, au udiwani, ubunge na urais mwakani, atalazimika kutokana na chama cha siasa.
Swali linalosumbua wengi kwa miaka sasa, ni kwa nini Tanzania inaogopa mfumo wa siasa ambao ni wa kidemokrasia unaoendeshwa chini ya mfumo wa chama atakacho mtu, pia uachie uhuru wengine ambao hawataki kujiunga na vyama vya siasa ila wanataka kusimama kama wagombea huru/binafsi? Ni kwa nini hata pale mahakama iliposema kuwa mgombea binafsi ni haki ya mtu, na kutaka kutungwa kwa utaratibu wa kisheria wa kuwapo kwa mgombea binafsi/huru, suala hilo halijakubaliwa katika mfumo wa utawala wa nchi yetu?
Kumekuwa na hoja nyingi kuhusu kuwekwa vigingi vya kuruhusu mgombea huru/binafsi katika nafasi za uongozi wa nchi. Miongoni mwa sababu hizi ni pamoja na dhana kwamba kuna uwezekano mgombea binafsi akawa anawakilisha matakwa ya wenye pesa chafu kutoka nje; anaweza kutumiwa vibaya kuhatarisha usalama na ustawi wa nchi, kwa ujumla inaelezwa kwamba mgombea binafsi hadhibitiki kama ambavyo ni rahisi kudhibiti chama cha siasa.
Ingawa hofu hizi zinaweza kufikirisha watu na kwa maana hiyo kusababisha watu kupata woga wa kuruhusiwa kuwapo kwa fursa ya mgombea binafsi nchini, bado kisheria mgombea binafsi akiruhusiwa nchini ni dhahiri zitawekwa taratibu za kisheria za kutimiza kabla mtu hajaruhusiwa kugombea nafasi yoyote ya mamlaka ya dola ya kuchaguliwa. Kwa maneno mengine, hofu ya udhibiti wa mwenendo wa mgombea binafsi inawezwa kuondolewa kwa kuanzishwa kwa utaratibu wa kisheria unaokubalika. Utaratibu huo ukianzishwa utasaidia kurejesha haki ya kisiasa ya mtu kuchaguliwa kuwa yake binafsi na siyo ya chama cha siasa. Kwa upande mwingine wananchi nao watakuwa na uhuru wao kuamua kuchagua watakavyo bila kuwa sehemu ya hekaheka za uanachama wa vyama vya siasa.
Hata hivyo, kuna jambo moja la muhimu ambalo halizungumzwi kuhusu haki ya mgombea binafsi. Hili ni utamaduni ambao kwa miaka na miaka limejengeka la kupoka haki binafsi kuwa haki shirikishi au haki iliyowekewa wigo ili kuipata, japokuwa ni haki ya binadamu.
Kwa miaka sasa, ukitafakari kwa undani sana mwenendo wa haki za kisiasa nchini picha inayopatikana ni kwamba kwa ujumla wetu tunataka kuaminishana kwamba haki za kisiasa nchini zinaweza kuendeshwa na zikawa na manufaa kwa sababu tu zimeshikamanishwa na chama cha kisiasa. Tumejengeana dhana kwamba bila chama cha siasa hakuna kuendesha siasa.
Ukichunguza mwenendo wa vyama vya siasa nchini, kwa kiasi kikubwa vimekuwa ni jumuiko la kudhibiti zaidi haki za kisiasa za raia badala ya kurahisisha upatikanaji wake.
Kwa mfano, jaribu kutafakari vikumbo ambavyo watu wanapigana ili tu wapate fursa ya kuteuliwa na chama cha siasa kugombea nafasi fulani fulani. Jaribu kufikiria ni mara ngapi wanachama waliamua kumpitisha mwanachama wao kugombea nafasi hizo za kuchaguliwa, lakini vikao vya maamuzi vikaamua kinyume cha utashi wa wanachama.
Kuna nyakati tulishashuhudia wenye madaraka katika vyama vya siasa wakiwatisha wanachama wenzao wanaokuwa mstari wa mbele kuhoji utendaji wa viongozi wao, kwamba hawatapitishwa na vikao vya maamuzi kugombea nafasi hizo? Ni mara ngapi kwa mfano tumesikia kauli na maonyo dhidi ya wanachama wa vyama siasa kwamba kuongoza kura za maoni (ambazo hupigwa na wanachama), siyo tikiti ya kuteuliwa kuwania nafasi ya kuchaguliwa katika nafasi za dola. Kumbe mwenye haki ya kuamua ni nani basi?
Matukio ya vyama vya siasa kutumika kama nyenzo ya kunyamazisha sauti huru za wanachama wake, hasa wale wanaoonekana kutaka uwajibikaji kwa wenye mamlaka, yamekuwa ni mengi na yamepora wengi haki zao.
Tunapotafakari hali kama hii, hakika mtu anapata hisia kwamba huenda tunapenda utumwa. Kwamba inakuwa vipi kwa mfano mbunge anayejituma kuwatumikia waliompigia kura, anayetekeleza wajibu wake sawasawa na wananchi wanampenda, aogope suala la mgombea binafsi? Kwa nini mbunge wa namna hiyo aogope uhuru wa kumwezesha kuwa huru na kutekeleza wajibu wake bila kutishwa na kauli za kukatwa jina lake kwenye kogombea?
Ukisikiliza kwa makini michango ya wabunge wengi bungeni, unapata hisia kwamba hofu ya kudhibitiwa na vyama vya siasa ni kubwa mno. Hofu hii yamkini inatokana na ukweli kwamba anajua kuwa haki yake ya kisiasa siyo mali yake, bali ya chama chake.
Tafakari ya hali hii inatoa picha kwamba huenda tumezingirwa sana na madhila ya ‘utumwa’ kwa kuwa uhuru wetu umepokwa kwa kujengwa kwa mfumo uliohalalishwa wa kuendesha siasa nchini, kiasi kwamba yeyote anayechagiza uwepo wa mgombea binafsi anaonekana kama muasi, mhaini na mtu asiyelitakia taifa mema. Tunasahau kama taifa kwamba haki ya mgombea binafsi siyo tu itaheshimu haki za binadamu katika nchi, bali pia itaongeza kiwango cha nidhamu na utii wa sauti ya wananchi katika kuamua nani awe kiongozi wao. Kuendelea kukwepa na kukataa mgombea binafsi ni sawa kabisa na kuchagua kuishi utumwani, wakati mlango kuwa huru u wazi.