Mapendekezo ya Tume Jinai, ndiyo yatasafisha Polisi

UCHAGUZI wa viongozi wakuu wa dola ni tukio muhimu sana kwa ustawi wa taifa lolote, hasa linalofuata misingi ya demokrasia. Ni kwa sababu hiyo rasilimali nyingi, fedha, muda na nguvu za watu hutumika kufanikisha mchakato wa uchaguzi.

Nchini Marekani kwa sasa hivi wako kwenye joto kubwa la uchaguzi wa rais na wabunge utakaofanyika Novemba 5, mwaka huu. Wamarekani watachagua rais ambaye ataongoza kwa kipindi cha miaka minne ijayo, pia watachagua wabunge na maseneta. Watachagua wabunge 435 na maseneta 34.

Wakati joto hilo likiwa juu, Marekani imekumbwa na taharuki ya majaribio mawili ya kutaka kumuua mmoja wa wagombea urais. Donald Trump Agosti 15, mwaka huu aliponea tundu la sindano kuuawa baada ya risasi iliyomlenga kumkosakosa na kuchana sikio lake la kulia akiwa kwenye mkutano wa hadhara. Mwezi mmoja baadaye yaani Septemba 15 mwaka huu, akiwa katika uwanja wake wa gofu akicheza, inasadikiwa alikuwa anaviziwa na mtu aliyekuwa amejiandaa kumlenga risasi. Mtu huyo raia wa Marekani anadaiwa kuwa alikuwa amejificha kichakani kwa zaidi ya saa 10 akisubiri fursa ya kummiminia risasi Trump wa chama cha Republican. Mpinzani wake katika kinyang’anyiro cha urais kwa tikiti ya Democrat ambaye pia ni Makamu wa Rais, Harris Kamala, amelaani jaribio hilo. Pia Rais Joe Biden amelaani jaribio hilo.

Matukio haya siyo ya kawaida. Jaribio la kwanza taarifa za kina hazikupatikana kwa sababu mtuhumiwa, Thomas Matthew Crooks (20) alidunguliwa akiwa juu ya paa na kuuawa, hata hivyo katika jaribio la pili, mtuhumiwa Ryan Wesley Routh (58) amekamatwa. Matukio haya mawili yanaamsha hisia kali za kisiasa ndani ya Marekani na hata ulimwenguni kote kwa ujumla. Hisia hizi zinaibuka kwa sababu katika vitu ambavyo jamii ya binadamu inapenda na mara nyingi imechagua, ni kuendesha mambo kwa uhuru, kuruhusu kila raia wa nchi kuamua nani awe kiongozi wake.

Inapotokea kwamba wale wanaotafuta ridhaa ya wananchi kuchaguliwa ili kuwaongoza, wanashambuliwa, tena katika taifa linaloaminika kuwa linafuata misingi ya demokrasia, hali ya ubaridi inakumba mataifa mengine. Hii ni kwa sababu duniani hapa kuna kawaida ya watu kuiga kutoka kwa wengine.

Jumatatu wiki hii Waziri Mkuu Kasim Majaliwa Mjaliwa akizungumza wakati wa Baraza la Maulidi, alitaka taifa litafakari na kuhoji kwa nini matukio ya kuteka watu, kupoteza watu na kuua yanatokea karibu na vipindi vya uchaguzi. Alitoa ilani kwamba ni rahisi kuwasukumia polisi lawama, lakini ni muhimu kutafakari ni kwa nini wakati wa uchaguzi na ni nani wanafanya matukio hayo.

Waziri Mkuu alisema mapema mwaka 2022 Rais Samia Suluhu Hassan alimwelekeza kuunda Tume kuchunguza tukio lililokuwa limetokea Mtwara likihusu polisi. Tume hiyo ilichunguza chombo cha ulinzi. Alieleza kuwa Tume hiyo ilifanya kazi na ikakabidhi ripoti, hatua zilichukuliwa ikiwamo kuundwa kwa Tume ya Haki Jinai. Alisema Rais Samia aliunda Tume hiyo na kuipa kazi ya kwenda kuangalia hali ilivyo nchini kote. Tume hii iliongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman. Tume hiyo ilizinduliwa na Rais Samia Januari 31, 2023 na ilikabidhi ripoti yake kwa Rais Julai mosi 2023.

Tume ya Haki Jinai ilitoa mapendekezo 360 katika kuboresha upatikanaji wa haki jinai nchini. Sasa ni mwaka mmoja na ushei tangu Tume hiyo iwasilishe mapendekezo yake. Yanawezekana kuna ambayo yamekwisha kufanyiwa kazi na mengine, labda, taratibu zinaandaliwa kutekelezwa.

Kwa mfano, Tume ilibaini kuwa hakuna mkakati mahususi wa kitaifa wa kubaini na kuzuia uhalifu ambao, pamoja na mambo mengine, ungeainisha majukumu

ya taasisi mbalimbali pamoja na vyombo vya utekelezaji na jamii kwa ujumla.

Vilevile, ilibainika kuwa vyombo vya utekelezaji sheria vimejikita zaidi katika ukamataji baada ya uhalifu kutokea na sio kubaini na kuzuia uhalifu usitokee. Mbali na ukosefu wa mkakati, pia ilionekana kuna upungufu wa vitendea kazi.

Kadhalika, Tume ilibaini kuwa vyombo vyenye mamlaka ya kukamata, mara nyingi hutumia nguvu kubwa kupita kiasi na kusababisha mateso kwa watuhumiwa. Uwepo wa taasisi nyingi zenye mamlaka ya kukamata pia ulilalamikiwa na wananchi kuwa inakuwa vigumu kutambua taasisi iliyomkamata ndugu yao na mahali alipohifadhiwa. Aidha, uwepo wa vyombo vingi vya ukamataji na vyenye mahabusu umetafsiriwa na jamii kuwa ni sababu mojawapo ya watu waliokamatwa kupotea wakiwa mikononi mwa vyombo vya dola.

Wakati haya yaliainishwa kwa kina na kwa lugha fasaha kabisa na Tume ya Haki Jinai, bado matukio ya kuteka, kutesa na kuuawa watu yamezidi kuripotiwa. Waziri Mkuu alizungumzia mambo hayo baada ya Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Dkt. Abubakar Zubeir Bin Ally kutaja matukio hayo ambayo tayari yalikuwa yametolewa tamko na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata). Katika Baraza hilo Mufti alionya juu ya kumwaga damu na kudhuru nafsi za watu wengine.

Wakati Bakwata wakiwa wametoa tamko hilo, pia Baraza la Maaskofu wa Katoliki Tanzania (TEC) na Kanisa la Kiinjili la Kiliutheri Tanzania (KKKT) nao wakiwa wametia neno katika matukio ya utekaji, utesaji na mauaji, bado nchi imejaa hofu.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema kwamba kuna uhusiano wa matukio haya na nyakati za uchaguzi. Na aliahidi kwamba maagizo ya Rais ya kufanya uchunguzi wa matukio hayo ni lazima yatatekelezwa. Watanzania wakiendelea kusubiri kufanyika kwa uchunguzi wa matukio ya kutekwa, kuteswa na kuuawa kwa wananchi, ni wakati wa kujiuliza sasa ni kwa kiwango gani na kwa kasi gani mapendelezo ya Tume ya Haki Jinai yanafanyiwa kazi. Kumekuwa na wito kwamba siyo sawa kulaumu au kunyooshea kidole Jeshi la Polisi kuhusu matukio haya yenye madhila kwa wananchi.

Hapo juu nimegusia kwa kifupi sana matukio ya majaribio ya kumuua mgombea urais huko Marekani. Mpaka sasa hivi hakuna mahali ambako matukio hayo yanaonekana kwamba ama yamepangwa na vyombo vya ulinzi vya Marekani au kufanywa navyo maja kwa moja. Mtuhumiwa mmoja aliuawa na mwingine amekamatwa. Wote hawana uhusiano na vyombo hivyo.

Kwetu ni giza nene. Haijulikani ni nani hasa yuko nyuma ya matukio haya. Hata hivyo, ukisikia simulizi za mashuhuda mbalimbali wenye taarifa za undani juu ya matukio haya mabaya, kuna harufu isiyopendeza inaelekezwa kwa vyombo vya usalama.

Ukiitafakari ripioti ya Tume ya Haki Jinai iliyokabidhiwa kwa Rais Samia Julai mosi mwaka jana, kuna shida kubwa imeizinga Jeshi la Polisi. Kwa mfano, Tume imesema kwa uwazi kwamba: “Kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi kuhusu vitendo vinavyochafua taswira ya Jeshi la Polisi.

“Malalamiko hayo dhidi ya Jeshi la Polisi yanahusu kushindwa kuzuia uhalifu,

matumizi ya nguvu kupita kiasi, kubambikia kesi, vitendo vya rushwa, mali

za watuhumiwa kupotea vituoni na kuchelewa kufika kwenye maeneo ya

matukio. Hali hiyo inasababisha wananchi kupoteza imani kwa Jeshi la Polisi

na kutokutoa ushirikiano unaotakiwa.”

Katika mazingira hayo, Tume ilipendekeza Jeshi la Polisi lifanyiwe tathmini ya kina itakayowezesha kufanyiwa maboresho makubwa na kuundwa upya ili kuondoa kasoro za kiutendaji zilizopo; Jeshi la Polisi libadilishwe kisheria, kimuundo na kifikra na kuwa Polisi Tanzania (National Police Service) ili kutoa taswira kuwa ni chombo cha kuwahudumia wananchi; na kubadilisha mitaala ya mafunzo na mtazamo wa askari wa Jeshi la Polisi ili kutoka katika dhana ya ujeshi (police force) kwenda dhana ya kuhudumia wananchi (police service).

Ni dhahiri, kama taifa tumechelewa kama tunataka kuwa watetezi wa uadilifu wa Jeshi la Polisi kama mapendelezo ya Tume ya Haki Jinai bado yanaendelea kubakia kwenye makabrasha serikalini. Tupige hatua ya kubadili polisi ili kwa pamoja tulitetee kama chombo chenye uadilifu.

spot_img

Latest articles

Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi yaanza kazi, yakaribisha wananchi kutoa maoni

Na Winfrida Mtoi Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi nchini, imesema tayari imeanza...

Urathi wa Mwalimu Nyerere usaidie kukubali kukosolewa

JUMATATU wiki hii Watanzania walikumbuka kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliyefariki...

Nimemsikiliza Gachagua, nikatamani Lowassa 2008 angelipambana vivyo

KWA zaidi ya wiki mbili sasa majirani zetu, Kenya, kumekuwa na siasa za moto....

Kukataa mgombea binafsi ni kukumbatia utumwa

HISTORIA inashuhudia kwamba wapo watumwa walikataa kuwa huru kwa sababu waliamini kwamba pamoja na...

More like this

Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi yaanza kazi, yakaribisha wananchi kutoa maoni

Na Winfrida Mtoi Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi nchini, imesema tayari imeanza...

Urathi wa Mwalimu Nyerere usaidie kukubali kukosolewa

JUMATATU wiki hii Watanzania walikumbuka kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliyefariki...

Nimemsikiliza Gachagua, nikatamani Lowassa 2008 angelipambana vivyo

KWA zaidi ya wiki mbili sasa majirani zetu, Kenya, kumekuwa na siasa za moto....