Ni kiburi kibaya Polisi kusigina R4 za Rais

Hakuna ubishi kwamba Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha kwa matendo halisi nia yake ya kutaka kufanya mabadiliko mengi muhimu katika uendeshaji wa mambo nchini. Nitataja machache.

Mara tu baada ya kuingia madarakani Machi 2021 aliamua kufungua nchi. Na alisema anakwenda kufungua nchi. Aliibuka na mkakati wake wa R4 kwa kimombo Reconciliation, Resilience, Reforms na Rebuild, kwa Kiswahili ni Maridhiano, Ustahimilivu, Mabadiliko na Kujenga tena.

Tuliona akichukua hatua za kuondoa amri nyingi zilizokuwa zinakiuka sheria zilizokuwa zimewekwa na mtangulizi wake, John Magufuli, kama kuharamisha mikutano ya vyama vya siasa. Kwa mara ya kwanza baada ya miaka zaidi ya sita, tuliona haki ya Watanzania kushiriki mikutano ya kiasiasa ya hadhara na maandamano vikirejea.

Ilikuwa ni kama Tanzania mpya, tuliposhuhudia Jeshi la Polisi likisimamia usalama wa maandamo ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) yaliyofanyika Jiji Dar es Salaam na baadaye katika mikoa mingine nchini kote. Tuliona vyama vya siasa vya upinzani vikifanya mikutano ya kujinadi kwa wananchi. Kote huko, hatukuona mtu yeyote akifanya uhalifu. Hatukusikia duka la mtu limeporwa, ukiacha watu fulani waliokuwa na nia ovu ya kutaka kuleta rabsha katika viwanja vya Mwembe Yanga jijini Dar es Salaam kuzuia mkutano wa CHADEMA. Tunakumbuka hekima ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mobare Matinyi, alivyoepusha shari iliyokuwa inapaliliwa mahali pale.

Kwa ujumla, hali ya kisiasa imekuwa na utulivu mkubwa. Vyama vya siasa vimekuwa na ratiba zao kufanya mikutano katika maeneo mbalimbali nchini. Wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikikatiza huko na huko kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025, vyama vya upinzani navyo vimekuwa vikipita huko na huko kukumbusha ni wapi kazi haijatendeka ipasavyo. Siasa inapigwa.

Ustawi huu wa kisiasa uliasisiwa mwaka 1992 mara tu Taifa hili lilipoamua kuingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa. Ulikuwa ni uamuzi wa nchi. ikatungwa sheria ya vyama vya siasa. Vyombo vya dola kama Jeshi la Polisi, Jeshi la Wananchi la Ulinzi, Jeshi la Magereza, pamoja na watendaji wa mahakama wakaondolewa kwa sheria kuwa wafuasi wa vyama vya siasa.

Hata hivyo, safari haikuwa ya mteremko, Taifa limepita katika mapito mengi. Mwaka baada ya mwaka likipiga hatua. Ilipofika mwaka 2015, taifa lilikuwa limeneemeka kisiasa, Bunge lillikuwa ni moja ya mihimili ya dola iliyokuwa inatekeleza wajibu wake kwa ufanisi mkubwa. Kwa mara ya kwanza, kiongozi mkuu wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, akawaambia wanachama wa chama chake kwamba hawawezi kuendelea kutegemea polisi kushinda uchaguzi, akataka chama chake kijijenge kisiasa, kutafuta uhalali wa kukubalika kwa wananchi.

Ni bahati mbaya sana kwa taifa hili, kwamba uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ulitoa matokeo ambayo wengi waliokuwa upande wa chama tawala hawakufurahishwa nayo. Na ndiyo mwaka Tanzania ilishuhudia mchuano mkali zaidi wa kisiasa kwa kiwango cha juu kabisa.

Kwa kuwa wapo waliojaa hofu baada ya kuona matokeo hayo, mwaka 2016 hadi Machi 2021, nchi ilipitishwa katika tanuru la moto mkubwa. Mauaji, mateso, uonevu, uporaji, uvunjaji wa haki za raia, uvunjaji wa sheria na katiba na mambo mengine yasiyoelezeka. Ndiyo hali aliyoikuta Rais Samia.

Kwa bahati mbaya, kama ambavyo alipata kusema kwamba ndani mwake pia wapo wasiotaka maridhiano, ndicho kitu ambacho Jeshi la Polisi limeonesha wiki hii mkoani Mbeya. Jeshi hilo limetumia nguvu kubwa kukamata viongozi wa CHADEMA na wafuasi wao na kuzuia kufanyika kwa mkutano wao wa kuadhimisha siku ya vijana dunani.

Sababu zilizotolewa na Jeshi la Polisi za kuharamisha mkutano na maadamano ambayo yangefanyika Mbeya mapema wiki hii, ni aibu na fedheha kwa chombo hicho chenye dhima ya kulinda maisha na mali za raia.

Kinachoonekana kutoka ndani ya Jeshi la Polisi ni mazoea ya kutaka kujinufaisha na uovu ambao wamekuwa wanatenda miaka na miaka katika nchi hii. Ukisoma taarifa ya Polisi na ukisikiliza kauli za maofisa wa polisi juu ya kilichotokea Mbeya, siyo tu unapata majibu kwamba bado wapo katika matamanio ya uovu wa kudidimiiza haki za raia, bali pia wana maslahi binafsi na hali ya uvunjaji wa sheria hizo.

Rais Samia aliunda Tume ya Haki Jinai, na Julai mwaka jana ilimkabidhi ripoti, kisha akaunda Kamati pana zaidi kufanyia kazi mapendekezo ya Tume hiyo. Kamati hiyo iliyoongozwa na Jaji Mkuu Mstafuu Mohamed Chande Othman, Juni mwaka huu iliwasilisha ripoti yake kwa Rais. Yapo mambo mengi makubwa yanapendelezwa kufanyiwa marekebisho ili mfumo wa taifa hili wa haki jinai ufanye kazi sawasawa. Jeshi la Polisi ni miongoni mwa taasisi sita zinazohusika na mfumo wa haki jinai. Kwa bahati mbaya, wakuu wa chombo hiki ni kama wanaelekea magharibi wakati Rais mwenye serikali yake akielekea na kutaka nchi ielekee mashariki.

Yamekuwako mapendekezo ya kufanyiwa marekebisho makubwa Jeshi la Polisi kuwa chombo cha kutoa huduma. Mabadiliko haya kwa bahati mabaya yatahusu fikra, tabia na sheria ili kuondokana na dhana ya Jeshi la Polisi ya kutumia misuli tu, sasa kutumia zaidi maarifa na ujuzi.

Ukiacha Inspeka Jenerali wa Polisi (IGP) mstaafu Said Mwema, ambaye alikuwa na upeo wa kutaka na kutamani sana Jeshi la Polisi libadilike kwenda kwenye chombo cha kuhudumia wananchi, ni vigumu kumwona mwingine ambaye anawaza katika mwelekeo huo. Ni jambo la bahati mbaya kwamba maono ya Rais Samia na ambayo kwa hakika yamesaidiwa pia kusukumwa na Tume ya Haki Jinai, ni kama  hayana wa kuyafanyia kazi ipasavyo ndani ya Jeshi hilo.

Kwa mfano, ni vigumu kuelewa kwa hatua za ovyo zilizochukuliwa na Jeshi la Polisi mkoani Mbeya zilikuwa na faida gani, kwanza kwa jeshi hilo lenyewe, kwa hadhi ya serikali na nchini mbele ya Jumuiya ya kimataifa kama siyo kuidhalilisha nchi kuwa inashabikia vitendo vya uvunjaji wa sheria na kukanyaga haki za raia wake?

IGP Camilus Wambura na makamanda wake wanaweza kusema wamesaidia nini nchi kwa yaliyofanyika Mbeya? Wamepata nini mbali tu ya kuendeleza vitendo ambavyo dhahiri vinakinzana na msimamo wa Rais kuhusu R4?.

Rais Samia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, ndiye anayechagua IGP, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Mkuu wa Jeshi la Magereza, Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (DGIS). Hawa wote ni wasaidizi wakuu wa Rais, ndiyo wanaopaswa kumsoma Rais kwa bidii kubwa na kumsaidia kutekeleza kwa vitendo zile R4 ambazo zinaangukia kwenye maeneo yao. Kama hawawezi, kuna shida.

Tangu aingie madarakani Rais Samia amefanya kazi na DGIS wanne, yeye ndiye anajua kwa nini amekuwa nao wengi ndani ya miaka mitatu na miezi minne hivi. Hakuna wa kumuuliza, ni mamlaka yake Kikatiba. Hata hivyo, kama kuna msaidizi wa Rais ambaye anatamani kumrejesha katika giza la kuuawa kwa watu ovyo, kutekwa kwa watu ovyo, kuzuia haki za raia za kukusanyika kwa amani na kufanya shuguli zao za kijamii, kisiasa au kiuchumi, huyo hakika hana msaada wowote mbali ya kumchonganisha na wananchi. Sijui ni kwa nini kila nikimwangalia IGP Wambura ninakumbuka kesi ya ugaidi dhidi ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Mwandishi wa Makala haya ni Mkurugenzi wa Media Brains

spot_img

Latest articles

Tulia alipoteza fursa ya kuokolewa uhai wa Kibao

INAWEZEKANA Agosti 27 2024 ilikuwa ni siku ambayo maisha ya Ally Mohamed Kibao yangeokolewa...

DCEA yakamata kilo 1,815 za skanka

Na Mwandishi Wetu Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imewakamata...

Waziri Mkuu: Suala la mazingira liwe ajenda ya Kitaifa

Na Mwandishi Wetu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema suala la uhifadhi wa mazingira liwe...

NECTA yawaonya wamiliki na wakuu wa shule

Na Winfrida Mtoi Baraza la Mtihani la Tanzania (NECTA), limewataka wamiliki na wakuu wa shule...

More like this

Tulia alipoteza fursa ya kuokolewa uhai wa Kibao

INAWEZEKANA Agosti 27 2024 ilikuwa ni siku ambayo maisha ya Ally Mohamed Kibao yangeokolewa...

DCEA yakamata kilo 1,815 za skanka

Na Mwandishi Wetu Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imewakamata...

Waziri Mkuu: Suala la mazingira liwe ajenda ya Kitaifa

Na Mwandishi Wetu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema suala la uhifadhi wa mazingira liwe...