Enyi Polisi amkeni sasa, mtakuja kuvuna mabua

MAADHIMISHO ya wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani kitaifa yatafanyika Jijini Dodoma Agosti 26 mwaka huu. Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango atakuwa mgeni rasmi. Maadhimisho haya, japo yamekuwa ni ya kiutaratibu tu, yangeliweza kuwa na maana kubwa kama yangechukuliwa kwa uzito unaostahili katika kukabiliana na suala la usalama barabarani, badala yake ni kama yamekuwa ya kuuza tu stika za kubandika kwenye magari.

Vyanzo vya habari kutoka safu za mashirika ya kimataifa yanayohudumu hapa nchini na hata ofisi za balozi za nje, zinasema kuwa miongoni mwa mambo ambayo wafanyakazi wao wanaoletwa kufanya kazi nchini wanayotakiwa kuwa makini nayo, ni suala la usalama barabarani. Wanaelezwa wazi kwamba kinachoua watu wengi sana katika bara la Afrika na hususani Tanzania, siyo magonjwa, bali ajali za barabarani.

Janga la ajali za barabarani katika miaka ya hivi karibuni limeongezeka kutokana na kuongezeka kwa aina ya vyombo vya usafiri vinavyoruhusiwa kubeba abiria kibiashara. Vyombo vilivyokuwa vimezoeleka kwa shughuli ya kubeba abiria kibiashara ni magari kama mabasi makubwa na madogo pamoja na magari madogo yaliyosajiliwa kama teksi. Hata hivyo, uhitaji wa vyombo vya usafiri na changamoto za gharama kwa wasafiri ikijumuisha na msongamano mkubwa wa magari, pikipiki na bajaji nazo ziliingia katika shughuli ya kusafirisha abiria kibiashara.

Katika miji mingi kama siyo yote nchini kwetu, pikipiki na bajaji ndiyo usafiri unaotumiwa na watu wengi. Zipo sababu za watu kupendelea usafiri huu, kwanza ni uwezo wa vyombo hivyo kukwepa foleni kubwa za magari, lakini pia uharaka wa kufikisha abiria wanakokwenda na kubwa ya yote gharama za nauli zake ni rafiki kwa wenye kipato kidogo.

Ukitafakari kwa kina ni kama vyombo hivi vya usafiri, yaani pikipiki maarufu kama bodaboda na bajaji, ndivyo vimeteka miji mingi. Vinafanya kazi kubwa ya kusafirisha abiria. Usiku na mchana. Wengine ambao tunatoka vijijini zile njia za miguu zilizokuwa zinatumika kutembea kutoka kijiji kimoja hadi kingine, labda kuvuka mto, kwa sasa zimekufa. Sababu ya kufa kwake ni moja tu, hata watu wa vijijini nao hawatembei tena umbali mrefu. Pikipiki zimebadili mfumo mzima wa maisha yao. Wapo wanaoita bodaboda au bajaji kuwapeleka sokoni, msibani, kanisani, kwanye sherehe na sehemu nyingine ya matukio ya kijamii. Vyombo hivi vya usafiri vimeleta mabadiliko makubwa ya mtindo wa maisha.

Kwa bahati mbaya kama walivyosema wahenga, kwamba kila masika huja na mbu wake, kama bodaboda na bajaji ni neema ya kutatua changamoto ya usafiri kwa watu wa kipato cha chini, zimeachwa pia kuwa chanzo kikubwa cha maafa. Vyombo hivi, hasa bodaboda, zinasababisha ajali nyingi mno kila leo.

Kwa zaidi ya muongo mmoja na ushei bodaboda zimetawala shughuli ya usafiri nchini, awali ilionekana kama vyombo hivi vya usafiri vingeliweza kudhibitiwa chini ya sheria za usalama barabarani ambazo zinasimamia vyombo vingine vya moto, kama magari, lakini kiuhalisia kadri siku zinavyokwenda ndivyo udhibiti wake unakuwa mgumu kiasi cha kuwafanya askari wa usalama barabarani kunyoosha mikono juu.

Ni kawaida kabisa kuona dereva wa bodaboda akipita kwenye taa nyekundu mbele ya trafiki, hajavaa kofia ngumu, kapakia mshikaki, na kwa ujumla hana ulinzi wowote wa mavazi ya kuendesha pikipiki. Ni kawaida kabisa dereva wa bodaboda kuendesha mwelekeo usioruhusiwa kwenye barabara kuu, na trafiki wala hawajishughulishi nao. Utukutu huu wa madereva wa bodaboda, kutokujali kuheshimu sheria za usalama barabarani, kuendesha vyombo vya moto wakiwa wamelewa, kutokuzingatia ishara za usalama barabarani, kutokuwa na leseni ya udereva, kutokukata bima ya vyombo vya moto, ni mambo ambayo yamechangia ajali nyingi, aghalabu zikiacha wengi na vilema vya kudumu na hata vifo.

Hospitali nyingi za umma mijini, zimejaa majeruhi wa ajali za bodaboda. Tabia ya uendeshaji wa bodaboda bila kutii sheria za usalama barabarani, imekuwa janga la taifa.

Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Ramadhani Ng’anzi, hivi karibuni alisikika akizungumzia maadalizi ya siku ya maadhimisho ya wiki ya usalama barabarani ambayo kitaifa itakuwa Agosti 26, jijini Dodoma. Alisema wamejipanga katika maadhimisho haya kuelekeza nguvu katika kutoka elimu kwa madereva wa bodaboda na bajaji.

Ukitafakari kauli ya Kamanda Ng’azi utapata ujumbe mmoja muhimu, kwamba labda sasa Jeshi la Polisi limesikia kilio cha kila siku kuwa kuna kila sababu ya kudhibiti mwenendo wa madereva wa bodaboda nchini. Kwamba ajali wanazosababisha kila leo, ni moja ya majanga ya kujitakia. Kwamba haielezeki kwamba eti polisi wa Tanzania wote, wameshindwa kudhibiti mienendo hii isiyofaa. Uendeshaji wa fujo, uvunjaji wa sheria za usalama barabarani vitu ambavyo vimekuwa ni utamaduni wa madereva hawa.

Tumeshuhudia mara nyingi trafiki wakikimbizana na magari mpaka uchochoroni pale dereva alipovunja sheria ya usalama  barabarani na ama akakataa kusimama alipotakiwa kufanya hivyo, au alimkimbia trafiki baada ya kutenda kosa ili kuepuka adhabu. Tumeshuhudia trafiki wakiomba msaada wa kuongezewa nguvu kudhibiti madereva watukutu, wasiotii sheria za usalama barabarani. Kama trafiki wanamudu kufanya hivyo kwa madereva wa magari, ni nini kinawashinda kwa madereva wa bodaboda?

Kama polisi wanaweza kupambana na majambazi yenye silaha mpaka wanayazidi nguvu, ni kitu gani hasa kinawashinda kwa madereva wa bodaboda? Kama polisi wanaweza kufanya upelelezi wa wahalifu na kukamilisha uchunguzi na kuwasilisha ushahidi mahakamani, ni nini kinashindikana kwa bodaboda?

Madereva wa bodaboda na wamachinga katika miaka ya hivi karibuni wamekuwa ni mtaji mkubwa wa wanasiasa. Bodaboda wanatumika kufanikisha harakati nyingi za kisiasa za baadhi ya wanasiasa. Kama ilivyo kwa wamachinga, wanaonekana kuwa ni mtaji wa kisiasa wa baadhi ya wanasiasa kufanikisha malengo yao. Hali hii ndiyo inasababisha madereva wa bodaboda kuvimba vichwa kwa upande mmoja na trafiki kuingiwa baridi kwa upande mwingine katika kusimamia sheria.

Pengine sasa kwa tamko la Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani juu ya mwenendo wa madereva wa bodaboda na bajaji katika dhima ya maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani mwaka huu, labda kuna dawa inaandaliwa kurejesha madereva hawa katika mstari unaostahili.

Hata hivyo, ni vema angalizo likawepo, ni hakika kama hatua za haraka za kudhibiti madereva wa bodaboda hazitachukuliwa sasa, kama taifa tujue tu, tunapalilia kujengeka kwa genge baya katika jamii na tusije kushangaa likawa kichocheo cha uasi mbaya katika taifa letu. Tuwe na tahadhari, sasa ni wakati wa kudhibiti mwenendo usiofaa wa madereva wa bodaboda.  Wanasiasa watapita, lakini nchi yetu itabaki. Yeyote anayewapa kiburi madereva hawa, naye adhibitiwe. Mchelea mwana kulia, hulia yeye. Tutafakari.

spot_img

Latest articles

Tulia alipoteza fursa ya kuokolewa uhai wa Kibao

INAWEZEKANA Agosti 27 2024 ilikuwa ni siku ambayo maisha ya Ally Mohamed Kibao yangeokolewa...

DCEA yakamata kilo 1,815 za skanka

Na Mwandishi Wetu Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imewakamata...

Waziri Mkuu: Suala la mazingira liwe ajenda ya Kitaifa

Na Mwandishi Wetu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema suala la uhifadhi wa mazingira liwe...

NECTA yawaonya wamiliki na wakuu wa shule

Na Winfrida Mtoi Baraza la Mtihani la Tanzania (NECTA), limewataka wamiliki na wakuu wa shule...

More like this

Tulia alipoteza fursa ya kuokolewa uhai wa Kibao

INAWEZEKANA Agosti 27 2024 ilikuwa ni siku ambayo maisha ya Ally Mohamed Kibao yangeokolewa...

DCEA yakamata kilo 1,815 za skanka

Na Mwandishi Wetu Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imewakamata...

Waziri Mkuu: Suala la mazingira liwe ajenda ya Kitaifa

Na Mwandishi Wetu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema suala la uhifadhi wa mazingira liwe...