Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa na utamaduni wa kualika vyama rafiki kuhudhuria katika mikutano yake. Katika Mkutano Mkuu wa CCM wa mwaka 2005 uliofanyika Dodoma, ambao ulikuwa ni wa kuchagua mgombea urais kupitia chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo, miongoni mwa vyama vilivyokaribishwa kilikuwa chama cha Kenya African National Union (KANU) ambacho kilitawala Kenya tangu uhuru mwaka 1963 mpaka kilipoangushwa kwenye uchaguzi wa vyama vingi wa Disemba 2022 na Muungano wa Vyama uliojulikana kama National Rainbow Coalition (NARC).
Ni uchaguzi uliofikisha mwisho zama za KANU katika siasa za Kenya. Katika mkutano huo, mwakilishi wa KANU alipopata fursa ya kuzungumza alikuwa na ujumbe huu kwa CCM: “Ninawaomba mchunge sana msipoteze madaraka.”
Mwakilishi wa KANU alikuwa anawasilisha ujumbe huo kwa wanachama wa CCM akiwakumbusha na kuwaasa kuwa kuwa na madaraka kuna raha yake. Kwa upande wao, KANU ambacho kiliasisiwa na Rais wa Kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta aliyeongoza Kenya tangu mwaka 1963 hadi mwaka 1978 na kisha kupokewa na Daniel arap Moi hadi alipostaafu mwaka 2002, kilikuwa kinajuta kuwa chama cha upinzani nchini Kenya. KANU ilitawala Kenya kwa takribani miaka 40; miaka 24 ya Moi na miaka kama 15 ya Kenyatta.
KANU siyo chama cha kwanza kwa vyama vilivyoleta uhuru kwa nchi mbalimbali za bara la Afrika kupoteza madaraka, ama kupitia sanduku la kura au kwa njia ya mapinduzi ya kijeshi. Katika nchi zote za Afrika Mashariki, yaani Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi ni Tanzania tu chama chenye nasaba na kile kilicholeta uhuru bado kingalipo madarakani.
Uhuru wa Tanganyika uliletwa na TANU mwaka 1961, wakati Zanzibar uhuru wao ijapokuwa ulikuwa ni kwa mapinduzi, uliletwa na ASP. Tanganyika na Zanzibar zilipoungana mwaka 1964 na kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwaka 1977 vyama hivyo, yaani ASP na TANU viliungana na kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi.
Ukitafakari hali ya vyama vya siasa vilivyopigania uhuru barani Afrika kwa kweli vinazidi kupukutika. Chama cha mwisho kabisa kilicholeta uhuru katika nchi za Afrika ni African National Cogress (ANC) nchini Afrika Kusini mwaka 1994. Kwa maneno mengine ANC imetawala Afika Kusini kwa miaka 30 sasa.
Kwenye kila uchaguzi mkuu uliofanyika Afrika Kusini tangu mwaka 1994, chaguzi sita, ANC haijawahi kupata kura chini ya asilimia 50, isipokuwa uchaguzi wa mwaka huu 2024. Kwa maana hiyo ANC kwa miongo mitatu mfululizo imeshikilia kuwa chama bora kabisa chenye nguvu chenye ridhaa ya wananchi kuongoza kupitia sanduku la kura.
Matokeo ya kura yaliyotangazwa wiki iliyopita yameacha mshangao na gumzo kubwa nchini Afrika Kusini na dunia kote kwa ujumla. ANC kwa mara ya kwanza kimepata kura chini ya asilimia 50, hali ambayo sasa inakilizamisha kutafuta mshirika wa kuungana naye kuunda serikali. ANC imeongoza kwa kupata asilimia 40.18, Democratic Alliance (DA) 21.81%, Chama cha uMkhonto weSizwe (MKP) 14.58% na Economic Freedom Fighters (EFF) 9.52%. Vipo vyama vingine vingi pia. Matokeo haya ni kama yamwepindua meza za siasa za Afrika Kusini.
Ukitafakari sana matokeo haya utaona kitu kimoja kikubwa ambacho kinanyonyoa nguvu za ANC ni magomvi ndani ya chama hicho. Pamoja na changamoto za shida za wananchi ambao bado Weusi waliowengi wanaona kuwa maana ya uhuru kwao haijatimia kutokana na suala la ardhi kubwa kuendelea kukaliwa na Weupe wachache, magomvi ya ndani ya chama ni kwa muda sasa, kuanzia kufukuzwa kwa Rais Thano Mbeki, baadaye kufukuzwa kwa Jacob Zuma na hata kutimuliwa kwa Julius Malema aliyekuwa kiongozi wa vijana wa ANC, ni chanzo kikubwa kupoteza nguvu.
Katika uchaguzi huu kwa mfano, aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma na chama chake kipya cha MKP amepata 14.18%, ukichukua na za EFF cha Julius Malema asilimia 9.52, ingawa alitarajiwa kupata zaidi kutokana na sera zake za ardhi, vimenyofoa ‘mnofu’ wa ANC. Ukijumlisha kura hizi ni asilimia 23.7 ambazo kama siyo jadi ya mizozo ya ANC hizi zingelikuwa kura zake.
Hawa (Zuma na Malema) walikuwa wandani wa ANC. Kwa hiyo mwaka baada ya mwaka ANC inapoteza nguvu kutokana na mizozo. Mzozo wa Zuma, ndiyo wa karibuni zaidi. Mnofu aliochomoka nao Zuma kutoka ANC ni mkubwa mno, asilimia 14.18. Huu ungebaki ANC ingeshinda kwa zaidi ya asilimia 54.
Ingawa hesabu za kisiasa hazipigwi hivyo, bado kuna somo moja muhimu la kujifunza juu ya utulivu na ustahimilivu wa vyama vya siasa kama vinataka kusonga mbele. Hapo juu nimetaja KANU, tangu ilipopoteza madaraka mwaka 2002 imekuwa kama iliyokuwa Uganda People’s Congress (UPC) ya Milton Obote, rais wa kwanza wa Uganda, UNIP ya Zambia na vingine vingi.
Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine za Afrika hatuna tofauti kubwa ya kimuundo, kimaadili na mikakati ya kuendesha vyama vya siasa na harakati zenyewe za kisiasa. Kwa mfano, mtu anaweza kujiuliza ni nini hasa kilivisibu vilivyochokuwa vyama vikuu vya upinzani Tanzania, Civic United Front (CUF) na NCCR-Mageuzi. Je, ni kwa kiwango gani vyama hivyo vilisukwasukwa na migogoro ambayo hatimaye ilivinyong’onyesha na sasa kubaki hoi bin taaban kisiasa?
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 CCM ilishuhudia kwa mara ya kwanza uwezekano mkubwa wa kupoteza madaraka. Hali hiyo ilitokana na mizozo ya ndani ya kuminya haki za wanachama wake nafasi ya kugombea nafasi ya urais. Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Marehemu Edward Lowassa, alienguliwa kwa hila kwenye mchakato wa kuomba ridhaa ya chama chake kugombea nafasi ya urais.
Lowassa alijiondoa CCM na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuteuliwa kuwania urais. Uchaguzi wa mwaka 2015 uliibua hamasa kubwa. Kwa mara ya kwanza CCM ilipoteza majimbo mengi katika miji mikubwa ya nchi, lakini pia ikipoteza mabaraza ya madiwa katika majiji yote ya nchi hii.
Mizozo ndani ya vyama vya siasa ni sumu. Ndiyo maana kwa wanaozijua siasa za Kenya aliyekuwa Rais wa Kenya Moi, anatajwa kuwa bingwa wa kuwapenyezea wenzake kwenye vyama vyao mizozo.
Na ndiyo maana hata baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwanzoni mwa miaka ya 90, Moi aliendelea kushinda uchaguzi hata kama idadi ya kura za jumla za wapinzani wake zilikiwa nyingi kuliko zake. Biashara ya Moi inatajwa kuwa ni kupenyesha mizozo kwenye vyama pinzani.
Mfumo wa kupenyeza mizozo kwenye vyama vya siasa ni mbinu ambazo hapa Tanzania imeshika kasi. Ni nani hasa muhusika wa udhia huo, ni swali la kujiuliza.
Hata hivyo, yafaa kujiuliza sasa baada ya matokeo ya uchaguzi Afrika Kusini siasa za Tanzania zina lolote la kujifunza? Je, wimbi la vyama vya ukombozi kuendelea kufungaswa virago litaendelea barani Afrika?
CCM na ANC ni vyama rafiki. Ni marafiki wa kweli, chanda na pete. Matokeo haya kwa vyovyote siyo habari njema kwa CCM. Siyo habari njema pia kwa vyama vingine vichache vya ukombozi vilivyobakia barani Afrika kama Frelimo huko Msumbuji, Swapo huko Namibia, MPLA huko Angola na BDP huko Botswana, kwa sababu siasa za nchi za Kiafrika zina tabia ya kuambukizana.
Sababu kubwa matatizo ya nchi za Afrika zinafanana sana. Kukosekana kwa uwajibikaji miongoni mwa watawala, wizi wa mali ya umma, kukosekana kwa ajira, mifumo ya utawala isiyozingatia weledi na kwa kiwango kikubwa kujengeka tabia ya upendeleo kwenye fursa zilizoko nchini.
Wenye madaraka kuyabinafsisha na kuyashikamanisha ama na familia zao au ‘magenge’ wanayoyazalisha ili kujiimarisha madarakani. Itoshe tu kusema kansa inayokula vyama vya ukombozi barani Afrika bado ina nguvu na inaendelea kuteketeza.