TANZANIA ni nchi salama sana dhidi ya majanga ya asili kama vimbunga, matetemeko ya ardhi na hata mafuriko. Yako mataifa ambayo majanga ya asili ni ya kila mara. Katika nchi hizo sera na sheria mbalimbali zimebuniwa ili kusaidia jamii kukabiliana na madhara ya majanga hayo.
Miongoni mwa nchi zinazosumbuliwa na majanga ya asili kama matetemeko ya ardhi ni pamoja na Japan, Uturuki na Syria. Februari mwaka 2023 Uturuki na Syria zilikumbwa na tetemeko kubwa la ardhi lenye ukubwa wa kipimo cha 7.8 na jingine la 7.6. Maafa ya matetemeko hayo yaliyotajwa kutokushuhudiwa kwa karne moja iliyopita, yalikuwa makubwa sana. Inakisiwa zaidi ya watu 50,000 walikufa, huku zaidi ya majengo 156,000 yakibomoka. Malaki ya wananchi walikosa makazi.
Serikali ya Uturuki ilitoa hati zaidi ya 100 za kukamatwa kwa wahandisi, wasanifu majengo na wakandarasi waliohusika katika ujenzi wa majengo hayo. Watu hao walitakiwa kukamatwa kwa sababu iliaminika kwamba walihusika katika kukiuka masharti ya ujenzi unaozingatia mbinu za kuhimili matetemeko ya ardhi. Kesi mbalimbali zinaendelea mahakamani zikihusu mashitaka ya uzembe na kushindwa kuzingatia kanuni za ujenzi dhidi ya matetemeko ya ardhi.
Kama nilivyoeleza hapo juu kwamba Tanzania hatuna tatizo kubwa la majanga ya asili, na kwa maana hiyo majanga hayo hayajawahi kuwa ni jambo linalosumbua sana watunga sera, sheria na kanuni katika ujenzi. Hivyo, tunaposikia na kuona majanga ya matetemeko ya ardhi makubwa yanayotokea kwingineko duniani, au tunapoona vimbunga vinavyoleta madhara katika nchi zinazopatwa na majanga hayo mara kwa mara, tunapaswa kumshukuru Mungu kwamba ametuondolea kikombe hicho hivyo kutufanya tuishi kwa usalama zaidi.
Hata hivyo, pamoja na neema hiyo ya kuepushwa na majanga hayo, tunayo majanga yetu. Haya ni majanga tunayotengeneza wenyewe kwa sababu kuu moja, kutokuwa makini sana katika kuzingatia kanuni za usalama hasa katika ujenzi. Tumeona watu wetu wakijenga kwenye njia za mito, kwenye mabonde ambako kimsingi hakufai kwa makazi ya binadamu. Tameshuhudia makazi ya wananchi yakizingirwa na maji au mafuriko mara kwa mara. Wapo watu walioamua kuishi maeneo hatarishi na kila mwaka wanavumilia adha ya mafuriko. Haya ni majanga ya kujitengenezea kama siyo kujitakia.
Katika eneo la ujenzi nako kuna changamoto nyingi. Hizi ni za kujenga bila kuzingatia sheria, taratibu na pengine ubora wa viwango vya vifaa vya ujenzi. Katika miji mingi ya Tanzania kuna ujenzi mwingi holela. Vyombo vya usimamizi wa ujenzi mijini ni kama vimezidiwa nguvu au vimeamua kupumzika huku kasi ya wananchi ya kujenga ikiongezeka kila uchao.
Katika mazingira ya mwamko mkubwa wa wananchi kujenga majengo mapya makubwa, ya ghorofa, ukiwa juu na uhitaji wa majengo hayo ukiwa juu pia, ingelitarajiwa kwamba vyombo vya usimamizi siyo tu navyo vingeongeza kasi na umakini, bali pia vingejibidiisha kutafuta vifaa vya kisasa vya kuwasaidia kurahisisha kazi yao ya ukaguzi na usimamizi.
Ajali ya kupomoka kwa jengo la ghorofa nne iliyotokea mwishoni mwa wiki katika eneo lenye pilika nyingi za kibiashara nchini, Kariakoo Dar es Salaam, imetukumbusha kwa mara nyingine kuwa tumejiachia sana. Wakati tukiungana kama taifa kuwapa pole wote waliokumbwa na janga hilo, tukiwapa pole wafiwa wote na kuwatakia majeruhi uponyaji wa haraka, janga hili linatufikirisha sote.
Watu wengi ambao wamezungumzia janga hilo wamesema wazi kwamba, kengele ya uwezekano wa kutokea kwa kitu kama hicho ilipigwa mwaka 2006 baada ya kuporomoka kwa jengo jingine la ghorofa la Chang’ombe Village Inn eneo la Keko jijini Dar es Salaam. Ajali hiyo ambayo iliua mtu mmoja na kujeruhi wengine kadhaa, ilimsukuma aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, Edward Lowassa, kuunda tume ya kukagua maghorofa yote katika jiji la Dar es Salaam.
Tume ya Lowassa ilikamilisha kazi yake, ijapokuwa mwenyewe hakuwa madarakani, aliyekuwako wakati ripoti inakamilika alikuwa ni Mizengo Pinda. Pinda akihitimisha mjadala wa bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu Bungeni kwa mwaka wa fedha wa 2008/2009 aliliambia Bunge kuwa jumla ya majengo 505 yalikaguliwa, kati ya hayo 147 hayakuwa na nyaraka za ujenzi, 81 yalikuwa yamekiuka masharti ya ujenzi, majengo 22 wamiliki wake hawakupatikana mpaka tume inakamilisha kazi yake, huku taratibu za ujenzi na sheria katika majengo hayo vikiwa havikuzingatiwa.
Kutokana na kilichoonekana kati ya 2006 – 2009, ni dhahiri hatua za udhibiti wa taratibu wa ujenzi wa majengo, hasa ya ghorofa, ilipaswa kuimarishwa ili kuepuka janga kama hili ambalo limetokea wiki iliyopita Kariakoo.
Hakuna ubishi kwamba Kariakoo ni eneo maarufu la biashara na ndiyo maana limepewa hadhi ya soko la biashara la kimataifa. Kariakoo zinafanyika shughuli nyingi sana za kibiashara. Mataifa kadhaa ya jirani kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zambia, Malawi, Burundi, Rwanda na Uganda wafanyabiashara wao wanafika kununua vitu. Mapato ya kodi kwa eneo la Kariakoo ni makubwa. Utitiri wa wafanyabiashara umejaa Kariakoo.
Pamoja na umuhimu huu wa kiuchumi wa soko la biashara la kimataifa la Kariakoo, eneo hili linaacha maswali mengi sana kuhusu usalama. Maswali haya ya kiusalama yanajikita katika ujenzi wa miundombinu hasa majengo, ambayo yamesongamana sana. Nafasi kati ya jengo na jengo Kariakoo ni finyu sana kiasi kwamba katika mazingira ya majanga kama la wiki iliyopita utoaji wa huduma za uokoaji zinakuwa na changamoto nyingi.
Mitaa mingi ya Kariakoo haipitiki kwa urahisi kwa sasa. Barabara karibia zote zimevamiwa na wafanyabiashara wamachinga ambao wamepanga meza zao kandokando ya barabara sehemu zote mbili, wapo waliomwaga bidhaa zao katikati kabisa ya barabara. Yaani kutembea hata kwa miguu katika mitaa mingi ya Kariakoo ni changamoto kubwa.
Ni hakika kama hatua za haraka za kiusalama na kitaalamu hazitachukuliwa kuinusuru Karaiakoo, kuna kila uwezekano wa kutokea kwa maafa makubwa zaidi siku za usoni. Tayari serikali kupitia kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa imetangaza kuunda tume ya watu 19 itakayochunguza ubora wa majengo yote Kariakoo. Kuundwa kwa tume hii kunatokana na agizo alilolitoa Rais Samia Suluhu Hassan Jumapili iliyopita akiwa safarini Rio de Janeiro ambako anahudhuria mkutano wa G20. Rais Samia alitoa agizo hilo katika hotuba yake ya kuwapa pole wote waliofikwa na maafa ya Kariakoo.
Hatua ya serikali ya kuunda tume ni nzuri, inastahili kupongezwa, lakini wakati huo huo yafaa kujihoji ni kwa jinsi gani ripoti ya timu ya ukaguzi wa majengo iliyoundwa miaka 19 iliyopita kufuatia kuporomoka kwa jengo la Chang’ombe Village Inn ilifanyiwa kazi? Leo takribani miaka 20 baadaye hali ya usalama wa majengo yetu imekuwa nzuri zaidi au imezidi kuwa mbaya?
Ni kweli hiki siyo kipindi cha kulaumiana, tunapaswa kuwapa pole waliofikwa na maafa haya, lakini pamoja na kuwa na utu wa kuomboleza na kusikitika na wote walioathirika na janga hili, ni dhahiri kama hatuwezi kujifunza kwa makosa yetu wenyewe tutazidi kulia kila baada ya kipindi fulani.
Ukisikia simulizi za watu wanaoishi Kariakoo juu ya harakati za ujenzi wa majengo mapya, unajiuliza swali gumu, hivi ni nani anajali kuhusu usalama wa Kariokoo? Kwa kuwa Mungu kwa neema yake ametuepusha na majanga makubwa ya asili, basi sasa itoshe kuona majanga yanayosababishwa na uzembe wa binadamu yanachukua nafasi ya majanga ya asili. Tusema hapana. Sasa tudai uwajibikaji kutoka kwa vyombo vyote vya usimamizi wa usalama wa majengo nchini.