Bangkok, Thailand
Mtu mmoja amefariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa leo wakati ndege ya shirika la ndege la Singapore kutoka London Uingereza kuekea Singapore ilipokumbwa na msukosuko mkubwa, shirika hilo la ndege limethibitisha.
Ndege hiyo aina ya Boeing 777-300ER ilielekezwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Suvarnabhumi huko Bangkok, Thailand, ambako ilitua kwa dharura saa 3:45pm (08:45 GMT) leo Jumanne.
Ndege ya SQ321 “ilikumbana na msukosuko mkubwa njiani,” Shirika la Ndege la Singapore limeeleza katika taarifa kwenye ukurasa wake wa Facebook.
“Tunaweza kuthibitisha kuwa kuna majeruhi na mtu mmoja aliyefariki kwenye ndege ya Boeing 777-300ER,” ilisema.
Saa nne baada ya kutua kwa dharura, watu 18 walisalia hospitalini huku wengine 12 wakitibiwa kwa msingi wa wagonjwa wa nje, imeeleza taarifa hiyo.
“Abiria na wafanyakazi waliosalia wanachunguzwa na kupewa matibabu, inapobidi,” iliongeza.
Ndege hiyo ilikuwa na abiria 211 na wahudumu 18.
Kittipong Kittikachorn, meneja mkuu wa Uwanja wa ndege wa Suvarnabhumi, aliambia mkutano wa wanahabari kwamba mwathiriwa alikuwa Muingereza ambaye alionekana kuwa na mshtuko wa moyo.
Kundi la Viwanja vya Ndege vya Thailand lilisema abiria waliojeruhiwa kidogo na ambao hawajajeruhiwa wanasaidiwa katika eneo maalum lililowekwa ndani ya kituo kwenye Uwanja wa Ndege wa Suvarnabhumi.