Wanasayansi wanasema wamefanikiwa kuondoa Virusi vya Ukimwi kutoka kwenye chembechembe zilizoambukizwa, kwa kutumia teknolojia ya “uhariri wa jeni ya Crispr” iliyoshinda Tuzo ya Nobel.
Wanasema teknolojia hiyo inafanya kazi kama mkasi, lakini katika kiwango cha molekyuli, hukata DNA ili chembechembe “mbaya” ziweze kuondolewa au kuzimwa.
Matumaini ni hatimaye kuweza kuondoa kabisa virusi mwilini, ingawa kazi nyingi zaidi inahitajika ili kuangalia kama itakuwa salama na yenye ufanisi. Dawa zilizopo za VVU kwa sasa zinaweza kuzuia virusi, lakini sio kuviondoa.
Hata hivyo timu ya Chuo Kikuu cha Amsterdam, ikiwasilisha muhtasari wa matokeo yao ya mapema katika mkutano wa kitabibu wiki hii, inasisitiza kwamba kazi yao inabaki kuwa “uthibitisho wa dhana” tu na haitakuwa tiba ya VVU hivi karibuni.
Dk James Dixon ambaye ni Profesa msaidizi wa teknolojia ya seli shina na tiba ya jeni katika Chuo Kikuu cha Nottingham, anakubali, akisema matokeo kamili bado yanahitaji kuchunguzwa.
“Kazi zaidi itahitajika ili kuonesha matokeo katika majaribio haya ya seli yanaweza kutokea katika mwili mzima kwa tiba ya siku zijazo,” anasema Dk Dixon na kuongeza: “Kutakuwa na maendeleo zaidi yanayohitajika kabla ya kuwa na athari kwa wale walio na VVU.”
‘Changamoto kubwa’
Dk Jonathan Stoye, mtaalamu wa stadi za virusi katika Taasisi ya Francis Crick ya London, anasema kuondoa VVU kutoka kwenye seli zote ambazo zinaweza kuvihifadhi mwilini ni “changamoto kubwa”.
“Athari zisizolengwa za matibabu, pamoja na athari zinazowezekana za muda mrefu, zinabaki kuwa wasiwasi,” anasema Dk. Stoye na kuongeza:
“Kwa hivyo inaonekana uwezekano kwamba miaka mingi itapita kabla ya tiba kama hiyo ya Crispr kuwa ya kawaida, hata ikizingatiwa kuwa inaweza kuoneshwa kuwa nzuri.”
Chanzo: BBC Swahili