Polisi wadaiwa kumjeruhi Binti kwa risasi

Mkazi wa Kijiji cha Kewanja Wilaya ya Tarime mkoani Mara, Neema Omari (16), amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere mkoani humo akidaiwa kupigwa risasi miguuni na polisi.

Neema alifikishwa hospitalini hapo Machi 2, 2024 baada ya kupewa rufaa kutoka Hospitali ya Nyamwaga wilayani Tarime alikopelekwa akitokea katika Kituo cha Afya cha Nyamongo ambako pia alipelekwa kwa matibabu baada ya kujeruhiwa.

Akizungumza hospitalini hapo jana Machi 4, 2024, daktari wa kitengo cha mifupa, Elias Nguti alisema baada ya kumfanyia uchunguzi wa awali ilibainika binti huyo ana vipande vya chuma kwenye miguu yote miwili.

“Tulimfanyia upasuaji siku hiyohiyo tukafanikiwa kutoa kipande cha chuma kwenye mguu wa kulia na jana tukafanya tena tukaondoa kwenye mguu wa kushoto, hivi sasa anaedelea vizuri ingawa bado amelazwa hapa hospitalini,” amesema Dk Nguti.

Mama mzazi wa mtoto huyo, Bhoke Chacha amesema tukio hilo lilitokea Februari 29, 2024 saa 12 jioni wakati yeye akiwa njiani akirudi kwenye mgahawa wake alipokuwa amemuacha binti yake, wakati yeye alipokwenda kwenye kikao cha kikundi.

Amesema alimuacha mwanawe huyo mgahawani kwake eneo la Mrwambe katika Kijiji cha Kewanja ili asimamia kazi.

“Nilienda kwenye kikao cha kikundi na kumuacha Neema kwenye mgahawa nikiwa narudi, ghafla tukasikia kelele vijana wakawa wanakimbia, mara likapita gari moja likiwa na askari, wakafyatua risasi ambazo moja kwa moja ziliingia kwenye mgahawa wangu,” amedai mama huyo.

“Na mimi nilivyoona vile, nikaanza kukimbia kuelekea kwenye mgahawa wangu na watu wengine wakawa wanelekea hapo, ghafla yakaja magari mengine manne ya maaskari wakafyatua tena risasi, watu wakaanza kukimbia kila mtu akijaribu kujiokoa, mimi nikafika kwenye mgahawa nikamkuta mtoto amelela chini huku akitokwa na damu nyingi,” anasimulia mama huyo.

Amedai chanzo cha askari hao kufyatua risasi ni kutokana na kudaiwa kulikuwa na vijana waliotaka kuvamia mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara kuokota mawe ya dhahabu.

“Na siku hiyo mvua ilinyesha na kawaida mvua zikinyesha kuna vijana huwa wanaingia mgodini kuokota mawe na pale Mrwambe ni jirani na mgodi,” amesema Chacha.

Neema alivyojeruhiwaAkieleza namna alivyojeruhiwa, Neema anasema akiwa mgahawani anakula chakula, ghafla walisikia mlipuko mkubwa nje ya mgahawa hali iliyomlazimu kukimbia na kufunga mlango.

“Nikiwa ninafunga mlango risasi ilipita kwenye uwazi wa mlango kwa chini na kunipiga kwenye miguu yote miwili hapo hapo nilianguka chini na sikujua kilichoendelea hadi nilipojikuta niko hospitalini,” amesimulia Neema.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Tarime/Rorya, Mark Njera alipotafutwa azungumzie tukio hilo, simu yake haikupokewa na alipotumiwa ujumbe wa maneno, amejibu kwa ufupi, “niko kikaoni nitatoa taarifa kwenu juu ya tukio hili.”Chanzo: Mwananchi

spot_img

Latest articles

Tanesco yazindua ndege nyuki (Drones) kuboresha miundombinu ya umeme nchini

📌Ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati yake kuimarisha huduma kwa wateja kwa kutumia njia...

Senegal yavuliwa ubingwa wa AFCON 2025, wapewa Morocco

Na Mwandishi Wetu SENEGAL imevuliwa ubingwa  wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 baada...

Yanga kuikabili TRA bila Depu, kocha aeleza ugumu ulipo

Na Mwandishi Wetu WAKATI Yanga ikitarajiwa kushuka dimbani kesho Machi 18, 2026  kuikabili TRA United katika Ligi...

Vijana 3,967 waomba uwezeshaji kupitia Go Green na IMBEJU ya CRDB Bank Foundation

Na Mwandishi wetu JUMLA ya vijana 3,967 kutoka maeneo mbalimbali nchini wamewasilisha maombi ya...

More like this

Tanesco yazindua ndege nyuki (Drones) kuboresha miundombinu ya umeme nchini

📌Ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati yake kuimarisha huduma kwa wateja kwa kutumia njia...

Senegal yavuliwa ubingwa wa AFCON 2025, wapewa Morocco

Na Mwandishi Wetu SENEGAL imevuliwa ubingwa  wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 baada...

Yanga kuikabili TRA bila Depu, kocha aeleza ugumu ulipo

Na Mwandishi Wetu WAKATI Yanga ikitarajiwa kushuka dimbani kesho Machi 18, 2026  kuikabili TRA United katika Ligi...