Na Nora Damian
Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (Tughe) kimeiomba Serikali kushughulikia changamoto ya malipo ya nauli za likizo kwa watumishi wasio walimu katika halmashauri za wilaya ili kuleta tija sehemu za kazi.
Akizungumza Februari 21,2024 Katibu Mkuu wa Tughe – Taifa, Hery Mkunda, amesema wanapendekeza watumishi hao walipwe moja kwa moja na hazina kama ilivyo kwa walimu badala ya kutumia mapato ya ndani ya halmashauri.
“Wafanyakazi wasio walimu walioko halmashauri likizo zao hawalipwi toka hazina, wanalipwa kutokana na mapato ya ndani ya halmashauri. Wakati mwingine hawalipwi kwa wakati, tunaomba haki zao zilipwe moja kwa moja kutoka Serikali Kuu badala ya halmashauri.
“Serikali ifanye kila linalowezekana kuhakikisha wafanyakazi wanalipwa haki zao bila kutegemea mapato ya ndani ya halmashauri,” amesema Mkunda.
Chama hicho pia kimeishukuru Serikali kwa kukubali ombi lao la kuwalipa posho ya madaraka waganga wafawidhi katika vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi.
Hivi karibuni Serikali ilitangaza kuanza kulipa posho hizo katika mwaka wa fedha wa 2024/25 kutokana na kazi kubwa wanayofanya watumishi hao ya kusimamia utoaji wa huduma za afya, utawala na usimamizi wa miradi.
Kwa mujibu wa Mkunda, kwa muda mrefu waliwasilisha hoja hiyo na nyingine serikalini kwa sababu majukumu ya watumishi hao ni makubwa.
“Mara kwa mara kwenye majukwaa na vikao tumekuwa tukizungumzia kuwapa motisha waganga wafawidhi katika vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi ili kuboresha utendaji wao na kufikia malengo yaliyowekwa.
“Tunafurahi Serikali imesikia maombi yetu na inaleta motisha kwa wafanyakazi, tunaomba watumishi waendelee kutoa huduma kadiri inavyotakiwa, waongeze ubunifu na kujituma zaidi…wasiviangushe vyama vya wafanyakazi,” amesema Mkunda.
Chama hicho kimeiomba Serikali kuendelea kushughulikia changamoto nyingine kama vile ajira za mikataba kwa baadhi ya watumishi wa umma, nyongeza ya posho ya kuitwa kazini na kutokamilika kwa muundo wa watumishi wa maha