1953 – 2024 Lowassa amegoma kufa

Na Jesse Kwayu

EDWARD Lowassa, waziri mkuu mstaafu wa Jamhuri ya Muungano na mwanasiasa machachari nchini, aliyefariki dunia, Jumamosi iliyopita, “amegoma kufa,” MwanaHALISI laweza kuripoti.

Lowassa anayetarajiwa kuzikwa mwishoni mwa wiki nyumbani kwake Monduli mkoani Arusha, pamoja na majaribio kadhaa yaliyoelekezwa kwake, aligoma kufa kisiasa tangu mwaka 1995.

Kifo cha kisiasa cha Lowassa kilitarajiwa kiwe mwaka 1995, baada ya kutupa karata yake ya kwanza kuutaka urais wa Jamhuri ya Muungano, wakati uliporejeshwa tena mfumo wa vyama vingi nchini na hivyo kufunguliwa kwa siasa za ushindani. 

Akiwa ameshakuwa waziri katika wizara mbalimbali wakati wa utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi, Lowassa alijipatia umaarufu mkubwa kisiasa kutokana na uwezo wake wa kukabiliana na changamoto kwa nafasi alizopewa na uthubutu wake wa kukemea dhuluma.

Katika tukio mojawapo kubwa lililompambanua kama kiongozi anayejali maslahi ya wananchi, akiwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Lowassa alifuta uamuzi uliochukuliwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam mwaka 1994, kutaka kumilikisha mmoja wa wafanyabiashara uwanja wa wazi wa Mnazi Mmoja. 

Kauli ya Lowasa, iliibua hasira ya umma na wananchi waliamua kuulinda uwanja huo kwa kuvunja uzio wa mabati ambao tayari ulikuwa umezungushiwa na mfanyabiashara huyo. 

Kutokana na kipindi cha kati ya mwaka 1990 hadi 1995 kuwa na harakati nyingi za kisiasa nchini na Rais Mwinyi kuelekea kumaliza muhula wake wa pili wa urais na hivyo kuzuiwa na Katiba kuwania tena nafasi hiyo, jina la Lowassa lilizidi kutawala vinywa vya watu kama mmoja wa wanasiasa wanaoweza kuvaa viatu vya urais baada ya Mwinyi.

Waliobebea bango jina la Lowassa, wakati huu ambapo siasa za vyama vingi zilizidi kupambamoto, walikuwa ni Jumuiya ya Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM), chini ya uenyekiti wa John Guninita.

Jina la Lowassa, lilikuwa miongoni mwa majina matano yaliyotajwa hadharani na UV-CCM, kwamba wanaoona wanafaa kuwa warithi wa Rais Mwinyi.

Wengine waliotajwa na UV-CCM kuwa wangepigiwa debe, ni pamoja na Jakaya Kikwete na Dk. Salim Ahmed Salim. Hatua hiyo ya UV-CCM, mbali ya kuibua taharuki kubwa kwenye chama hicho, ilisababisha uongozi wote wa juu wa umoja huo, kusambaratishwa.

Ni katika vuguvugu hizo za kisiasa jina la Lowassa lilizidi kujipambanua kama mmoja wa watu wanaopewa nafasi kubwa zaidi kupata fursa ya kuwania urais kupitia chama hicho tawala. 

Wakiwa wamekwisha kujipanga kuunda ushirikiano na Kikwete, milango ya kuwania urais ilipofunguliwa kupitia CCM, Lowassa alikuwa miongoni mwa wanachama wengine 16 walioamua kujitosa kuwania kiti hicho. 

Wakati huo nyota yake iking’aa, aliambatana na Kikwete kwenda Dodoma, makao makuu ya chama hicho, kwa ajili ya kuchukua fomu ya kuwania urais. Katika safari hiyo, wagombea hao wawili, walitumia ndege ya kukodi na ndipo baadaye wakajipachika jina la “Boys two Men.”

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa wawili hawa, ambao baadaye walikuja kuunda mtandao uliomweka madarakani Kikwete mwaka 2005, walipoulizwa kati yao, yaani Kikwete na Lowassa nani anamsindikiza mwenzake, wote kwa pamoja walisema, “tunasindikizana.” 

Ilikuwa ni katika kikao cha Kamati Kuu (CC), iliyoketi Dodoma kupitisha majina ya wagombea urais kwenda Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ndipo jaribio la kwanza la kumuua kisiasa Lowassa lilifanyika. 

NEC ilipitisha majina sita kwa ajili ya kwenda mkutano mkuu kupigiwa kura. Waliopitishwa walikuwa Kikwete, Cleopa Msuya, Benjamin Mkapa, Pius Msekwa, Joseph Warioba na Mark Bomani, hali iliyozua taharuki kubwa hasa kwa rika la vijana kwamba ‘kulikoni’ chaguo lao, Lowassa halipo. 

Hata Mwalimu Julius Nyerere ambaye aliamua kurejea kwenye ulingo wa kuratibu (kudhibiti) mchakato wa kupata mgombea urais kupitia CCM, alipofanya mkutano na waandishi wa habari na kujibu baadhi ya maswali kadhaa, miongoni mwao likiwa ni kwa nini jina la Lowassa lilikatwa, hakuweza kuwa na jibu la moja kwa moja. 

Badala yake, Mwalimu pamoja na kujaribu kutokutaja sababu mahusi iliyoipa CC nguvu ya kuondosha jina la mwanasiasa huyo, kuwa miongoni mwa wagombea wake wa urais, alisema tu hoja ilitolewa na ikakubalika. 

Aidha, Mwalimu Nyerere alisema, “hata vijana wa CCM waliotaka ‘kushinikiza’ jina la Lowassa lirudi ndani ya NEC kwa ushabiki mkubwa, walielezwa juu ya hoja za Kamati Kuu na kuelewa.” 

Katika uwanja wa siasa kile kilichomtokea mwaka 1995, ilikuwa ni sawa na shambulio la mapema dhidi ya mpinzani wako wakati akijiandaa kwa pambano, ili asipate fursa ya kufika uwanja wa mapambano. 

Ni dhahiri kwa kasi, umaarufu na kujipanga kwa Lowassa mwaka 1995 kama siyo ‘mizengwe’ ndani ya Kamati Kuu, ni hakika ndiye angelikuwa Rais wa awamu ya tatu. 

Hili lilikuwa jaribio la kwanza la kumuua Lowassa kisiasa, lakini aligoma kufa.

Hata Mkapa, ambaye ushindi wake kuwa mgombea urais mwaka 1995 ulihitaji pia nguvu ya Mwalimu Nyerere kuomba kura kwa wananchi ili ashinde, naye aliingia baridi kuhusu nafasi ya Lowassa kisiasa.

Katika baraza lake la kwanza la mawaziri baada ya kutangazwa mshindi, Lowassa hakuwa miongoni mwa aliyoingia nao serikalini. Alimrejesha katika baraza la mawaziri kupitia mabadiliko madogo aliyofanya mwaka 1997.

Safari ya Lowassa katika baraza la mawaziri la Mkapa katika muhula wake wa pili, akiwa waziri wa maji, ilizidi kumpeperusha katika siasa za ndani na kumuweka katika nafasi ya juu ya kuwania urais baada ya kiongozi aliyeko madarakani kumaliza utumishi wake.

 Uamuzi wa Lowassa kuhusu haki ya wananchi ya kupata maji, ikiwa ni pamoja na kuvunja mkataba wa kampuni ya City Water na Dawasa na kupambania haki ya Tanzania kutumia maji ya Ziwa Victotria, ndivyo viliwezesha kuimarisha ushirikiano wake tena na Kikwete uliojenga mtandao uliomuingiza Kikwete Ikulu, mwaka 2005.

Hata hivyo, mwaka 2008 likatokea jabio la pili la kumuua Lowassa kisiasa, wakati akiwa waziri mkuu. 

Jaribio hili lilikuja kwenye sura ya kilichoitwa, “mkataba tata wa Richmond,” ulioshirikisha kampuni hiyo ya kigeni na shirika la umeme la taifa (Tanesco), ambako ilijengwa hoja ya ‘zimwi’ la rushwa. 

Kwamba Lowassa ndiye alikuwa nyuma ya Richmond, kampuni iliyodaiwa kuwa ya mfukoni na ambayo ilipewa kazi ya kuzalisha megawati 150 za umeme wa dharura na kisha umeme huo, kuingizwa kwenye gridi ya taifa.

Kamati teule ya Bunge iliyoundwa na Spika Samwel Sitta, ambaye habari zinasema, ndiye alikuwa mwenyekiti wa mtandao wa kumuingiza Ikulu Kikwete, ndiye aliyechochea mtafaruku, akitumia ugomvi wake binafsi na Lowassa na “madai kuwa mwanasiasa huyo amepanga kuwania urais mwaka 2010.

Tangu siku ya kwanza, Sitta hakufurahia nafasi ya Lowassa ya waziri mkuu, kwani katika makubaliano yao, Kikwete alikuwa amemuahidi Sitta na Lowassa, kushika nafasi moja ya waziri mkuu, jambo ambalo rais huyo mstaafu, hawezi kujiepusha na chimbuko la chuki hizo.

Pamoja na kutokea ugmvi huo kati ya Spika wa Bunge na Waziri Mkuu, mgogoro ulizaa makundi ya washindani ndani ya CCM, Lowassa akabaki na Kikwete wake, Sitta akashikamana na Dk. Harrison Mwakyembe, aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge, iliyochunguza mkataba wa Richmond.

Vilevile, baada ya siasa za kuzungukana ndani kwa ndani, wanamtandao wakajeruhiana na kisha Kikwete akiwa ameanza kupoteza nguvu na uwezo wa kudhibiti uhasama ndani ya kundi hilo, hasa kufuatia baadhi ya wanamtandao kutofarahishwa na walichovuna baada ya safari ya miaka 10 ya jasho na damu ya kumweka madarakani kiongozi wao, hitimisho la jaribio la kumuua Lowassa kisiasa, lilifanyika ambako aliamua kujiuzulu uwaziri mkuu, Februari 2008.

Safari ya Lowassa nje ya serikali ikaamsha mlolongo wa majaribio kadhaa ya kuhakikisha haibuki tena. 

Harakati hizi ziliongozwa na watu wengi, miongoni mwao, ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Spika Sitta, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye; Dk. Mwakyembe na Paul Makonda, aliyekuwa UV-CCM, ambao waliunda ushirika wa ‘uovu’ wa kumtukana na kumdhalilisha mwanasiasa huyo, kila mahali. 

Kwenye vyombo vya habari, mikutano ya hadhara na ndani ya vikao vya CCM, walifikia hatua ya kuanza kampeni ya vua gamba, ambayo ilibarikiwa na Kikwete mwenyewe.

Juhudi zote hizo, hata hivyo, hazikufanikiwa kufunika nyota ya Lowassa. Hazikuondoa uungwaji mkono wake ndani ya CCM, badala yake, vikundi vingi vya kumuunga mkono mwanasiasa huyo kupitia chama hicho vilizaliwa. 

Wafuasi wa Lowassa, waliweza kudhibiti Jumuiya ya Wanawake (UWT), UVCCM na hata NEC yenyewe. 

Makao makuu ya chama hicho, yakageuka kuwa sehemu ya kupanga mikakati ya kumzuia Lowassa kusonga mbele kisiasa. 

Akapewa karipio kwamba ameanza kampeni za kuwania urais kabla ya wakati, huku ziara za Kinana na Nape mikoani, zikiwa mkakati wa kufikisha mwisho ndoto zake za kuingia Ikulu, walau kupitia chama hicho.

Hitimisho la kumua kisiasa likaja mwaka 2015 wakati wa mchakato wa kupitisha majina ya wawania urais.

Kikao cha NEC, ambako Kikwete aliingia akiwa na majina yake matano mfukoni – Bernard Membe, John Magufuli, Dk. Asha Rose Migiro, January Makamba na Amina Salim Ali. Lowassa na wawania urais wengine 32, majina yao yaliondolewa. 

Hata hapa, Lowassa aligoma tena kufa kisiasa. 

“Hii siku Kikwete hataisahau. Alipoingia kwenye NEC, alipokewa na wimbo wenye maneno, ‘tuna imani na Lowassa,’ huku akiwa tayari amelishaliondoa jina lake usiku wa jana,” ameeleza kiongozi mmoja mwandamizi wa chama hicho, ambaye hakupenda kutajwa jina.

Baada ya kufanyiwa zengwe hilo, Lowassa aliondoka CCM na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo, na kisha kupitishwa kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2015, chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA). Lowassa aliondoka CCM na kujiunga na Chadema, 29 Julai 2015.  

UKAWA iliundwa na vyama vinne vya Chadema, CUF, NCCR-Maugeuzi na NLD. 

Uchaguzi wa mwaka 2015 uligeuza kabisa sura ya Tanzania kutoka nchi inayofungamanishwa na siasa za chama kimoja chenye nguvu zaidi na vingine vikionekana kama wasindikizaji. 

Nguvu ya Lowassa aliyopeleka UKAWA, ilisababisha kwa mara ya kwanza upinzani kutwaa halmashauri zote za miji mikubwa kama Dar es Salaam, Arusha, Mbeya, Moshi, Bukoba na majimbo ya uchaguzi lukuki. 

Upinzani uliingiza bungeni wabunge 112, wa jimbo wakiwa ni wabunge takribani 75, huku wa viti maalum wakiwa 37. 

Katika uchaguzi huo, nguvu za Lowassa alizoongezea UKAWA kwa mara ya kwanza katika historia ya upinzani nchini (tangu uhaguzi wa 1995, 2000, 2005, 2010), CCM ilipata chini ya asilimia 60. 

Pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kutokuwa huru, kuvurugwa na kukamatwa kwa mawakala wa UKAWA na vituo vyao vya kuhesabu kura kuvamia na kuhujumiwa, Lowassa alipata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97 huku Magufuli akipata kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46.

Hatimaye Lowassa alirejea CCM, tarehe mosi Machi 2019, katika kipindi ambacho upinzani ‘ulikuwa unabatizwa kwa moto’ chini utawala wa Rais Magufuli. 

Alirejea kipindi ambacho upinzani ulionekana kama uhaini, huku wabunge na madiwani wake, wakitangaza kujiunga na CCM, katika falsafa ya “kuunga mkono juhudi.”

Lowassa amelala kifo cha kuondokewa na uhai, lakini hata sasa akiwa katika umauti, bado amendelea kuishi kisiasa. Umati wa watu wanaofurika nyumbani kwake Masaki, Dar es Salaam, Karimjee na kanisani KKKT Azania Front, ni kielelezo kingine kwamba amegoma kufa. 

Akizungumza wakati wa kuaga mwili wake, juzi Jumanne, waziri mkuu mstaafu, Joseph Warioba, alimtaja Lowassa, kama mtu aliyekuwa na sifa zote za uongozi.

Alisema, “Lowassa alikuwa ni mtu mwenye imani na maono ya kulitumikia taifa lake. Alikuwa na maono yake na vipaumbele vyake alivionyesha kwenye utumishi wake.  Alipata kejeli na matusi, lakini hakurudisha hata siku moja. Alikuwa ni kiongozi mvumilivu mwenye sifa za uongozi na mwenye kuweza kulitumikia taifa hili.”

Hata hivyo, rais Kikwete, alipopewa nafasi ya kuzungumza, hakutaka kujadili kabisa safari yao ya kisiasa ya miaka mingi na kile ambacho mwenzake alikipitia.

Huyu ndiye Edward Ngoyai Lowassa tunayekwenda kumlaza kwenye makazi yake ya muda wilayani Monduli, alikotumikia wananchi wake kama mbunge wao tangu mwaka 1995. Alistaafu ubunge mwaka 2015.

spot_img

Latest articles

Soma Ripoti ya UHIFADHI WA UHAI: UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU NDANI YA SEKTA YA UHIFADHI TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Utafiti mpya umebaini kwamba mamlaka za serikali zimekuwa kichocheo kikuu...

RAIS DKT. SAMIA ATOA MAAGIZO KWA BASHE, NFRA KUNUNUA MAHINDI KWA WAKULIMA TSH 700 KWA KILO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassanamemuagiza Waziri wa Kilimo...

Upi upepo unaoweza kufika Tanzania,wa Wiliam Ruto au Paul Kagame?

KUNA upepo wa aina mbili unavuma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mmoja...

Watu wawili wafariki, 16 wajeruhiwa katika ajali ya basi Songwe

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Watu wawili wamefariki dunia na wengine 16 kujeruhiwa baada ya...

More like this

Soma Ripoti ya UHIFADHI WA UHAI: UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU NDANI YA SEKTA YA UHIFADHI TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Utafiti mpya umebaini kwamba mamlaka za serikali zimekuwa kichocheo kikuu...

RAIS DKT. SAMIA ATOA MAAGIZO KWA BASHE, NFRA KUNUNUA MAHINDI KWA WAKULIMA TSH 700 KWA KILO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassanamemuagiza Waziri wa Kilimo...

Upi upepo unaoweza kufika Tanzania,wa Wiliam Ruto au Paul Kagame?

KUNA upepo wa aina mbili unavuma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mmoja...