Acheni maigizo yasiyo na tija, ondoeni mgawo wa umeme

MWAKA jana mgawo wa umeme ulipoanza kidogo kidogo kulikuwa na hisia ndani ya jamii kwamba hali hiyo ilitokana na hujuma. Wapo waliooanisha hali hiyo ama na uwezo wa menejimenti ya Shirika la Umeme nchini (Tanesco) au na Wizara ya Nishati. Hisia hizi zilitiwa nguvu sana hasa baada ya kutokea kwa mabadiliko ya mtendaji mkuu wa Tanesco na kwa Waziri wa Nishati.

Waziri wa Nishati Januari Makamba alihamishiwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki mwishoni mwa Agosti mwaka jana. Naye Maharage Chande aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco alihamishwa kutoka shirika hilo nyeti kwa uchumi wa nchi Septemba mwaka jana. Chande sasa ni Mkugenzi wa Shirika la Posta.

Hisia za hujuma zilipamba moto na kuonekana kwamba suala la mgawo wa umeme huenda ulikuwa ni mpango mahususi wa watu kujinufaisha. Hali hii ilichangiwa zaidi na clip fupi iliyokuwa inazungushwa kwenye mitandao ya kijamii ikikumbushia kauli aliyopata kutoa Rais wa Tanzania enzi za uhai wake, marehemu Dk. John Magufuli.

Hayati John Magufuli.

Magufuli alipata kusema kuwa mgawo wa umeme uliokuwa wanatikisa nchi kila wakati ulikuwa ni mpango wa watu kuuza majenereta. Alisema chini ya utawala wake hakutakuwa na mgawo wa umeme. Ukweli wa kauli ya Marehemu Magufuli ni fumbo zito mpaka leo. Lakini ni kauli ya kufikirisha.

Hata hivyo, leo tunapotazama nyumba sasa ni takribani miezi mitano, Septemba, Oktoba, Novemba, Disemba na Januari imekatika, nchi ingalipo kwenye mgawo wa umeme. Hii ni miezi mitano. Ni karibia nusu mwaka. Kwa matiki hii, tatizo la kukosekana kwa umeme ni kubwa kuliko wakubwa wanavyouambia umma. Tanesco imekuwa ikitoa sababu kuu mbili zinazosababisha taifa kuingia katika mgawo wa umeme.

Nazo ni ukame ambao ni matokeo ya kutokunyesha kwa mvua kwa muda mrefu au kwa wakati mwafaka; na uchakavu wa mitambo ambao unahitaji matengenezo- hali hii husababisha upungufu wa umeme katika gridi ya taifa kwa sababu baadhi ya mitambo haizalishi umeme.

Katika uchambuzi mwingine nilioandika katika safu hii ukibeba kichwa kisemacho ‘Tanesco hoi, shida ni Tanesco au serikali?’ nilikumbusha kwamba shirika hili kongwe la kuzalisha nishati ya umeme, Novemba mwaka 2022 lilikuwa limetoa taarifa kwa umma juu ya uwezekano wa mgawo wa umama. Na sababu zao zilikuwa ni hizo hizo.

Yaani Novemba 23, 2022 walisema kuwa mgawo huo ni kutokana na kupungua kwa uzalishaji wa umeme hasa katika mabwawa ya kufua umeme kwa kutumia maji. Walifafanua kwa kina kiasi cha upungufu kwa kila bwawa. Uchambuzi uko hapa, rejea inaweza kufanyika. Leo ni Januari 31, 2024, miaka miwili tangu zile sababu zitolewe. Uhaba wa maji na matengenezo ya mitambo.

Leo mtu anaweza kujiuliza hivi, ni muda kiasi gani Tanesco wanahitaji ili kufanikisha kurejesha uzalishaji wa nishati ya umeme katika hali ya kawaida? Yaani kusiwapo na mgawo hata kidogo? 

Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Gissima Nyamo Hanga akiwa na walau miezi miwili ofisini tangu alipoteuliwa kwenye nafasi hiyo Septemba mwaka jana, Novemba 24 mwaka jana, alikutana na waandishi wa habari jijini Dodoma na kueleza hali ya upatikanaji wa umeme nchini. Alisema wazi kuwa upatikanaji umeme kwa kipindi cha Septemba hadi Novemba mwaka jana uliimarika baada ya kuongeza zaidi ya megawati 197 kwenye Gridi ya Taifa na kufanya upungufu wa umeme kushuka kutoka megawati 410 hadi megawati 213 hivyo kupunguza makali ya mgao wa umeme nchini.

Alitaja sababu za kuimarika kwa uzalishaji wa umeme kuwa ni matengenezo ya mitambo, kuongezeka kwa upatikanaji wa gesi asilia kutoka TPDC, sambamba na upatikanaji wa mvua katika ukanda wa vituo vya kuzalisha umeme vya Nyumba ya Mungu, Hale na Pangani.

Katika mkutano huo, Nyamu Hanga alisema kuwa mvua zilizokuwa zinanyesha nchini, ambazo kwa hakika zimekuwa kubwa na zilizoleta maafa makubwa, hazijawa na faida kwa mabwawa ya Mtera, Kidatu na Kihansi kwa sababu mvua hizo hazikunyesha katika mikoa ya Iringa, Mbeya, Tabora, Singida na Dodoma. Kwa maneno mengine, alisema kuwa mvua zilizokuwa zinanyesha na ambazo kwa hakika zimeendelea kunyesha hadi sasa katika mikoa ya Pwani, Tanga, Mara, Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Geita na Kagera hazijawa na faida kwa mabwawa ya Mtera, Kihansi na Kidatu!

Bila kuingia katika mjadala wowote wa kupima kama kauli ya kiongozi huyo mkuu wa Tanesco ina mashiko au la, tukumbuke kwamba katika taarifa mbalimbali za Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) nchi nzima inapata mvua. Mvua kubwa. Tumeona mafuriko maeneo na maeneo. Tumeshuhudia mafuriko Morogoro ambako ndiko kuliko vyanzo vya mito mingi inayolisha mikoa mingine mingi. Tumeona maji kila kona ya nchi hii, lakini bado mabwawa hayana maji?

Hapa kwenye mkutano wa Mkurugenzi Nyamu Hanga na waandishi alisema kuwa wamepata gesi asilia nyingi kutoka TPDC ambayo imesaidia kuongeza kiwango cha uzalishaji umeme. Swali linaendelea kubaki, ni lini kumekuwa na uhaba wa gesi asilia? Je, tatizo ni nini? Imeisha Lindi na Mtwara? Au shinda iko kwenye nini hasa? Kuna kitu hakisemwi au hakiwekwi wazi.

Leo ni siku ya mwisho ya Januari 2024, hakuna dalili kwamba mgawo wa umeme unaisha lini. Leo ni takribani miezi mitano tangu mgawo huu uanze, lakini kwa bahati mbaya sana hakuna yeyote ndani ya serikali anayejali kusema au walau kuja na takwimu kuonyesha madhara ya kiuchumi ambayo nchi inakwenda kupata.

Kilichopo ni sinema na maigizo yasiyoisha. Watu kutumia gharama kubwa kufanya ziara ndani ya nchi huku wakijitutumua kwamba wanakagua utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Wakati wakikagua utekelezaji huo, nchi haina umeme. Shughuli nyingi za uzalishaji mali zimesimama. Gharama za uzalishaji zimekwenda juu kwa sababu ya kuendesha viwanda kwa kutumia majenereta yanayobugia mafuta ya dizeli. Hali ni ngumu, lakini Watanzania tunachezewa sinema na watu wanaotafuta ‘kiki’. Aibu!

Ni katika tafakari hii mtu anajiuliza hivi Tanesco wanasema ukweli juu ya hali halisi ya kurejea kwa huduma ya umeme nchini? Ni lini? Je, Tanesco wanasema ukweli juu ya hali ya miundombinu yake ya kusafirisha umeme? Je, Tanesco wanauambia umma ukweli kwamba nini kilitokea mpaka wakafika hapo walipo na sasa mgawo ndani ya miezi mitano bado upo?  Wataumaliza lini? Kama miezi mitano haijatosha, ni muda gani wanahitaji. Je, kusema ukweli si kungesaidia umma kujipanga kisaikolojia? Nilipata kusema pale Tanesco mtabadilisha wakurugenzi mpaka mtaazima kutoka nje, lakini shida ya mgawo wa umeme haitaisha kwa sababu, ukweli hausemwi.

Ninafikiri kwa kiasi kile kile serikali ya CCM inavyofurahi kupongezwa na kujitangaza kwamba imefanya mambo makubwa nchini, amani na utulivo na kujenga uchumi; sasa pia ikubali kwamba mkwamo wa Tanesco katika kuzalisha umeme wa kutosha katika nchi hii pia ni mzigo wake. Na isione aibu kusema katika hili, tumewaangusha Watanzania ambao kwa mwezi wa tano sasa mfululizo wanaendelea kutaabika na mgawo wa umeme.

spot_img

Latest articles

Safari ya ‘TLP’ ya Lissu ni ipi?

MWAKA 1992 wakati nchi hii ilipoingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, kulikuwa...

Karibu 2025, tuyakatae magenge haya sasa

LEO ni siku ya pili katika mwaka mpya wa 2025. Ninawatakia wasomaji wa safu...

Kuubeba uozo wa 2024  kuingia 2025 ni fedheha

NI siku nne tu zimebakia kuupa kisogo mwaka 2024. Mwaka huu ulikuwa na mambo...

Hivi vikosi kazi vimerejea kwa mlango wa nyuma?

KUNA kila dalili kwamba taifa letu kidogokidogo linakumbwa na hali ya kutokuaminiana. Hali hii...

More like this

Safari ya ‘TLP’ ya Lissu ni ipi?

MWAKA 1992 wakati nchi hii ilipoingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, kulikuwa...

Karibu 2025, tuyakatae magenge haya sasa

LEO ni siku ya pili katika mwaka mpya wa 2025. Ninawatakia wasomaji wa safu...

Kuubeba uozo wa 2024  kuingia 2025 ni fedheha

NI siku nne tu zimebakia kuupa kisogo mwaka 2024. Mwaka huu ulikuwa na mambo...