Kiev, Ukraine
Ukraine imesema leo Jumanne Oktoba 3, kuwa imezidunguwa takribani ndege 29 zisizo na rubani zilizotengenezwa na Iran pamoja na kombora la masafa marefu lililorushwa na vikosi vya Urusi kutoka Rasi ya Crimea.
Jeshi la anga la Ukraine limesema kuwa usiku wa kuamkia leo, washambuliaji wa Urusi katika eneo hilo la Crimea, waliishambulia nchi hiyo kwa kutumia ndege hizo zisizo na rubani na kombora aina ya Iskander-K.
Taarifa ya jeshi hilo imeeleza kuwa udunguaji huo ulifanywa na vikosi vinavyohusika na eneo la kusini la Mykolaiv na eneo la kati la Dnipropetrovsk.
Ukraine yaonya
Ukraine imeonya kuwa Urusi inaanzisha upya kampeni ya mashambulizi ya anga dhidi ya miundombinu ya nishati ya Ukraine ambayo kwenye majira ya baridi kali ya mwaka jana yaliwaacha mamilioni ya watu bila gesi ya kupashia joto nyumba zao na maji kwa muda mrefu.
Wiki hii, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine aliuhimiza Umoja wa Ulaya kuongeza vikwazo vyake dhidi ya Urusi na pia Iran kwa kupeleka ndege zake zisizo na rubani nchini Urusi.
Shirika la habari la serikali ya Urusi, RIA, limemnukuu Waziri wa Ulinzi wa Urusi, Sergei Shoigu, akisema kuwa jeshi la nchi hiyo halina mipango ya kuwahamasisha wanaume zaidi kujiunga katika vita vya Ukraine kwa sababu lina maafisa wa kutosha.
Katika hatua nyingine, wakati wa taarifa zake za kila siku kuhusu vita vya Ukraine, Wizara ya Ulinzi ya Uingereza imesema kuwa kura ya maoni iliyofanywa hivi karibuni na kituo cha serikali cha utafiti wa maoni ya umma iligundua kuwa asilimia 61 ya wale waliohojiwa wanachukulia neno “mawakala wa kigeni” kuwa wasaliti wanaoeneza uwongo kuhusu Urusi.