Na Mwandishi Wetu
KAIMU Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipangomiji (TPRB), TP. Martha Mkupasi, ameshiriki mafunzo elekezi kwa watendaji wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali yanayolenga kuimarisha uongozi wenye matokeo na kuongeza uwajibikaji katika utendaji wa taasisi za umma unaoendana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

TP. Mkupasi amehudhuria mafunzo hayo yaliyoongozwa na kaulimbiu isemayo “Kutoka Maono Mpaka Matokeo: Kufungamanisha Utekelezaji wa Mashirika ya Umma na DIRA 2050”, yaliyoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi, yaliyofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.
Akizungumza baada ya kushiriki mafunzo hayo ya siku nne, TP. Martha Mkupasi amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwani yamewajengea viongozi hao uwezo wa kuunganisha maono ya kitaifa katika majukumu ya kila siku ndani ya taasisi na yatawasaidia kuandaa mipango inayoakisi utekelezaji malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema wamepata fursa ya kujifunza namna bora ya kusimamia taasisi kwa kuzingatia matokeo, kuandaa mipango, uwajibikaji na ubunifu ikiwa ni njia ya kuwasaidia kuchangia kikamilifu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa manufaa ya umma.



