Na Mwandishi Wetu
WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) umeibuka mshindi wa pili na kutunukiwa tuzo ya Banda Bora katika kipengele cha Sekta ya Milki na Real Estate wakati wa sherehe za kufunga Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Tuzo hiyo ilipokelewa kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro, na Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa TBA, Amina Lumuli, ambaye alisema ushindi huo umetokana na ubunifu uliotumika katika maandalizi ya banda la taasisi hiyo pamoja na namna lilivyofanikiwa kuwasilisha fursa mbalimbali za uwekezaji kwa wananchi na wadau wa maendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupokea tuzo hiyo, Lumuli alisema ushiriki wa TBA katika maonesho hayo umefanikisha lengo la kuwafikia Watanzania kwa kuwaelimisha kuhusu majukumu ya taasisi hiyo, ikiwemo utoaji wa huduma za ushauri wa ujenzi, usimamizi wa miradi na milki za Serikali, pamoja na fursa zilizopo katika sekta ya real estate.

Alisema TBA imeweka mkazo katika kuonesha fursa za uwekezaji kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), huku ikieleza miradi ya kimkakati inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.
“Miongoni mwa miradi iliyovutia wageni wengi ni ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, majengo ya Serikali na ukarabati pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya michezo, ikiwemo Uwanja wa Benjamin Mkapa. Hii imeonesha uwezo wa kitaalamu wa TBA katika sekta ya ujenzi na usimamizi wa majengo,” alisema.

Alibainisha kuwa, wananchi waliotembelea banda la TBA walipata fursa ya kujionea kazi zinazotekelezwa na taasisi hiyo pamoja na kutambua nafasi zilizopo za kushiriki katika uwekezaji wa milki za Serikali.
Alifafanua kuwa, kwa sasa TBA imeainisha milki 149 zenye fursa za uwekezaji, huku 38 tayari zikiwa zimetangazwa rasmi kwa wawekezaji.
“Kwa sasa tunazo milki 149 tulizoziainisha na tayari tumetangaza milki 38 kwa ajili ya uwekezaji. Tunawaalika Watanzania na wawekezaji wenye nia ya kuwekeza kwenye sekta ya real estate kushirikiana na TBA ili kunufaika na fursa hizi,” alisema.

Aidha, alisema tuzo hiyo ni ishara ya kuendelea kuaminiwa kwa TBA kutokana na ubora wa huduma, ubunifu wa kihandisi na uwezo wa kutekeleza miradi yenye tija kwa maendeleo ya Taifa.
“Tuzo hii kwetu ni mwanzo wa safari ya mafanikio makubwa. Hatuna jambo dogo TBA, kila kitu tunakichukulia kwa umakini mkubwa. Mafanikio haya yametupa chachu ya kujipanga kwenda viwango vya juu zaidi vya kimataifa,” alisema.
Aliongeza kuwa TBA tayari imeanza kutekeleza Mkakati mpya wa miaka mitano wa 2026/27 hadi 2030/31, unaolenga kuifanya taasisi hiyo kuwa kinara barani Afrika katika utoaji wa huduma za makazi, ushauri wa ujenzi na usimamizi wa miradi.
“Dira yetu ni kwenda Afrika. Tunataka kuwa taasisi inayotoa huduma bora zaidi za makazi, ushauri na ujenzi, si Tanzania pekee bali Afrika nzima,” alisema.

Sherehe za utoaji wa tuzo na kufunga Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam ziliongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.


