Na Mwandishi wa OTR
Dar es Salaam. Gawio na michango mingine ambayo Serikali imepokea kutoka taasisi za umma pamoja na kampuni ambazo ina hisa chache kwa mwaka wa fedha 2025/26 imeongezeka kwa asilimia 30 ikilinganishwa na mwaka uliopita, hatua inayoakisi kuimarika kwa usimamizi wa uwekezaji wa umma na ufanisi wa taasisi hizo.
Kwa mwaka huu wa fedha, Ofisi ya Msajili wa Hazina imekusanya Sh1.327 trilioni ambazo zilikabidhiwa kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Jumanne, Juni 30, 2026, Ikulu, Dar es Salaam.
Akipokea gawio hilo, Mhe. Rais alionesha kuridhishwa na ongezeko la asilimia 30 la gawio na michango mingine kwa serikali, akibainisha kuwa linaonesha juhudi za kuimarisha uwajibikaji, ufanisi na nidhamu katika taasisi na mashirika ya umma zinaendelea kuzaa matunda.

Aliwapongeza wenyeviti wa bodi, watendaji wakuu wa taasisi za umma pamoja na kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache kwa kuendelea kuongeza ufanisi, kuboresha ukusanyaji wa mapato na kuongeza thamani ya uwekezaji wa Serikali.
Hata hivyo, alionya kuwa mafanikio hayo yasiwafanye viongozi wa taasisi za umma kuridhika, akisisitiza kuwa kila taasisi inapaswa kupimwa kwa matokeo halisi kupitia thamani inayozalisha, mapato inayochangia serikalini, ubora wa huduma inazotoa na uwezo wake wa kupunguza utegemezi wa Serikali.
“Hatupaswi kubweteka. Badala yake, mafanikio haya yawe chachu ya kufanya vizuri zaidi,” alisema Mhe. Rais, akisisitiza kuwa mwaka ujao anatarajia kuona kiwango cha gawio na michango kikiongezeka zaidi.
Alisema ili kufanikisha azma hiyo, Ofisi ya Msajili wa Hazina, inayosimamia taasisi za umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa chache 308 zenye thamani ya uwekezaji wa Sh92.3 trilioni, inapaswa kuendelea kuimarisha usimamizi wa taasisi hizo ili kuongeza idadi ya zinazotoa gawio na michango kwa Serikali.
“Kadri taasisi za umma zinavyoimarika na kuongeza mchango wake katika Mfuko Mkuu wa Serikali, ndivyo tunavyoongeza uwezo wa Serikali kugharamia miradi ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi, ikiwemo afya,” alisema.

Aidha, Rais Samia alisema wakati Taifa linapoanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 Julai 1 mwaka huu, taasisi na mashirika ya umma zitakuwa nguzo muhimu katika kujenga uchumi mkubwa, shindani, jumuishi na endelevu.
“Utekelezaji wa Dira 2050 unahitaji taasisi zenye uwezo wa kushindana. Taasisi zinazofanya vibaya zitafutiwe dawa ili twende pamoja,” alisisitiza Mhe. Rais.
Alisema Serikali itaendelea kuzitathmini taasisi zake kwa mchango wake katika uchumi wa Taifa, mapato inayoingiza, ubora wa huduma, uwezo wa kujitegemea na thamani inayozalisha kwa Watanzania.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, alisema ongezeko la makusanyo ya gawio na michango mingine linaakisi mafanikio ya sera za mageuzi ya kiuchumi zinazoongozwa na Mhe. Rais.
“Tunaona matokeo ya sera zake za mageuzi kupitia falsafa ya 4Rs, si tu katika taasisi za umma, bali pia katika sekta binafsi,” alisema Prof. Mkumbo.
Awali, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, alisema kiasi cha Sh1.327 trilioni kilichowasilishwa kama gawio na michango mingine ni ongezeko la yapata Sh300 bilioni ikilinganishwa na Sh1.028 trilioni zilizokabidhiwa kwa Mhe. Rais katika mwaka wa fedha 2024/25.
Alisema ongezeko hilo linaonesha kuwa uwekezaji wa serikali unaendelea kutoa matokeo yanayopimika kwa kuongeza mchango wake katika Mfuko Mkuu wa Serikali, hivyo kuimarisha uwezo wa Serikali kugharamia vipaumbele vya maendeleo ya Taifa na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kiasi cha Sh1.327 trilioni kilichokusanywa hadi Juni 29, 2026 kimetokana na vyanzo mbalimbali vya mapato vinavyotokana na uwekezaji wa serikali katika taasisi za umma pamoja na kampuni ambazo serikali ina hisa chache.
Kati ya kiasi hicho, Sh800.5 bilioni, sawa na asilimia 60 ya makusanyo yote, ni gawio kutoka mashirika na kampuni za kibiashara; Sh406 bilioni, sawa na asilimia 30, ni michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi kutoka taasisi za umma zisizo za kibiashara; na Sh121.5 bilioni, sawa na asilimia 10, ni mapato mengine yanayotokana na uwekezaji wa serikali, ikiwemo faida za uwekezaji na michango mingine.
Bw. Mchechu alisema mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa mageuzi ya kiutendaji, kiusimamizi na kiutawala yaliyolenga kuongeza tija, uwajibikaji na ufanisi katika taasisi za umma.
“Matokeo hayo yanaonesha kuwa juhudi za kuimarisha usimamizi wa mali za umma na kuhakikisha uwekezaji wa Serikali unazalisha thamani kubwa zaidi kwa Taifa zinaendelea kuzaa matokeo Chanya,” alisema Bw. Mchechu.
Akizungumzia mageuzi yanayoendelea katika taasisi za umma, Bw. Mchechu alisema taasisi hizo zinaendelea kutekeleza falsafa ya R4 kwa kuweka msisitizo katika Mageuzi na Kujenga Upya, hatua ambazo zimeziwezesha kuboresha mifumo ya uongozi na biashara, kuimarisha uwajibikaji, kuongeza ufanisi na kujenga taasisi zenye tija na matokeo bora.
Alisema mafanikio yanayoonekana katika ongezeko la gawio na michango kwa Serikali, kuimarika kwa utendaji wa taasisi, ongezeko la thamani ya uwekezaji wa umma, kuimarika kwa utawala bora na kupungua kwa utegemezi wa ruzuku katika baadhi ya mashirika ni ushahidi wa utekelezaji wa falsafa hiyo.
Aidha, alisema thamani ya uwekezaji wa Serikali unaosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina imeongezeka kutoka Sh67.01 trilioni mwaka wa fedha 2020/21 hadi Sh92.3 trilioni mwaka wa fedha 2024/25, sawa na ongezeko la asilimia 37, hatua inayoonesha kuimarika kwa thamani ya mali za Serikali na matokeo ya mageuzi yanayoendelea katika usimamizi wa uwekezaji wa umma.


