MCHEZAJI wa soka nchini Ghana, Dominic Frimpong, ameuawa kwa kupigwa risasi baada ya jana Jumapili usiku na majambazi wenye silaha kushambulia basi la timu yake ya Berekum Chelsea.
Tukio hilo lilitokea katika barabara ya Goaso–Bibiani wakati timu ikirejea nyumbani baada mchezo wa ya Ligi Kuu ya Ghana dhidi ya Samartex katika mji wa Samreboi kusini mwa Ghana.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika klabu hiyo, majambazi hao walifunga barabara na kuanza kulishambulia basi lilikuwa limebeba viongozi na wachezajiwakati dereva akijaribu kurudi nyuma.
Jeshi la Polisi nchini humo limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema Frimpong alifariki wakati akipatiwa matibabu hospitalini kutokana na majeraha ya risasi.
Chama cha Soka nchini Ghana(GFA) katika taarifa yake iliyotoa leo Jumatatu Aprili 13,2026, kimesema kimepokea taarifa hiyo kwa mshtuko mkubwa, huku kikimueleza mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 kuwa mwenye kipaji na mapenzi ya mchezo huo.
Timu hiyo imekumbwa na mkasa huo wakati ilipokuwa ikirejea kutoka kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Ghana dhidi ya Samaetex huko Samreboi. Umbali wa kilomita 270 kutoka Berekum.


