Na Mwandishi Wetu
KLABU ya Fountain Gate FC imemtangaza Fred Felix Minziro kuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, akichukua nafasi ya Mohamed Laizer ambaye amefutwa kazi kutokana na mwenendo usioridhisha wa timu.
Kwa mujibu wa taarifa ya klabu hiyo, Minziro ataongoza benchi la ufundi akisaidiwa na makocha wengine Mathias Wandiba pamoja na Abubakari Francis, ambaye anaendelea na majukumu yake ndani ya kikosi hicho.
Minziro anapewa jukumu hilo wakati Fountain Gate ikiwa katika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kucheza michezo 17 na kujikusanyia alama 16.
Uongozi wa klabu hiyo umesema una Imani na Minziro kutokana na uzoefu wake katika soka la Tanzania, huku ikiendelea kuhakikisha inajenga timu imara.


