Na Mwandishi Wetu
WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia TUME ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na CRDB Benki Foundation imetenga jumla ya Shilingi bilioni 4.6 kwa ajili ya kuwawezesha mitaji vijana wabunifu waliofikia hatua ya kupeleka bidhaa na huduma zao sokoni.
Akizungumza leo Februari 13, 2026 jijini Dar es Salaam katika warsha ya kuwajengea uwezo wabunifu wanufaika wa Mfuko wa Samia wa Ubiasharishaji Ubunifu, Naibu Waziri Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidhi Ameir ameielekeza –COSTECH na CRDB kuwasimamia vijana hao kuzalisha bidhaa bunifu ili ziingie katika soko shindani.
Amesema uwekezaji huo unawalenga watanzania wenye bunifu zilizo tayari kuingia sokoni lakini wanakosa mitaji, akisisitiza kuwa mfuko huo uko wazi kwa wabunifu wote wenye bidhaa au huduma zilizo tayari kuwafikia walaji.

“Wizara ilitenga Sh. bilioni 2.3 kwa ajili ya kutoa mikopo nafuu kwa wabunifu, fedha ambazo ziliwekwa kwenye Mfuko wa Samia wa Ubiasharishaji Ubunifu. Kutokana na wingi wa wabunifu nchini, Serikali iliingia makubaliano na Benki ya CRDB ambayo nayo ilichangia shilingi bilioni 2.3, hivyo kufanya mtaji wa mfuko huo kufikia bilioni 4.6,” amesema.
Hata hivyo, Naibu Waziri huyo, ameeleza kusikitishwa na kasi ndogo ya uchukuaji wa mikopo akisema kuwa katika kipindi cha miezi 10, ni vijana saba pekee waliokuwa wamenufaika na mfuko huo huku kiasi cha Sh. milioni 767 tu kikiwa kimetumika kati ya bilioni 4.6 zilizotengwa.
Kutokana na hali hiyo, ametoa wito kwa vijana wenye bunifu zinazoweza kuwa bidhaa au huduma kuwasilisha maombi yao kupitia COSTECH ili kunufaika na fedha zilizopo, ambazo zitasaidia kuanzisha biashara, kutoa ajira na kuchangia uchumi wa taifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji CRDB benki foundation, TullyEsther Mwambapa amesema ushirikiano huo ni dhamira ya benki hiyo kuendelea kuwainua vijana kujikwamua kiuchumi ikiwemo kuwapatia mitaji.

Amesema vijana wengi wana mawazo bunifu na suluhisho mbalimbali lakini changamoto kubwa imekuwa upatikanaji wa mitaji ya kuyapeleka sokoni.
Amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha mfuko huo akisema umeanzishwa kwa wakati sahihi kusaidia vijana kubadili mawazo yao kuwa biashara zinazozalisha ajira.
Amesema katika awamu ya kwanza, maombi 152 yalipokelewa, ambapo 22 yalitimiza vigezo kikamilifu na hatimaye wabunifu saba walichaguliwa na kupatiwa jumla ya Sh. milioni 667, kila mmoja akipata fedha kulingana na mahitaji ya mradi wake.
Miongoni mwa wanufaika, Paul Musiba ambaye ni mmiliki wa kampuni ya ufugaji nyuki, amesema alipata mkopo wa sh. milioni 135 uliomwezesha kununua vifaa vya kisasa, kuanzisha kliniki ya nyuki na kuongeza uzalishaji wa asali kwa ajili ya soko la nje, hali iliyosaidia pia kuajiri vijana wenzake.


