MIONGONI mwa viongozi wakuu waliopata kuiongoza Tanzania na kukumbana na upinzani mkubwa katika kurekebisha mifumo ya uchumi, ni Marehemu Benjamin William Mkapa. Upinzani huo, ulimfanya siku moja katika mfululizo wa hotuba zake kwa umma ambazo aghalabu alikuwa akizitoa kila mwezi, kumnukuu kiongozi wa zamani wa China, Deng Xiaoping katika usemi wake maarufu wa mithali ya “Haijalishi kama paka ni mweusi au mweupe, almradi anakamata panya.” Deng aliongoza taifa hilo katika mageuzi ya kiuchumi kuanzia mwishoni mwa miaka ya 1970.
Kiongozi huyo wa China alitumia msemo huu kuonyesha kuwa katika maisha ya mwanadamu kila wakati ni lazima abadili mbinu kama kweli anataka kuleta mabadiliko ya maana ya maendeleo yake na ya kizazi chake. Ikumbukwe wakati huo Deng alikuwa anasukuma sera za kiuchumi za soko huria – Mageuzi na Ufunguaji – wakati taifa hilo kwa miongo kadhaa likiwa limebobea katika sera na siasa na uchumi wa kijamaa. Kwa maana hiyo, kwa Deng alichokuwa anawinda kama jambo la msingi katika utawala wake ni ufanisi, si kama sera fulani inafuata itikadi kali ya kikomunisti au kibepari. Kama sera ingesaidia kuendeleza China, ilikubalika hata kama ilikuwa imeigwa kutoka kwa mifumo ya kibepari.
Kila ninapotafakari na kutazama hali ya huduma ya usafiri wa Mabasi ya Mwendokasi katika jiji la Dar es Salaam, ninamkumbuka Mkapa kwa kauli yake hii ya “Haijalishi kama paka ni mweusi au mweupe, almradi anakamata panya.” Mkapa alitoa kauli hii akikabiliana na shinikizo kubwa kutoka kwa watu mbalimbali, akiwapo Mwalimu Julius Nyerere, juu ya mageuzi ya kiuchumi aliyokuwa akiyasukuma. Kubwa ubinafsishaji wa mashirika ya umma, pia kuendeleza sera za uchumi wa soko ambazo tayari mtangulizi wake, Ali Hassan Mwinyi, alikuwa ameanzisha katika miaka ya mwishoni ya utawala wake.
Kwa nini nimemkumbuka Mkapa hivi na kwa nini nimekumbuka kauli yake ya kukopa neno la busara kutoka kwa Wachina? Ni kwa sababu, bila kuongeza chumvi huduma ya usafiri wa umma ya Mwendokasi katika jiji la Dar es Salaam, imekuwa ni janga. Ni janga kwa sababu moja tu, imeshindwa kufikia viwango vya huduma ambayo wakazi wa jiji hilo walikuwa wanatamani. Imeshindwa kusaidia wakazi wa jiji hilo kuachana na adha ya kuendesha magari yao binafsi kwenda kwenye mihangaiko yao na badala yake watumie usafiri huo wa umma; imeshindwa kuwapunguzia gharama za maisha wakazi wa jiji hilo kwa kuepuka kuendesha magari yao; imeshindwa kusaidia kupunguza msongamano wa magari barabarani, kwa kuwa kila mwenye gari lake dogo anaona ni bora tu ang’ang’ane barabarani kuliko kukabiliana na adha na kero ya mabasi ya Mwendokasi.
Adha hizi ni pamoja na kupoteza muda mrefu kituoni bila basi kufika kwa wakati; mabasi mabovu na yaliyochoka kiasi cha kushindwa kumaliza safari kwa wakati; vurugu na msongamano mkubwa wa abiria; lugha zisizo za staha kutoka kwa madereva ambao wameathirika kisaikokojia kutaja kwa uchache tu.
Mwendokasi imefikaje hapa? Ni matokeo ya mfumo wa mashirika ya umma. Mfumo ambao kwa miaka mingi ulishindwa kuzaa matunda tarajiwa. Ndiyo mfumo ambao Mkapa alikumbana nao na akaanza kuubadili kwa ama kuuza/kubinafsisha baadhi ya mashirika au kuyafunga mengine ili kuchochea ufanisi- ndiyo maana ya kauli yake kumrejea Deng na dhana yake ya “Haijalishi kama paka ni mweusi au mweupe, almradi anakamata panya.”
Kilichoshindwa kwa Mwendokasi ni huduma ya mabasi. Yako hoi. Huduma hii ilianza Juni 2016 kwa matarajio ya wengi kwamba sasa Dar es Salaam litakuwa ni miongoni mwa majiji bora kabisa kwa huduma ya usafiri wa umma. Miundombinu iliyojengwa kwa ajili ya mabasi haya ni ya ubora wa hali ya juu. Gharama ya kujenga miundombinu hii – barabara, madaraja, vituo vya abiria, karakana – ni kubwa. Miundombinu hii imejengwa kwa awamu tofauti, gharama kubwa imetumika, na ni hakika imependezesha Jiji la Dar es Salaam kwa uzuri na ubora wake.
Katikati ya ubora huu wa miundombinu ya kisasa na bora, jiji la Dar es Salaam limezidi kuzama katika huduma duni kabisa ya usafiri wa umma. Awali mabasi ya daladala yaliondolewa katika barabara ya Morogoro kuanzia Mbezi Mwisho kupitia Kimara mpaka Kivukoni na Kariakoo; Ilitarajiwa kwamba huduma bora ya usafiri wa umma ingetolewa na mabasi ya Mwendokasi. Hali kwa sasa ni kinyume kabisa. Huduma ni duni mno.
Na isivyo bahati, katika ubora wa miundombinu hii, abiria wengi katika barabara ya Morogoro ambako ndiko Mwendokasi ulikoanzia huduma, wamekimbilia kwenye usafiri wa bajaji na pikipiki. Usafiri wa hatari kabisa. Idadi ya bajaji na pikipiki katika barabara hii haielezeki, asubuhi, mchana na usiku. Yaani katika neema ya ubora wa mtandao wa barabara na miundombinu mingine ya BRT, wakazi wa Dar es Salaam wanakombolewa na bodaboda na bajaji. Kweli?
Jiji la Dar es Salaam linatajwa kuwa ni miongoni mwa majiji 10 yanayokua kwa kasi zaidi duniani. Makadirio ya Umoja wa Mataifa (UN) yanaonyesha kuwa Dar es Salaam ifikapo mwaka 2030, yaani miaka mitano tu kutoka sasa linaweza kuwa na wakazi milioni 13 au milioni 16 kufikia mwaka 2035, jambo linalolifanya kuwa moja ya miji mikubwa barani Afrika. Kati ya mwaka 2010 na 2025, kiwango cha ukuaji wa idadi ya watu Dar es Salaam kilikuwa wastani wa asilimia 5–6% kwa mwaka, hiki ni kiwango cha juu sana ikilinganishwa na wastani wa ukuaji wa miji duniani wa takribani asilimia 2%.
Kwa mji wenye sura kama hii, inakuwa ni muhali sana kutegemea usafiri wa aina ya bajaji na bodaboda kuwa ndiyo usafiri wa kutegemewa na wakazi wake. Hakuna ubishi kwamba bajaji na bodaboda hizi zimeongeza adha katika barabara kuu za mijini. Uendeshaji wake ni wa hatari wakati wote. Usalama wa abiria ni wa hatari wakati wote. Vurugu zake hazielezeki kwa maneno matupu. Ni adha ya kweli. Ni vyombo vya moto ambavyo kwa sasa vinachangia kwa kiwango cha juu kabisa kama chanzo cha ajali.
Ni katika kutafakari haya, hatuna budi kujiuliza, ni lini shirika la umma hapa nchini lilipata kuwa na mafaniko ya maana katika kutoa huduma yoyote ikilinganishwa na sekta binafsi? Ni kwa mantiki hii Mwendokasi ulipaswa kuanzia siku ya kwanza kabisa uingizwe katika ushindani. Bila ushindani hata kama yataletwa mabasi mapya 1,000 ni hakika huduma haitaimarika. Mkapa alikopa busara China – “Haijalishi kama paka ni mweusi au mweupe, almradi anakamata panya.” Tusaidiane kujenga uwajibikaji katika usafiri wa umma – Mwendokasi wametukumbusha tena kwamba rangi ya paka siyo hoja.


