Natoa nishani ya uthubutu kwa Kanisa Katoliki 2025

Siyo hulka yangu kujadili masuala ya dini katika chambuzi ninazofanya. Wala, sikusudii kujikita kuibua mijadala ya kiimani katika maandishi yangu, siyo leo wala siku za usoni. Ila leo itoshe tu kusema kwamba wakati tumeufunga mwaka 2025 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2026, kama taifa yafaa kujitazama na kujiuliza kama mwenendo wetu ulikuwa mwema kiasi gani kwa nia ya kujenga Tanzania bora zaidi kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Nilipata kusema katika safu hii kwamba mwaka 2025 unabaki kuwa mwaka wa giza na machungu kwa taifa letu. Tuliobarikiwa na Mola kuvuka na kuingia mwaka 2026 yafaa kula viapo kwa kusema ‘kamwe uovu uliotokea katika nchi yetu usijirudie tena.’ Kiapo hiki kitatusaidia kujisahihisha na kutafuta mwenendo mwema wa kujenga taifa linalojali kulinda haki na kutunza amani. Haki na Amani!

Ni katika tafakari hii, ninashawishika kulitaja Kanisa Katoliki kama taasisi ya kiimani ambayo bila kujali gharama, mwaka 2025 liliamua kusimama na kuheshabiwa katika nchi yetu kulinda Haki na Amani. Msimamo huo, ndio unanisukuma kuamini kwamba Kanisa Katoliki Tanzania linastahili kupewa nishani ya uthubutu ya kutetea Haki na Amani kwa ajili ya ustawi wa taifa letu.

Mtazamo wa uchambuzi wa kijamii na kisiasa unaliweka Kanisa katika nafasi ambayo wengine wengi wanaofanana nao waliogopa kufanya. Wamechagua ‘kufunika kombe ili mwanaharamu apite.’ Wameogopa kulipa gharama. Kanisa hili limekubali kubeba gharama. Huu kwangu ni utumishi na utume. Kwao kula meza kuu na wakuu, haikuwa kitu cha kuwafurahisha kama haki za wananchi ziliendelea kukanyagwa. Wamethubutu kusema bila kujali gharama ya kupoteza fursa au nafasi!

Tunaambiwa na watawala waliokasirika kwamba Kanisa hili limetoa matamko mengi. Tunaambiwa ni jumla ya matamko manane. Wakuu wamekasirishwa na matamko hayo. Wamechukizwa kwa nini Kanisa linatoa matamko hayo. Wakuu wana hasira kali dhidi ya Kanisa. Katikati ya hasira hizi wameibuka watu, kwa nafasi yao eti kama ‘waumini wa Kanisa Katoliki nchini, kuandaa waraka kwenda kwa wakuu wa Kanisa hilo kushitaki watumishi wa Kanisa walioko nchini. Wanawatuhumu kujihusisha na siasa. Wanawatuhumu kusaidia vyama vya upinzani. Wanawatuhumu kwa kiwango na kasi na kiwango kile kile kilichoonyeshwa na wakuu wa nchi juu ya msimamo thabiti wa Kanisa wa kutetea haki. Kukataa kukaa kimya huku haki za raia zikikanyagwa kwa kiburi cha kutisha.

Kanisa Katoliki limeamua kusimama lihesabiwe. Limeamua kubeba gharama ya kusimama upande wa haki hata katika mazingira ambayo wakuu wangetaka kila mmoja awe upande wao, bila kujali kama haki inasimama au la.

Inawezekana wote waliokasirishwa na Kanisa Katoliki hapa nchini wamesahau historia. Naomba niwakumbushe kidogo kwamba Kanisa linapogusa masuala ‘yasiyopendwa na wenye nguvu’ linazidi kudhihirisha historia yake ndefu ya kusimama upande wa haki za binadamu, utu, na wanyonge. Hapa Kanisa bila kuyumba wala kumung’unya maneno limekuwa likikemea mambo yafuatayo: ukiukwaji wa haki; matumizi ya nguvu kupita kiasi; ukosefu wa uwajibikaji; uchaguzi batili, amani na haki. Kwa kugusa masuala haya linaonekana na baadhi ya watu kuwa linahoji mamlaka au maslahi yao.

Ni katika juhudi za kujaribu kuliondoa Kanisa katika msimamo huo wa kutetea haki linafanyiwa figisu ili liondoke kwenye reli, limeundiwa hoja kwamba linajiingiza kwenye siasa. Wakosoaji wanadai kuwa Kanisa linapaswa kubaki madhabahuni, si kwenye masuala ya umma. Wanaojenga hoja hii wanasahau kuwa maadili ya jamii hayawezi kufikiwa bila kugusa masuala ya haki, amani na utu wa binadamu. Mambo haya kimsingi siyo siasa pekee—ni ‘maadili ya kijamii’ ambayo Kanisa lina wajibu wa kuyatetea na kuyalinda hata kama ikiwalazimu kupoteza nafasi ya kuwa karibu na watawala.

Kimaadili Kanisa lina wajibu kwa waumini wake kuwajenga kiroho, pia kimaadili. Ni katika msingi huo Kanisa Katoliki lina waumini wengi, taasisi za elimu na afya na wakati wote limekuwa sauti yenye kuaminika katika jamii. Kauli hizi aghalabu huamsha fikra za wananchi, jambo ambalo halipendwi na wale wanaotaka hali ibaki kama ilivyo.

Msimamo huu wa kutetea haki unawachukiza wote wanaotamani kuona hali ya utulivu wa juu juu (silence), ikitamalaki nchini na si kustawi kwa haki ya kweli. Wanaochukizwa wanataka watu wasilalamike, taasisi zisizungumze na raia wakubali hali iliyopo. Kanisa limesema wazi huu ni utulivu wa hofu, si amani ya haki. Wanaochukizwa wangependa sana kulinda maslahi au mfumo uliopo.

Kwa mantiki hii, Kanisa Katoliki linachukiwa, linalaumiwa kwa kuwa linasukuma mbele ajenda ya utetezi wa haki, kuibua maswali, kuomba uwajibikaji na kuweka wazi makosa. Msimamo huu wa Kanisa umeonekana kama tishio kwa mfumo au watu wanaonufaika nao.

Kwa hiyo, Kanisa Katoliki linaandamwa na watawala kwa sababu linatetea haki, ambayo kama ikiruhusiwa kujengeka nchini, kukuzwa na kuwa ndio mfumo uliokubalika katika kuendesha mambo nchini, huzaa amani; hujenga imani ya wananchi kwa watawala wao; hupunguza chuki na hasira zilizofichika katika jamii; na kwa maana hiyo huleta amani ya kweli na ya kudumu. Kinachofanywa na Kanisa kwa sasa kina manufaa makubwa chanya kwa taifa kwa muda mrefu ujao.

Hata hivyo, wasiotaka manufaa haya ambayo ni ya maana zaidi katika kujenga ustawi wa taifa haki na amani ya kudumu, wanasumbuliwa na athari za muda mfupi za watu kuleta upinzani dhidi ya dhuluma, kuchochea mijadala mikali yenye lengo la kusukuma mabadiliko chanya katika mfumo wote wa utawala, kijamii na uwajibikaji.

Kanisa Katoliki linapozungumza juu ya haki ni hakika halivurugi amani, bali linaibua msingi wa amani ya kweli. Wanaochukizwa na utetezi wa haki mara nyingi hawapingani kwa hoja, bali chanzo cha hoja. Wanatamani na kupendelea ukimya kuliko uwazi.

Kwa hali ya kisiasa ilivyo nchini kwa sasa, ambayo kwa hakika imejijengea uhalali kwa takribani miaka 10 iliyopita- mfumo usiohojiwa. Mfumo unaweza kumpoteza yeyote na kusiwe na uwajibikaji wowote, msimamo wa Kanisa Katoliki siyo tu ni ujasiri mkubwa bali pia ni utume wa ukombozi kwa ujumla wake bila kujali mtu ni wa imani gani. Ninapendekeza tutoe nishani ya uthubutu kwa Kanisa Katoliki kwa mwaka 2025.

spot_img

Latest articles

Yanga yaikung’uta vibaya Mashujaa FC

Na Winfrida Mtoi WANANCHI Yanga wameichakaza timu ya Mashujaa mabao 6-0, huku nyota mpya wa...

Watumishi wapya wa Ofisi ya Msajili wa Hazina wapigwa msasa

Na Mwandishi Wetu, Pwani OFISI ya Msajili wa Hazina (OMH), kwa kushirikiana na Chuo cha...

Kituo cha kupoza umeme Mtera kuboresha upatikanaji wa Umeme Iringa na Dodoma

Na Mwandishi Wetu SERIKALI kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imezindua Kituo cha Kupoza...

Tanesco Kigamboni yatoa elimu y nishati safi ya kupikia shule ya msingi Malaika

Na Mwandishi Wetu KATIKA kuunga mkono jitihada za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati...

More like this

Yanga yaikung’uta vibaya Mashujaa FC

Na Winfrida Mtoi WANANCHI Yanga wameichakaza timu ya Mashujaa mabao 6-0, huku nyota mpya wa...

Watumishi wapya wa Ofisi ya Msajili wa Hazina wapigwa msasa

Na Mwandishi Wetu, Pwani OFISI ya Msajili wa Hazina (OMH), kwa kushirikiana na Chuo cha...

Kituo cha kupoza umeme Mtera kuboresha upatikanaji wa Umeme Iringa na Dodoma

Na Mwandishi Wetu SERIKALI kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imezindua Kituo cha Kupoza...