Mwendokasi: Adha kwa abiria, gubu la madereva

Na Mwandishi Wetu

Inakaribia miaka 10 tangu usafiri wa mabasi ya haraka maarufu kama Mwendokasi ulianza rasmi kufanya kazi katika Jiji la Dar es Salaam kwa safari za Kariakoo, Kivukoni, Morocco, Kimara, kisha Mbezi – Kibaha.

Usafiri huo ulitarajiwa kuwa mkombozi wa wananchi wengi wanaotumia njia hiyo ikiwamo kuepukana na foleni, pia kusaidia kuwahi kwenda kwenye shughuli zao mbalimbali za kuhangaikia maisha.

Wakati mradi huo unazinduliwa ulianza ukiwa na mabasi 140, yanayojumuisha mabasi makubwa 39 yenye uwezo wa kubeba abiria 160 kila moja kwa wakati mmoja na mabasi madogo 101 yenye uwezo wa kubeba abiria 60 kila moja.

Kwa utaratibu wa mabasi hayo, yanatoa huduma kwa saa 18 kila siku kuanzia saa 11:00 asubuhi hadi 5:00 usiku. Huu ni muda ambao wakazi wa jiji la Dar es Salaam huwa katika pilikapilika nyingi za kimaisha.

Hata hivyo, siku zinavyozidi kwenda mradi huo unazidi kuwa na hali mbaya. Kama ni mgonjwa amefika hatua ya kuwa mahututi kutokana na kero iliyopo kwa sasa. Usafiri huu sasa ni kero, adha na tabu kwa abiria wanaoutumia.

Licha ya viongozi mbalimbali kujitokeza kuzungumzia hali hiyo na kutaka Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kufanya marekebisho, kauli zao zimekuwa ni ahadi tupu ambazo hazina vitendo, huku wananchi wakiendelea kutaabika kwa usafiri huo uliotarajia kuwa mkombozi wao.

Hizi ni baadhi ya karaha zinazopatikana Mwendokasi kwa sasa

Kurudi nyumbani na kiatu kimoja
Kutokana na msongamano wa watu wakati wa kupanda mabasi ya hayo hasa nyakati za asubuhi na jioni watu wakiwa wanasukumana kuwahi nafasi ya kuingia ndani, mara nyingi watu wanapoteza viatu na kujikikuta kufika nyumbani na kiatu kimoja, endapo hutakuwa na fedha ya kununua vingine njiani. Mfano mzuri pale kituo cha Gerezani Kariakoo na kivukono walipo watu wa matangazo viatu vimejaa pale ni vya watu wanaondosha wakati wa kupanda magari.

Wadada kudondosha mawigi

Kwa wanawake unapotumia usafiri huu unatakiwa kuhakikisha kama umevaa wigi limekaza vizuri, vinginevyo utajikuta kichwa kipo wazi ilhali ulivaa wigi lako. Hali hii ina inatokana na vurumai ya kusukumana, kuvutana huko na huko hali ambayo ikukumbana na wigi lililoegeshwa tu kichwani, ni hakika litadondokea bila taarifa yoyote. Kuna adha na maumivu mengine kwa wanawake wanaosuka rasta, kama ni ndefu, zitavutwa huku na huko wakiwa wanagombania kuingia kwenye magari. Unakuta watu ni wengi, katika kutafuta sehemu ya kujishika mwingine anamua kushika chochote au yeyote ili kumsaidie kuingia ndani ya basi. Hakuna kuchagua pa kushuka na kama huna nguvu utashia kuwa ngazi za wenzio kupanda.

Upo utaratibu wa kupanga foleni, lakini kutokana na hali ya kusubiri mabasi kwa muda mrefu kituoni, utaratibu huo haufuatwi tena, gari likija ni nguvu zako kupata nafasi. Hapa ni ile dhana ya mwenye nguvu mpishe, ndiyo inatawala utaratibu wa kupanda kwenye mabasi kwa sasa.

Gubu/Ubabe wa madereva
Baadhi ya madereva ni kama wameathirika kisaikolojia, kwa sababu wamekuwa ni wababe kwa abiria. Wanawajibu abiria wanavyojisikia na hawataki kuambiwa chochote, wakiona abiria wanalalamika sana wanafanya kile wanachotaka. Hapa ni kama watumiaji wote wa usafiri huu wameathirika, madereva hawana tena utulivu kama ilivyo kwa abiria wao.

Hali hiyo ipo hasa kwa madereva wa Kimara -Morocco. Unakuta dereva anaweza kushauriwa na abiria kuwa kwa sababu gari imejaa sana haina nafasi, basi  sio lazima kusimama kila kituo.  Hapo ndipo ugomvi unaanza kati ya abiria na dereva.

Muda mwingine hasa kituo cha Kinondoni Morocco, ni mara chache sana dereva anafika tu na kupakia abiria hata kama watu wamekaa muda mrefu. Atashuka kwenye gari atasubiri hadi kuona watu waliopo watapanda kwa kugombania.

Siku moja mmoja wa madereva alisikika akiwaambia abiria pale Kimara mwisho, kuwa: ‘ Sasa hivi mnatakiwa wenyewe mjiongeze, magari machache  sisi wenyewe kuja kazini tunapanda bodaboda. Mtu inakuwaje unakaa kituoni masaa mawili hadi matatu, hujiongezi tu ukajua magari ni machache. Sisi kama wanafanyakazi   hatuna  uwezo wa kuongeza magari au kusema usafiri hakuna,”

Kukaa kituoni muda mrefu
Imekuwa ni kawaida siku hizi mtu kukaa kituo cha Mwendokasi kwa saa mbili hadi tatu bila gari kuonekana. Hali hiyo inachangiwa zaidi na uchacha wa magari hayo. 

Magari kupaki mchana
Kuna tabia ya mabasi hayo kuegeshwa vituoni bila kufanya kazi hasa muda wa mchana. Abiria ukifika kituoni mchana tarajia kukaa muda mrefu hadi ifike idadi ya watu wanaotaka wao ndiyo gari itaondoka. Muda huo ambao kuna abiria wanaoingia kazini mchana unakuwa ni changamoto au muda mwingine unaona gari inapita tupu bila kuchukua mtu yeyote.

Kadi zimeadimika
Julai 30 mwaka huu DART ilisitisha rasmi matumizi ya tiketi na kuanza mfumo wa kadi, lakini cha ajabu ni kwamba sasa hivi ni mwezi unaisha kadi hizo kila unapokwenda hazipatikani. Hali hii imekuwa kero kwa wanaozihitaji ambao aidha walichelewa kukata au ni wageni wa usafiri huo. Kama huna kadi, inabidi uombe mtu akusaidie kukuwekea hela yako na akupitishe.

Kambi kokote

Safari siku hizi zimekuwa za mashaka, kwani imekuwa ni kawaida kukuta magari mawili au matatu yameharibika njiani na abiria wameshushwa katikati ya safari au kubaki ndani kusubiri litengenezwe.

Wiki iliyopita karibu na kituo kikuu cha Kimara Mwisho kulikuwa na burudani ya aina yake, basi moja lilikuwa linavuta jingine, lakini nalo likaharibika. Ukawa sasa ni kazi ya ziada ya kutengeneza lililoharibika walau likwamue hilo jingine. Hali hii inaonyesha kwamba DART haina hata breakdown ya kusaidia kukwamua magari yake barabarani yanapokwama.

Kwa muinekano tu, mabasi ya DART yamechakaa, yamechoka, hatavutii, siyo kwa muonekano wa rangi tu, bali hata uwezo wa bodi. Yapo yanayochafua mazingira kwa kutoa moshi kupita kiasi. Yapo ambayo yalibandikwa mabango ya matangazo na baada ya kuybaduliwa yameachwa na uchafu wa gundi. Kwa kifupi ni kama shughuli ya kuendesha mabasi ya mwendokasi, ni maji ya shingo kwa wenye dhamana.

spot_img

Latest articles

Ukatili huu wa Polisi unawapa faraja gani?

UKATILI uliofanywa na baadhi ya askari polisi dhidi ya raia waliokuwa wanakwenda kusikiliza kesi...

Vijana wahimizwa kuendelea kulinda amani

Na Tatu Mohamed VIJANA nchini wametakiwa kuhakikisha wanalinda na kuendeleza amani iliyopo kwa kuwa wao...

Serikali ya Austria kufadhili miradi ya umeme Tanzania

Na Mwandishi Wetu SERIKALI ya Austria kupitia Benki ya UniCredit imeahidi kuipatia fedha...

NIDA yawasajili watu wenye mahitaji maalum Temeke

Na Tatu Mohamed KATIKA kuadhimisha Siku ya Utambulisho Duniani, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA)...

More like this

Ukatili huu wa Polisi unawapa faraja gani?

UKATILI uliofanywa na baadhi ya askari polisi dhidi ya raia waliokuwa wanakwenda kusikiliza kesi...

Vijana wahimizwa kuendelea kulinda amani

Na Tatu Mohamed VIJANA nchini wametakiwa kuhakikisha wanalinda na kuendeleza amani iliyopo kwa kuwa wao...

Serikali ya Austria kufadhili miradi ya umeme Tanzania

Na Mwandishi Wetu SERIKALI ya Austria kupitia Benki ya UniCredit imeahidi kuipatia fedha...