Na Mwandishi Wetu
Chama cha National League for Democracy (NLD), kimezindua rasmi Ilani yake ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ikiwa ni maandalizi ya kuelekea katika mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29,20252.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyowasilishwa leo Agosti 6, 2025 na uongozi wa chama hicho, Ilani hiyo imetaja vipaombele vikuu vinne ambayo ni ajira kwa wote, elimu bora na jumuishi, afya kwa maendeleo ya Taifa, pamoja na miundombinu ya kukuza uchumi.
“Ilani ya NLD imejengwa juu ya misingi ya uzalendo, haki na maendeleo, na imejikita katika vipaumbele vinne vikuu vinavyolenga kuleta mabadiliko ya kweli na maendeleo jumuishi kwa kila Mtanzania” imesema taarifa hiyo iliyotolewa na idara ya Itikadi, Uenezi na Mahusiano ya Umma ya Chama hicho.
Imeeleza kuwa Ilani hiyo ni dira na mwelekeo wa kisera kwa mgombea urais kupitia tiketi ya NLD, Doyo Hassan Doyo, kwa ajili ya kuomba ridhaa ya kuwaongoza watanzania katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
NLD inawaomba watanzania na kuunga mkono mwelekeo mpya wa Taifa, kwa kumpa Doyo ridhaa ya kuwaongoza katika kulijenga taifa lenye uzalendo, haki, na maendeleo kama sehemu ya kuleta usawa na fursa kwa wote.