Na Tatu Mohamed
BARAZA la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA CCC) limeshiriki katika Maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) kwa lengo la kuwaelimisha wananchi kuhusu matumizi sahihi ya nishati na maji, pamoja na haki na wajibu wao katika huduma hizo muhimu.
Akizungumza katika maonesho hayo, Afisa Uelimishaji na Uhamasishaji wa EWURA CCC, Lugiko Lugiko, alisema kuwa sekta za nishati na maji ni mtambuka, zikigusa maeneo mbalimbali ya maisha ya kila siku ya Mtanzania.
“Watu wanaweza kufuga kisasa kwa kutumia maji vizuri, na viwanda hutumia maji na umeme. Tunawahamasisha watumiaji kutambua namna wanavyoweza kugeuza matumizi ya huduma hizi kuwa fursa za kiuchumi,” alisema Lugiko.

Alibainisha kuwa EWURA CCC, kama chombo cha uwakilishi wa watumiaji, hufanya mashirikiano na wadau mbalimbali, ikiwemo viwanda, ili kuhakikisha sauti za watumiaji zinasikika kwa watoa huduma, hasa pale wanapokumbwa na changamoto.
Amefafanua kuwa, katika banda la EWURA CCC, wananchi wanapata elimu ya moja kwa moja kuhusu haki zao, namna ya kuwasilisha malalamiko, na pia msaada wa kitaalamu kuhusu masuala kama vile bili kubwa au utoaji wa huduma usioridhisha.
“Huduma zetu ni bure. Tunaeleza namna bili zinavyokokotolewa na kusaidia kutatua changamoto ili kuhakikisha huduma zinaboreshwa. Wananchi wana nafasi ya kutumia EWURA CCC kupata taarifa sahihi na msaada,” aliongeza Lugiko.
Aidha, EWURA CCC imeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikieleza kuwa sasa kuna teknolojia ya majiko ya kisasa yanayopunguza gharama na kuokoa mazingira.
“Kila mwananchi akidhamiria sasa anaweza kumudu kutumia huduma hizi, na hivyo kulinda afya na mazingira yetu,” alisisitiza.
Katika maonesho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma alitembelea banda la EWURA CCC na kufurahishwa na kazi inayofanyika.
Alitoa wito kwa baraza hilo kuendelea kusambaza elimu kwa wananchi na pia kufikisha huduma hadi vijijini.
“Changamoto tuliyopewa ni kufikisha elimu vijijini. Tunakiri kwa sasa tumefika mikoa yote, lakini tunawahakikishia Watanzania kwamba tutaendelea kutumia mitandao ya kijamii kuwafikia hadi walio mbali,” alisema Lugiko.


