JUMATATU wiki hii Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilipitisha majina ya wanachama wake watakaopigiwa kura ndani ya chama hicho ili kupata wagombea wa ubunge katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu. Ni mchakato ambao ulikuwa unasubiriwa kwa shauku kubwa na wananchi. Hatua ya mchakato huo sasa inafungua pazia kwa wanachama wa CCM kuamua kwa kura katika majimbo ya uchaguzi ni nani hasa anafaa kuwania ubunge katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Mchakato wa uchaguzi huu ambao Januari mwaka huu ulianza na vikao vya kupitisha wagombea urais na makamu wake, ndiyo ulimfanya aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, wiki mbili zilizopita kujiuzulu nafasi yake akilalamika kuwa mchakato huo haujakaa sawa. Polepole amekuwa na malalamiko mengi. Anahaha sana katika mitandao ya kijamii. Amefanya mkutano na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao. Malalamiko yake yamekuwa ni yale yale. Kukosekana kwa mchakato wa haki ndani ya CCM.
Leo nimesukumwa kujadili hoja za Polepole kwa kuzingatia mambo mawili makubwa. Mosi, kwamba Polepole anapata wapi uhalali wa dhamira kulalamikia mchakato wa uchaguzi ndani ya chama chake? Pili, Polepole anasimamia kwenye sheria ipi ambayo anaweza kusema inavunjwa au imevunjwa kiasi cha kumnyima usingizi? Kwa ushahidi wa kihistoria, Polepole hana hata chembe ya uhalali wa kulalamikia kitu kinachoitwa ‘rafu’ za uchaguzi.
Nitafafanua kidogo. Mtu anayedaiwa na kutajwa kwamba alikuwa anagawa fedha za kuwashawishi wabunge na madiwani wa upinzani kati ya mwaka 2016 na 2020 kujiengua kwenye vyama vyao kwa kilichokuwa kinaitwa kuunga mkono ‘juhudi’ za Rais John Magufuli, anapata wapi uhalali wa kidhamira kuzungumzia rafu katika mchakato wa uchaguzi?
Kama kuna mtu aliyegeuka kutoka mtu makini, anayejenga hoja, anayetetea mfumo dhabiti wa utawala wa demokrasia kwenda uimla, kusujudu watu, na matumizi mabaya ya fursa na nafasi za uongozi kati ya mwaka 2016 hadi mwaka 2020, Polepole hawezi kuepuka kuwapo kwenye hiyo orodha. Polepole hakuishia tu kuwakejeli wapinzani wa CCM, bali alitumia vilivyo fursa aliyokuwa nayo kwenye chama kuwakoga, kuwang’onga na hata kuwaumiza wale wote aliotofautiana nao kimtazamo na kimawazo.
Kwa mfano, tujiulize kama kauli za kutamba viongozi wa chama tawala wanatumia V8 na siyo Pick-up zilikuwa ni za kiongozi anayejali hashima za watu wengine achilia mbali hata taasisi kwa maana ya vyama vingine?
Kwamba Polepole huyu anayelia kwamba leo kuna rafu zinafanyika ndani ya CCM, akiwa amejificha kusikojulikana, mwaka 2019 (uchaguzi wa serikali za mitaa) na 2020 (uchaguzi mkuu) ‘uchafuzi’ wa uteuzi wa wagombea ulifanywa nchi nzima kiasi cha kufanya chaguzi hizo kuwa za ovyo zaidi kuliko chaguzi nyingine zozote ambazo zimewahi kufanyika katika nchi hii tangu kurejea kwenye mfumo wa vyama vingi, hakutoa neno lolote la kukaripia. Kikubwa alichofanya ni kupongeza ushindi wa kishindo wa chama chake. Aibu kubwa. Uovu wa uchaguzi katika nchi hii ulioasisiwa kati ya mwaka 2016 na 2020 Polepole hana pa kujificha kwamba hakuuona wala kuhusika.
Ni vigumu sana kumsafisha Polepole dhidi ya uovu wa uchaguzi wa mwaka 2019 na 2020. Ni vigumu pia kumsafisha Polepole na juhudi na matendo ya kusiginwa kwa kiwango cha juu kwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi kati ya mwaka 2016 hadi 2020. Ni vigumu kumtenganisha Polepole na uovu huo kwa sababu akiwa katika ofisi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi ya CCM siyo tu alikuwa ndiye msemaji na mtetezi wa usiginaji wa taratibu, kanuni na misingi ya utawala wa demokrasia ya vyama vingi, bali alikuwa shabiki mkuu wa kuwakoga na kuwang’onga wote waliokuwa wanaumizwa na maamuzi na matendo ambayo hayakuwa sawa katika kuenzi na kukuza demokrasia ndani ya nchi.
Inawezekana, Polepole wa mwaka 2025 siyo Polepole wa kati ya mwaka 2016 mpaka 2020, inawezekana ni mtu mpya huyu. Inawezekana ameongoka huyu, amejuta na sasa aujua ukweli na anataka kuuishi tena kama alivyokuwa zama akiwa mjumbe wa Tume ya Katiba Mpya iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba. Kwa maana hiyo, ana haki ya kusikilizwa.
Hata kama hoja ni hiyo, Polepole anapaswa kwanza kujitokeza hadharani, akiri wazi na kuomba radhi Watanzania kwa kushiriki uovu wa kisiasa kati ya 2016 hadi 2020. Akishaomba radhi, basi aeleza haya anayotaka kusema sasa. Labda katika muktadha huo anaweza kusikilizwa.
Polepole ni lazima ajue kwamba hawezi kuwa baridi na moto kwa wakati mmoja. Umma unajua fika Polepole aliyekubali kazi ya kuwa Mwenezi wa CCM chini ya Katibu Mkuu Dk. Bashiru Ally, siyo Polepole wa Tume ya Jaji Warioba ya Katiba Mpya; na ni hakika Polepole aliyejenga hoja sasa siyo yule aliyeshiriki kwa njia moja au nyingine kuharibu ustaarabu wa demokrasia ya vyama vingi iliyokuwa imestawi nchini tangu mwaka 1995 – 2015.
Ili Polepole aaminike, asikilizwe na akubalike, ni wito wangu kwake kwamba ajitokeze hadharani na kuomba radhi kwa Watanzania juu ya kuhusika kwake na uovu dhidi ya demokrasia ya vyama vingi aliyoshiriki kuufanya kati ya 2016 hadi 2020. Polepole aungame kwanza kwa uovu alioshiriki kuharibu mfumo wa demokrasia ya vyama vingi nchini, kama hataki kuungama, basi anyamaze milele.