Na Mwandishi Wetu
Mfanyabiasha Rostam Azizi ameeleza mbinu waliyotumia kuhakikisha tasnia ya habari inaimarika nchini na safari ya uanzishwaji wa vyombo binafsi vya habari ilivyokuwa.
Katika hotuba yake iliyosomwa leo Julai 15, 2025 na mwandishi wa habari mkongwe nchini ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Media Brains, Absalom Kibanda katika Mkutano wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika unaofanyika jijini Arusha mbele ya mgeni rasmi Makamu wa Rais Tanzania, Dk. Philip Mpango, imeeleza safari ya vyombo binafsi vya habari ilivyoanza nchini miongo mitatu iliyopita.


Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Leo, ninasimama mbele yenu kama shuhuda wa safari ya vyombo vya habari binafsi Tanzania tangu kuanza kwake mwanzoni mwa miaka ya 1990, zaidi ya miongo mitatu iliyopita.
Kama tulivyosikia hapa, miaka ya mwanzo ya 1990 ilikuwa ni miaka ya pambazuko jipya katika kurejea upya kwa ustawi tasnia ya habari nchini Tanzania na demokrasia.
Vuguvugu la kuanza kwa vyombo binafsi vya habari lilikwenda sambamba na kurejeshwa kwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi mwaka 1992.
Miezi kadhaa baadaye niliingia katika uwanja wa siasa nikiwa Mbunge wa Jimbo la Igunga kuanzia mwaka 1993.
Niliingia bungeni wakati joto la kurejea tena kwa vyombo binafsi vya habari lilipoanza na historia ikaanza kuandikwa kwa wamiliki wa mwanzo kabisa wa vyombo binafsi vya habari wakiwamo marehemu, Reginald Abraham Mengi, Rashid Mbughuni na Richard Nyaulawa, Jenerali Ulimwengu na wenzao wengine kuanzisha magazeti, redio na televisheni binafsi.
Kwa sababu ya kuwa kwangu muumini mkubwa wa uhuru wa habari na weledi wa kitaaluma, nikawa mmoja wa watu walioanza mapema kabisa kuguswa katika ustawi wa vyombo binafsi vya habari lengo likiwa kushamirisha umoja wa kitaifa, uwajibikaji na ustawi wa demokrasia na utawala bora.
Hulka hiyo ikanipa fursa ya kushawishiwa na waliokuwa wamiliki wa iliyokuwa Habari Corporation, Jenerali Ulimwengu, Salva Rweyemamu, Johnson Mbwambo na wenzao wengine kuwa mshauri wao wa kibiashara katika miaka ya mwisho ya 1990.
Wakati taifa likijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, Rais wa Tanzania wa wakati huo, Benjamin Mkapa alituita miye na Balozi Ferdinand Kamuntu Ruhinda na akatutaka kwa pamoja naye kukuna vichwa na kufafakari kuhusu umuhimu wa kuanzisha kampuni ya magazeti binafsi ambayo ubora wake wa kimaudhui na kitaaluma ungekuwa ni wa kiwango cha kimataifa.
Tulimkubalia Rais Mkapa na tukaanzisha Kampuni ya Mwananchi Communications mwaka 2000 ikiwa na magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Aidha tukaanzisha pia Radio Uhuru ambayo baadaye tuliikabidhi kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Ili kuimarisha ubora wa maudhui na kwa kuzingatia matakwa ya ustawi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na umajumui wa Afrika (panafrican spirit), mwaka 2003, miye na Balozi Ruhinda tulifikia makubaliano mahususi na Mtukufu Aga Khan kupitia kampuni yake ya Nation Media Group kuingia katika ubia na kampuni yetu ya Mwananchi Communications Ltd.
Hatua hiyo mbali ya kuimarisha ustawi wa vyombo vya habari nchini, ilisababisha nifikie uamuzi wa kuuza hisa zangu zote katika Mwananchi Communications na kisha nikawekeza katika kampuni ya iliyokuwa Habari Corportion ambayo wakati huo ilikuwa ikipitia kipindi cha uhitaji na tukaanzisha New Habari (2006) Ltd.
Uamuzi huo hatimaye ulisaidia kuyafufua na kuyapa uhai mpya, magazeti ya Rai, Mtanzania, The African, Dimba na Bingwa ambayo tayari ushapishaji wake uliishaanza kukabiliwa na changamoto kubwa wakati huo.
Mheshimiwa mgeni rasmi, mabadiliko ya mfumo na teknolojia ya upashanaji wa habari, yamesababisha mapinduzi makubwa katika sekta nzima ya habari na kuibua changamoto mpya ambazo zilisababisha baadhi yetu kukaa chini na kutafakari namna bora zaidi ya kuboresha vyombo vya habari.
Wapo wengine wengi waliothubutu kama sisi, lakini safari hii haikuwa rahisi; tulikumbana na changamoto nyingi kama uhaba wa waandishi wa habari wenye uwezo na weledi; pamoja na uhaba wa teknolojia ya kisasa.
Hata hivyo, tulisimama imara na kutumia fursa zilizojitokeza, na tunawashukuru marais wetu wote sita wa Tanzania ambao kila mmoja kwa namna yake aliimarisha vyombo vya habari binafsi.
Tulifanya huku vichwani mwetu tukiwa tumeizingatia kauli ya Rais wa zamani wa Marekani, Thomas Jefferson ambaye katika kuonyesha namna vyombo vya habari vilivyo muhimu katika taifa alipata kusema, iwapo angeambiwa achague ni nini kibakie kati ya serikali na magazeti, basi angechagua yawepo kwanza magazeti.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Leo hii, chini ya uongozi thabiti wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, uhuru katika sekta ya habari umeimarika, wajibu umezingatiwa na weledi unazidi kustawi.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Nitakuwa sijalitendea haki jukwaa hili kama nitaondoka bila ya kuzungumzia, alau kwa uchache, kuhusu zama mpya tunazoishi nazo ambapo tasnia ya habari imetawaliwa zaidi na mitandao ya kijamii matumizi ya artificial intelligence yaani AI.
Ninazungumzia haya si tu kama mfanyabiashara, wala si tu kama raia, bali kama mtu anayeamini kuwa roho ya taifa inaweza kujengwa au kubomolewa na uadilifu wa mazingira ya habari katika jamii yetu.
Tunaishi katika zama mpya — ambapo vita si tena kwenye uwanja wa mapambano wa kawaida, bali vinafanyika mtandaoni. Silaha siyo tena ni bunduki, bali algorithms. Kila simu ya mkononi imekuwa kipaza sauti. Kila “like” au “share” kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii ni kura ya maoni. Na kila uongo usiopingwa, hatimaye huwa sehemu ya majadiliano ya taifa na hatimaye kuwa sehemu ya kumbukumbu ya taifa.
Katika mazingira haya mapya, vyombo vya habari si tu vinakuwa mhimili wa nne kama tulivyozoea kusema — bali vimekuwa ndiyo kimbilio na tegemeo la kwanza la jamii kupata na kusambaza habari, hasa wakati wa mivutano ya kisiasa, majaribu ya kijamii, au mitafaruku ya kitaifa.
Lakini changamoto yetu kubwa leo ni hii:
Maudhui mengi yanayoongoza mijadala kuhusu Tanzania hayatoki ndani ya nchi. Yanazalishwa na kusambazwa na watu walioko nje ya mipaka yetu — watu wasioguswa na sheria zetu, mila zetu, wala misingi ya jamii yetu.
Watu hawa mara nyingi hawana hisa katika amani yetu, hawana uwekezaji katika maendeleo yetu, na hawawajibiki kwa madhara ya maneno yao.
Tuwe wakweli na tujiulize:
Je, ni sawa kwamba sauti zenye ushawishi mkubwa katika mjadala wa kitaifa ni zile zenye uwajibikaji mdogo kabisa kwa taifa letu na watu wake?
Na ikiwa si sawa, je, tunafanya nini kukabiliana na hali hii?
Jibu si kuziba midomo.
Jibu ni kuwekeza. Jibu ni kuijengea jamii uwezo.
Tunapaswa kuiwezesha Tanzania kumiliki na kuendesha majukwaa ya kisasa, yanayoweza kushindana katika uwanja wa kidijitali kwa kutumia ukweli, utu, ubunifu, na muktadha halisi wa Kitanzania.
Tunahitaji kuwajengea uwezo vijana wetu wa habari za kidijitali, wabunifu wa mitandao, wataalamu wa data na artificial intelligence (AI) — ili waweze kutoa habari na kusimulia simulizi ya taifa letu kwa macho yetu, kwa sauti yetu, na kwa misingi yetu.
Ninatoa wito hasa kwa sekta binafsi — wawekezaji na wafanyabiashara:
Huu ni wakati wa kuchukulia uwekezaji katika vyombo vya habari kwa uzito unaostahili.
Tunawekeza kwenye mahoteli na miundombinu, lakini tunasahau “miundombinu ya habari na simulizi” ambapo fikra, mitazamo na hulka za kizazi kipya zinafinyangwa kila siku.
Tunajenga viwanda, lakini tunasahau kuwa viwanda vya mtandaoni — ndivyo vinavyozalisha mitazamo ya kisiasa, maadili ya kijamii, na taswira ya taifa letu ndani na nje ya mipaka yetu.
Hili si suala tu la usalama wa taifa — ni suala la uhuru wa kifikra na uhuru wa kitaifa.
Tuwe wazi: uhuru wa kujieleza ni haki ya msingi inayopaswa kulindwa.
Lakini pia, ukweli nao unahitaji ulinzi.
Na ukweli unaweza kulindwa ipasavyo na wale ambao wana mizizi kwenye ardhi ya Tanzania, si wale walioko kwenye mawingu ya mtandao.
Tushirikiane — Serikali, sekta binafsi, wanahabari, na asasi za kiraia—kujenga majukwaa mapya ya kidijitali yasiyokuwa ya kukimbizana na uongo tu, bali ya kueneza ukweli kwa mvuto, kwa ubunifu, na kwa weledi.
Tuifanye Tanzania kuwa kinara si tu katika ukuaji wa uchumi, bali pia katika ubunifu wa vyombo vya habari, matumizi ya AI kwa maudhui ya maadili, na usimuliaji wa simulizi za kizalendo kwa njia shirikishi na za kidemokrasia.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Tasnia ya habari si sekta ya watu wachache. Ni hadithi ya taifa. Ni nguzo ya demokrasia, ni uwanja wa mijadala ya kisayansi, ni daraja kati ya wananchi na mamlaka.
Tuwe na ujasiri wa kuilinda. Tuwe na dhamira ya kuiendeleza. Na tuwe na akili ya kuibadilisha ili ikabiliane na zama za sasa.
Mungu ibariki Tanzania. Mungu ibariki Afrika.
Asanteni sana.