Na Mwandishi Wetu
Aliyekuwa Mbunge wa viti maalumu kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Esther Bulaya amesema alikuwa Chadema kwa mkopo sasa amerejea Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ni sawa Barcelona au Real Madrid na wanakwenda kutengeneza kikosi cha kushinda ‘Champions League’.
Bulaya ambaye amerejea CCM na kuchukua fomu ya kugombea Ubunge, Jimbo la Bunda Mjini mkoani Mara kupitia CCM, amejinasibu mbele ya waandishi wa habari kuwa chama alichokuwepo ni kama timu iliyoshuka daraja, hivyo amerudi kutoka kwenye mkopo.

“Unapozngumzia Chama Cha Mapinduzi ndio Barcelona ya Tanzania, Chama Cha Mapinduzi kimerudisha usajili kwa wachezaji wake wa Barcelona ambao waliwatuma kwa mkopo kwenye timu ya Leicester City ambayo imeshuka daraja,” amesema Bulaya.
Ameeleza kuwa alianza harakati ndani ya CCM tangu akiwa vyuoni, hivyo ana furaha kurejea katika chama kilichomlea.
Bulaya ni miongoni mwa wabunge 19 wa Viti Maalumu wa CHADEMA ambao chama hicho kilitangaza kuwavua uanachama, lakini walisalia bungeni hadi kuhitimishwa kwa Bunge la 12 kwa amri ya mahakama.