Na Mwandishi Wetu
Picha iliyotumwa na klabu ya Simba kwenye mitandao yao ya kijamii ni ujumbe tosha baada ya kocha wao Fadlu Davis na nahodha wa kikosi hicho kushindwa kutokea katika mkutano wa wanahabari leo Juni 24, 2025 kuzungumza kwa mujibu wa kanuni kuelekea mchezo wa kesho wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga unaotarajiwa kupigwa Uwanja wa Benjamini Mkapa.
Katika mkutano huo ambao Yanga ndiyo wenyeji, kama ratiba ilivyoonesha kocha wao Hamdi Miloud alifika kwa wakati akiwa na nahodha Dickson Job, wakazingumza na waandishi wa habari.

Baada ya kumaliza ilitakiwa kuwa zamu ya Simba lakini hakuna aliyeonekana ambapo kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, Karim Boimanda, wahusika hawapatikani kwenye simu.
Kutokana na hali hiyo, Boimanda aliamua kufunga mkutano huo na kuwataka waandishi wa habari waondoke kwa sababu kuna shughuli nyingine zinatakiwa kuendelea kuliko kisubiri watu ambao hawajui nini kimewakuta.

“Kwa mujibu wa ratiba ilitotumwa kwa klabu zote mbili, Simba ambaye ni mgeni katika mchezo huu alipaswa kuwepo hapa saa 5:30 kuanza mkutano, lakini tumefanya jitihada kadhaa bahati mbaya wahusika hawapatikani kwenye simu kwa hiyo tunashindwa kuelewa changamoto ni nini. Taarifa nyingine zitatolewa baadaye,” ameeleza Boimanda.
Ikumbukwe kuwa kumekuwa na matukio mengi tangu mchezo huu ulipotangazwa kuchezwa Machi 8, 2025 ambapo uliahirishwa baada ya Simba kushindwa kufika uwanjani. Ukapangiwa tarehe nyingine Juni 15, Yanga nayo ikazua jambo kwa kutoa masharti ili icheze mchezo hadi kusababisha baadhi ya viongozi wa Bodi ya Ligi kujiuzulu.