Dkt. Mpango awataka Watanzania kukemea vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto

Na Mwandishi Wetu

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Watanzania kukemea vitendo vya ukatili ulioshamiri dhidi ya wanawake na watoto na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa dhidi ya wahusika.

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Kanda ya Magharibi lililofanyika katika Ukumbi wa NSSF mkoani Kigoma.

Ametaja baadhi ya vitendo hivyo kama mauaji, ubakaji, ulawiti, kupigwa, kunyanyaswa, kunyimwa haki za kumiliki ardhi na mali nyingine za familia, urithi, fursa za elimu, ukeketaji, adhabu kubwa zisizowiana na kosa alilotenda mtoto.

Amesema baadhi ya vitendo hivyo vinafanywa na wanafamilia au ndugu wa karibu na sehemu kubwa ya vitendo hivyo havitolewi taarifa kwenye vyombo vya sheria ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

Ameongeza kwamba wakati mwingine, baadhi ya mila na desturi katika jamii hutumika kuwakandamiza wanawake na watoto.

Aidha Makamu wa Rais ametoa rai kwa Kongamano hilo ambalo idadi kubwa ya washiriki wake ni wanawake na ambao ni walezi wa familia, kuelekeza nguvu pia katika kumlinda mtoto wa kiume ili kumhakikishia usalama wake.

Amesema uwekezaji jitihada kidogo kwa mtoto wa kiume imepelekea mtoto wa kiume kujikuta katikati ya matatizo lukuki yakiwemo matumizi ya madawa ya kulevya, ushoga na aina nyingine za ukatili.

Amesisitiza umuhimu wa kuimarisha utoaji wa elimu na hamasa kwa umma kuhusu utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati safi ya kupikia. Amesema elimu kwa umma na hamasa ni muhimu katika utunzaji endelevu wa mazingira kwa kuwa tabiawatu ndiyo kisababishi kikuu cha uharibifu wa mazingira.

Ametoa rai kwa taasisi kama Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), TEMDO na nyingine kutafiti na kutengeneza teknolojia mbalimbali zinazotumia nishati safi na zenye gharama nafuu ili ziweze kusaidia uhamaji kwenda kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Vilevile ametoa wito kwa wafanyabiashara wakubwa na sekta binafsi kwa ujumla kujitolea kusaidia majiko na teknolojia rahisi kwa shule na vituo vinavyolea watoto na watu wenye mahitaji maalum.

Amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inatekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa Mwaka 2024 – 2034 ambao unalenga kuhakikisha 80% ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Amesema Serikali imesaini makubaliano ya awali na wawekezaji kuhusu Ruzuku ya Sh. Bilioni 8.64 kwa ajili ya nishati safi ya kupikia, ambapo jumla ya majiko 452,455 yamepata ruzuku kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa wananchi kwa gharama nafuu.

Pia amewasihi wanawake kushiriki kikamilifu katika kutoa hamasa kuhusu jukumu muhimu la kujiandikisha kupiga kura, kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kushiriki kuchagua viongozi wanaowapenda.

Amesema ni jukumu la kila mmoja kujenga na kudumisha umoja, amani, mshikamano na kuepuka vurugu katika mchakato wote wa uchaguzi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis amesema dhima ya kongamano hilo ni kuhimiza wanawake na jamii kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati safi.

Amesema pia Kongamano limedhamiria kuhamasisha wanawake kukaa na familia pamoja na kupata muda mzuri zaidi ili kujenga malezi na makuzi kwa mustakbali wa familia bora.

Kongamano la wanawake kanda ya magharibi ni sehemu ya maadhimisho ya Siku Kimataifa ya Wanawake Duniani ambayo kilele chake kitakuwa tarehe 8 Machi, 2025 Jijini Arusha. Kongamano hilo lina kaulimbiu isemayo ‘Mchango na ushiriki wa Wanawake katika matumizi ya nishati safi na utunzaji wa mazingira’.

spot_img

Latest articles

Timu ya Taifa kriketi ya wanawake kusaka tiketi ya kucheza Kombe la Dunia

Na Mwandishi Wetu Timu ya Taifa ya wanawake ya mchezo wa kriketi ya Tanzania inatarajiwa...

Ratiba ya Ligi Kuu msimu wa 2025/26 hadharani, Dabi ya Kariakoo Des 13

Na Winfrida Mtoi Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara(TPLB) leo  Agosti 29, 2025,  imetangaza ratiba...

TACTIC yaimarisha huduma za usafiri na usafirishaji Manispaa ya Sumbawanga

Na Mwandishi Wetu MRADI wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) unaelezwa kuimarisha huduma...

Hizi ndizo hisia dhidi ya INEC, Msajili wa Vyama vya Siasa

KATIKA safu hii wiki iliyopita niliandika uchambuzi nikihoji, ‘INEC, Msajili wa Vyama wanaweza kutupa...

More like this

Timu ya Taifa kriketi ya wanawake kusaka tiketi ya kucheza Kombe la Dunia

Na Mwandishi Wetu Timu ya Taifa ya wanawake ya mchezo wa kriketi ya Tanzania inatarajiwa...

Ratiba ya Ligi Kuu msimu wa 2025/26 hadharani, Dabi ya Kariakoo Des 13

Na Winfrida Mtoi Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara(TPLB) leo  Agosti 29, 2025,  imetangaza ratiba...

TACTIC yaimarisha huduma za usafiri na usafirishaji Manispaa ya Sumbawanga

Na Mwandishi Wetu MRADI wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) unaelezwa kuimarisha huduma...