KUNA habari njema tena kutoka ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Hizi ni za somo la demokrasia ambalo nchi ya Botswana imefundisha siyo majirani wake tu katika ukanda huo, bali kwa bara zima la Afrika, kwamba uchaguzi ni uamuzi wa wananchi. Si haki ya watawala.
Chama kilicholeta uhuru nchini Botswana mwaka 1966 na kukaa madarakani kwa karibia miongo sita, kimekubali kushindwa kwenye uchaguzi ambao Rais aliyekuwa madarakani,
Mokgweetsi Masisi (63), alikubali kushindwa na kumpongeza mpinzani wake wa muungano wa vyama vya upinzani – Umbrella for Democratic Change, Duma Boko (54), kwa kuibuka mshindi wa kiti cha urais.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 30, mwaka huu, upinzani walijikusanyia viti vya ubunge 35 katika Bunge la viti 61. Masisi alikuwa anatetea nafasi yake baada ya kuingia madarakani mwaka 2019 akimrithi Ian Khama.
Habari hizi njema kwamba Waafrika wanaweza kabisa kuendesha chaguzi huru na haki na rais aliyeko madarakani akakubali kushindwa na kukabidhi madaraka, zinaongeza ladha ya habari njema za Waafrika kujisimamia wenyewe kama ambavyo pia zilitokea tena katika ukanda wa SADC nchini Zambia Agosti 2021. Rais Edgar Lungu wa Zambia akipambana kutetea nafasi yake ili aongeze kipindi cha pili, alishindwa katika uchaguzi uliomwibua mpinzani wake, Hakainde Hichilema. Hichilema amekuwa na safari ndefu ya kuusaka urais na safari hii ilikuwa ni mara ya sita anarusha karata yake.
Hata hivyo, kwa Zambia haikuwa mara ya kwanza kwa rais anayetetea kiti chake kukubali matokeo ya kushindwa, kwani Oktoba mwaka 1991 Muasisi wa taifa hilo linalotambuliwa duniani kwa uzalishaji wa madini ya shaba, Kenneth Kaunda wa chama cha UNIP kilicholeta uhuru wa taifa hilo, alikubali kushindwa na Frederick Chiluba wa chama cha Movement for Multiparty Democracy (MMD). Ulikuwa ni ushindi wa kimbunga kwani Kaunda alipata kura 311,022 sawa na asilimia 24.23 tu wakati Chiluba aliibuka na kura 972,605. Ushindi wa Chiluba ulikuwa ni asilimia 75.77.
Habari za Botswana ni njema, kama ambavyo mwaka 2021 zilikuwa ni njema tena nchini Zambia kwamba nchi za Afrika zinaweza kuendesha chaguzi zake kwa amani, uhuru na haki na uamuzi wa wananchi kwenye sanduku la kura ukaheshimiwa.
Ni katika kutambua ukweli huo, Mwenyekiti wa Timu ya Waangalizi wa Uchaguzi wa SADC nchini Botswana, Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mizengo Pinda aliiambia jumuiya ya Watanzania wanaoishi Gaborone kwamba: “Kama kuna jambo la kjifunza ni hili la kukubali matokeo.” Pinda aliwaambia Watanzania hao na kusema alichoshuhudia ni kitu kizuri maana mpaka aliyeshindwa anampongeza mpinzani wake na kuahidi kumpa ushirikiano.
Kwa nini hizi ni habari njema kwa Waafrika? Zinavunja vunja dhana potofu kwamba Waafrika hawawezi kuendesha chaguzi huru na haki. Zinavunja dhana potofu kwamba Waafrika hawakubali matokeo ya uchaguzi kama anayetetea kiti chake hakushinda. Inavunja dhana potofu kwamba upinzani katika nchi za Afrika unasukumwa kwa nguvu ya mataifa ya nje yasiyozitakia nchi hizo mema.
Ni hakika, waliopiga kura mwaka 1991 nchini Zambia na kumpumzisha Jabali la siasa za nchi hiyo, Mzee Kaunda, ni wananchi wa Zambia. Ni wananchi wa Zambia hao hao Agosti 2021 walirejea kile walichokifanya mwaka 1991. Katika moto huo, Botswana ambayo kwa miongo yote ya uhuru wake imekuwa na mfumo wa vyama vingi, chama tawala kimetawala kwa uhuru na amani, lakini Oktoba 30, mwaka huu wananchi wa Botswana kwa uamuzi wao wenyewe wakaamua kukipumzisha chama hicho kikongwe barani Afrika.
Tunaposhuhudia matokeo kama haya kwa nchi za Afrika siyo tu kwamba rais aliyeko madarakani anaweza kukubali kushindwa na kujitenga kabisa na kebehi kama ambazo zimekuwa zikisikika kutoka kwa baadhi ya nchi kwamba hawezi kutoa madaraka kwenye karatasi kwa kuwa walifanya mapinduzi, tunapata moyo wa kuendelea kuhubiri siasa za kistaarabu. Siasa za kusikiliza uamuzi wa wananchi. Siasa za kuepusha zinazoitwa Tume za Uchaguzi, kupoka haki na mamlaka ya wananchi ya kuamua nani awe kiongozi wao.
Ni habari njema kwa sababu wale ambao wamekuwa na hila na inda katika bara hili kwamba eti siasa za vyama vingi ni pandikizi kutoka nje, kwamba eti siyo utamaduni wa Kiafrika, wanazidi kupata aibu na kufungwa midomo. Wakati wakisema siyo utamaduni wa Kiafrika na kwamba ni msukumo wa Kimagharibi, mtu anajiuliza swali, kwa nini basi tawala za kichifu ziliondolewa? Ni hoja dhaifu kukwepa siasa za ushindani wa vyama vingi kwa kudai kuwa ni chanzo cha mapigano, mparaganyiko na mauaji katika nchi za Afrika.
Zambia na sasa Botswana wametuonyesha kwamba kinacholeta mapigano siyo siasa za vyama vingi, bali ni tabia ya kukataa matokeo, tabia ya kukataa kujenga taasisi huru za kusimamia uchaguzi, tabia ya kuamini kwamba jeshi wakati wote litamsaidia rais aliyeko madarakani abakie madarakani hata kama uamuzi wa wananchi ni vinginevyo kwa uwazi kabisa kwenye sanduku la kura. Tatizo la nchi nyingi za Kiafrika ni kukataa kutengeneza taasisi imara, sheria na katiba zinazolinda uhuru na haki za raia wake ili uamuzi wa wananchi wakati wote uheshimiwe katika uchaguzi.
Matukio ya viongozi wa kijeshi barani Afrika kujitokeza hadharani nyakati za uchaguzi na kutoa kauli zinazoashirika kwamba kama ushindi hautakuwa wa chama tawala, hawatayakubali matokeo hayo yameathiri sana uwepo wa chaguzi huru katika nchi nyingi. Mambo haya ya aibu ambayo ni kinyume kabisa cha viapo vya kazi za wanajeshi, vimesababisha chaguzi katika nchi nyingi za Afrika kuwa vituko.
Matukio ya kutisha watu, kukamata watu, kufungulia mashitaka ya kupoka haki za watu kugombea nafasi za kuchaguliwa na mengine yanayofanana na hayo, ni masuala ambayo yanaaibisha hadhi ya chaguzi za baadhi ya nchi barani Afrika. Mfano uliodhahiri ni wa kiongozi wa upinzani nchini Senegal Ousmane Sonko, ambaye mapema mwaka huu aliundiwa kesi ambayo mwishowe ilimzuia kugombea urais. Matendo haya, siyo tu yanadhalilisha Afrika, bali pia yanaonyesha jinsi baadhi ya watawala wa mataifa haya wasivyokuwa tayari kusikia wanachotaka wananchi.
Ni suala la bahati mbaya kwamba utaratibu huu wa kushindwa au kukwepa kutengeneza mazingira ya kuhakikisha kwamba chaguzi zinakuwa huru, ikiwa ni pamoja na kujenga taasisi huru za kusimamia uchaguzi, kutungwa kwa sheria zinazohakikisha kila kura ya mwananchi inathaminiwa, umekithiri mno kiasi cha kujenga mfumo wa kifalme wa baadhi ya viongozi.
Pamoja na ukweli kwamba safari ya kuelekea kwenye demokrasia ya kweli katika nchi nyingi za Afrika bado ni ndefu, ngumu na ya kukatisha tamaa, yaliyotokea Botswana mwishoni mwa wiki iliyopita yanawafanya Waafrika wengi wapenda haki, uhuru na utawala wa sheria kuwa na uso wa kutabasamu japo kwa kitambo kifupi. Hongereni sana Watswana kwa kuing’arisha SADC na Afrika kwa ujumla.