Tumtarajie Kabudi yupi, wa makinikia au wa Tume ya Katiba?

PROFESA Paramagamba Kabudi ni mtu mwenye bahati sana. Huyu ni msomi mbobevu katika sheria. Yamkini watu wengi waliosoma sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walipita mikononi mwake. Kwa maana hiyo, huyu ni mwalimu wa wengi. Si jambo linaloweza kukubalika kumpuuza mtu mwenye hadhi ya uprofesa.

Ni nani asiyemkumbuka Profesa Kabudi na suala zima la mgogoro wa Tanzania na kampuni ya uchimbaji madini ya Dhahabu Barrick na kampuni yake tanzu ya Acacia katika sakata la makinikia na tuhuma za ukwepa kodi? Akiwa Waziri wa Sheria na Katiba Profesa Kabudi alisimama kidete kutetea hoja kwamba Tanzania ilikuwa ikiidai Acacia/Barrick jumla ya malimbikizo ya kodi na madai mengine yenye thamani Dola bilioni 190, kwa hesabu za wakati huo zilikuwa ni Sh. trilioni 440 na ushei.  Harakati za kudai fedha hizi zilianza mwaka 2017 hadi mwaka 2019.

Mwisho wa harakati hizi ni Tanzania kuingia makubaliano na Barrick ya kuja kulipwa Dola za Marekani milioni 300 sawa na Sh. bilioni 700 ambazo zingelipwa ndani ya miaka saba. Hata hivyo, fedha hizo zingelipwa baada ya Serikali kumalizana na Acacia ambayo ilikuwa inaidai Mamlaka ya Mapato Tanzania marejesho ya kodi ya ongezeko la dhamani (VAT) la Dola za Marekani milioni 240. Katika mukatadha huo, kama Acacia ilikuja kulipwa fedha zote hizo, basi kile kicholipwa na Barrick kwa serikali ni Dola za Marekani milioni 60 sawa na Sh bilioni 138 kwa viwango vya kubadili fedha za kigeni wakati huo.

Serikali iliunda timu za wataalam ikiongozwa na Profesa Nehemiah Osoro ambayo ilipewa kazi ya kuchunguza aina ya madini yaliyoko kwenye makinikia yaliyokuwa yamezuiwa kuuzwa nje ya nchi na thamani yake. Hakuna ubishi kwamba kazi ya kupambana na kampuni ya Acacia na baadaye Barrick ilikuwa ya changamoto kubwa, hasa kutokana na uzoefu wa Tanzania katika kuingia mikataba na kampuni za nje karibia kwenye kila eneo. Kila mahali tumekuwa shamba la bibi. Tunapigwa, na tunaendelea kupigwa hata leo!

Hitimisho la harakati zote dhidi ya Barrick taifa hili liliambulia kiasi hicho cha fedha kilichotajwa hapo juu, pamoja na kupata hisa za daraja B za Barrick asilimia 16, na kwamba Serikali itakuwa inagawana nao faida asilimia 50 kwa 50.

Profesa Kabudi akiwa Waziri wa Sheria na Katiba kama ambavyo amerejea kwenye kiti hicho tena, ndiye alikuwa kiungo kikuu cha majadiliano na kampuni ya Barrick, kama kuna tulichovuna ana cha kupongezwa kama tulipigwa, naye pia hawezi kukwepa lawama.

Tunaambiwa pamoja na serikali kushikilia makinikia kwa muda wote, mwishowe yaliendelea kusafirishwa kwenda nje. Kwamba ilikuwa iwe mwisho wa kusafirisha makinikia nje kwa kujengwa kiwanda cha kuyasafisha, mpaka leo hakuna ushahidi wa kujengwa kwa kiwanda hicho. Lakini la muhimu zaidi, bado mkataba ambao serikali ilikuja kuingia na Barrick baada ya kufurushwa kwa Acacia, unaeleza kwamba kama kuna kutokuelewana kesi zitaendelea kufunguliwa huko ughaibuni kinyume kabisa na msimamo wa awali wa kisheria kwamba kesi hizo zitafunguliwa katika mahakama za Tanzania. Pia sharti la Barrick kulazimika kuuza hisa zake asilimia 30 katika soko mitaji la hapa nchini halikufanikiwa, na iliendelea kupata vivutio vya uwekezaji kama ilivyokuwa mwanzo. Mathalan, Serikali ya Tanzania ilitoa misamaha mbalimbali ya Kodi kwa Kampuni ya Barrick Gold katika makubaliano yaliyoingiwa ikiwemo kodi ya ‘Capital Gains’ ambayo inatokana na mauzo ya hisa za Acacia kwa Barrick.

Ni katika picha hii, ile ndoto ambayo Watanzania waliooteshwa na kuaminishwa kwamba tungevuna sawasawa kutoka Barrick kiasi cha Dola bilioni 190 sawa na bajeti ya miaka 10 ya serikali wakati huo, pesa ambayo ingewezesha kila Mtanzania kununua gari aina ya Toyota Noah, haikutimia. Profesa Kabudi mwenyewe baadaye alikuja kusema kuwa serikali haikuwa inadai pesa hiyo zote, ila ilikuwa mbinu tu ya kuwavuta mezani Barrick.

Tuachane na suala la Barrick, tujiulize na kujikumbusha safari ya Mei 2020 ya Profesa Kabudi akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwenda Antananarivo, Madagascar na ndege ya Rais kufuata dawa ya kutibu UVIKO-19 ya CVO Tambavy ambayo aliuthibitisha umma wa Watanzania kuwa ilikuwa ni dawa iliyokuwa imegundulika na ilikuwa inatibu UVIKO-19. Alisema dawa ile ambayo alitumia ndege ya Rais Gulfstream, ilikuwa inagawa na Rais wa nchi hiyo pekee. Kabudi mwenyewe alionekana akiinywa akiwa huko huko Madagascar.

Ni safari ambayo Profesa Kabudi alirejea akiwa na shehena ya dawa hiyo, ambayo Madagascar iliipa Tanzania kama msaada/zawadi. Hakuna taarifa za kina hasa ni nani walipewa au walitumia dawa hiyo. Hata hivyo, Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMRI) nchini wakati huo, Profesa Yunus Mgaya, alisema dawa hiyo ingelifanyiwa uchunguzi wa kikemia na kibailojia ili kubaini utendaji wake.

Wakati Madagascar ikiaminisha dunia kuwa dawa hiyo ya mitishamba ilikuwa inatibu UVIKO-19, ndani ya wiki mbili baada ya safari ya Profesa Kabudi nchini humo, ilipigwa na wimbi kubwa la maambukizi ya UVIKO-19 kiasi cha kuomba msaada kutoka Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa.

Profesa Kabudi alikuwa miongoni mwa makamishina wa iliyokuwa Tume ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba. Zipo kumbukumbu za kutosha zikimuonyesha Profesa Kabudi akijenga hoja kwa nini ni lazima sasa kuwa na katiba mpya.

Ni bahati, Profesa Kabudi anarejea Wizara ya Sheria na Katiba ambayo ina wajibu wa kusimamia mchakato wa katiba mpya. Rais Samia Suluhu Hassan, alikuwa Mwenyekiti Mweza wa Bunge la Katiba. Rais na Waziri wake, wanajua kwa dhati ya mioyo yao, ni nini matamanio na mahitaji ya Watanzania kuhusu katiba mpya.

Jambo lisilojulikana mpaka sasa ni moja kwamba Profesa Kabudi wa safari hii tunayekwenda kumuona katika utendaji wake ni Kabudi wa Profesa wa sheria na mjumbe wa Tume ya Katiba, au Kabudi Waziri wa Sheria na Katiba wa mikataba kama sakata la makinikia na jinsi lilivyoishia, au tumtarajie Kabudi mpya? Pia kuna Kabudi Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambaye alikuwa na ujasiri wa kuwaambia mabalozi kwamba yeye siyo mwanadiplomasi?

Kwamba katika masuala ya kidiplomasia kwenye nchi yoyote mwanadilomasia namba moja ni Rais na msaidizi wake mkuu anayeweza kuitwa mwanadiplomasia namba mbili ni Waziri wa Mambo ya Nje. Ni katika nyakati za Kabudi akiwa Waziri wa Mambo ya Nje mabalozi na wakurugenzi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, waliona kila rangi, wakiwamo walioondolewa nchini katika mazingira tatanishi. Tumtarajie Kabudi yupi?

Mwandishi wa Makala haya ni Mkurugenzi wa Media Brains

www.themediabrains.com

spot_img

Latest articles

Hivi vikosi kazi vimerejea kwa mlango wa nyuma?

KUNA kila dalili kwamba taifa letu kidogokidogo linakumbwa na hali ya kutokuaminiana. Hali hii...

Chondechonde Polisi msisababishe wananchi wakate tamaa

ALHAMISI iliyopita yaani Desemba 5, mwaka huu wa 2024 lilitokea tukio baya la kuhuzunisha...

Ufaransa yaipatia Tanzania Sh bilioni 323.4

Na Mwandishi Wetu Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo La Ufaransa (AFD) wamesaini mikataba...

TANZANIA YAWEKA REKODI MKUTANO WA WAHASIBU WAKUU AFRIKA

Na Mwandishi Wetu Tanzania imeweka rekodi ya Mkutano wa Pili wa Wahasibu Wakuu wa Serikali...

More like this

Hivi vikosi kazi vimerejea kwa mlango wa nyuma?

KUNA kila dalili kwamba taifa letu kidogokidogo linakumbwa na hali ya kutokuaminiana. Hali hii...

Chondechonde Polisi msisababishe wananchi wakate tamaa

ALHAMISI iliyopita yaani Desemba 5, mwaka huu wa 2024 lilitokea tukio baya la kuhuzunisha...

Ufaransa yaipatia Tanzania Sh bilioni 323.4

Na Mwandishi Wetu Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo La Ufaransa (AFD) wamesaini mikataba...