Nape, Makamba watarejesha majambia alani?

“Mmekula kiapo hapa… Kiapo kina maana kubwa… si maneno tu… Mamlaka imewashuhudia na wananchi wamewashuhudia… Niwaibie siri. Kiapo kinapiga. Ukikiendea upande hakitakuacha. Ukikidhihaki kitakupiga…” Samia Suluhu Hassan akizungumza baada ya kuwaapisha viongozi aliowateua Ikulu Dar es Salaam, Julai 26.2024

Leo ninafanya rejea ya maneno ya Rais Samia Suluhu Hassan siku anawaapisha viongozi aliowateua Julai 21 mwaka huu. Ukiyasikiliza maneno hayo kwa haraka, huwezi kuelewa yamebeba uzito gani, lakini ukiyatafakari kwa kina unaweza kupata sababu hasa iliyomsukuma kutengua teuzi za mawaziri wawili, January Makamba, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye na waliokuwa Naibu Mawaziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Stephen Lujwahuka Byabato na Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk. Mbarouk atapangiwa kazi nyingine.

Mara kadhaa Rais Samia amekuwa mwepesi kudokeza, ingawa siyo moja kwa moja, sababu za kufanya mabadiliko katika nafasi za wateule wake. Amekuwa akikwepa sana kuwavua nguo hadharani wateule wake aliowaacha. Hii pengine ni kwa sababu ya haiba yake. Rais Samia siyo mtu wa kutunisha misuli. Alipata kuonya huko nyuma kwamba kwa wateule wake wanaofanya madudu, yeye atakuwa anafanya kazi kwa ‘kalamu tu’. Amesema mara kadhaa juu ya kutokutaka watumishi wa umma wanaogombana. Mizozo kwenye ofisi ya umma inamkera, na inamkera kweli.

Baada ya kuwaapisha wateule wake wapya, Balozi Mahmoud Thabiti Kombo (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki; Jerry Silaa (kutoka Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwenda Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari); Deogratius John Ndejembi (kutoka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwenda kurithi mikoba ya Silaa) na Ridhiwani Jakaya Kikwete kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), pamoja na viongozi wengine, aliwatobolea siri ya kiapo.

Ni kawaida kwa viongozi kula kiapo mbele ya mamlaka ya uteuzi. Hawa hula viapo viwili, kimoja ni cha kuwa mtii kwa mamlaka na pili kulinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na mambo mengine; cha pili ni cha uadilifu. Mambo haya hufanyika hadharani na kushuhudiwa na wengi. Haijapata kuelezwa kwa kina madhara ya viapo. Kwa kawaida wengi huchukulia viapo kama utaratibu wa kawaida tu, ni nadra sana kumsikia kiongozi yeyote akiwa na hofu ya kiapo. Ndiyo maana pamoja na utaratibu huu wa miaka yote, bado kuna ukengeufu mwingi katika ofisi za umma. Matumizi mabaya ya ofisi, wizi wa mali ya umma na hata wakati mwingine usaliti na uvujishaji wa siri za ofisi kwa maslahi binafsi.

Kwa muda sasa kumekuwa na mjadala kwamba Nape aliponzwa na kauli yake aliyoitoa kule Bukoba kwenye mkutano wa Mbunge wa jimbo la Bukoba Mjini ambaye pia alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Byabato. Kwamba kushinda uchaguzi siyo lazima kupata kura nyingi, kwamba kuna njia nyingi za ushindi.

Rejea ya Rais Samia kwenye ibara ya 8 (1) (a) inayotamka kuwa wananchi ndiyo msingi wa mamlaka yote, na serikali inapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa katiba, alipokuwa akizungumza baada ya kuwaapisha, inaashiria alikuwa anapeleka karipio kwa Nape. Kwamba hakuna njia mbadala ya kupata madaraka bila kutoka kwa wananchi. Na haya madaraka yanapatikana kwa ridhaa ya wananchi kwenye sanduku la kura. Ndiyo msingi wa kauli yake kwamba ‘ukikidhihaki kiapo kitakupiga.’

Watanzania wanajua na walimsikia Nape akijitetea kwamba alikuwa anafanya utani, akirejea kauli yake ya mwaka 2015 ya ushindi wa uchaguzi wa goli la mkono katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo. Wapo waliomwelewa, lakini wapo wengine waliosema kwamba ‘ukweli’ uliponyoka kwenye kinywa cha Nape. Ni suala litakaloendea kuamsha mjadala nchini kwetu juu ya dhana nzima ya uchaguzi huru na haki. Ni mjadala ambao umegubika mijadala na madai ya wadau mbalimbali wa demokrasia juu ya uwapo wa Tume Huru ya Uchaguzi katika chaguzi za Tanzania. Ni mjadala ambao pia umeshikamanishwa na madai ya Katiba Mpya. Nape ni mwanasiasa mkomavu, alipaswa kuelewa mawanda ya mambo hayo. Hakutafakari vya kutosha, imemgharimu na amemponza rafiki yake Byabato.

Ni vigumu kujua kwa undani juu ya nini hasa kimemtafuna tena January. Wakati wa Utawala wa Rais John Magufuli, wawili hawa, Nape na January walipata ajali ya kisiasa. Nape ‘alionewa’ kutokana na kuthubutu kuhoji vitendo visivyo sawa vya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ambaye alivamia kituo cha televisheni cha Clouds, jijini Dar es Salaam akiwa na askari wenye mitutu, usiku. Kwa kuwa Makonda alikuwa ‘mtoto deko’ wa Magufuli, Nape alipoanza kuchunguza suala hilo, aliondolewa kwenye nafasi yake ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

January alipoteza nafasi yake ya Waziri wa Mazingira na Muungano Julai 2019 baada Rais Magufuli kumfuta kazi kutokana na kunaswa kwa mawasiliano yaliyowahusu watu wanne, Makatibu Wakuu wa CCM wawili wastaafu, Abdulrahman Kinana, Yusufu Makamba (baba Mzazi wa January) na Nape, wakieleza kuchoshwa na udhalilishaji baadhi ya viongozi wastaafu wa CCM, wadhalilishaji walioonekana kuwa na kinga ya dola wakati huo.

Kwa bahati mbaya, siku nane tu baada ya wawili hao kutenguliwa, Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (Bara), Kinana amejiuzulu nafasi yake. Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amosi Makalla, ikimnukuu Mwenyekiti wa CCM Rais Samia, ilisema Kinana aliomba mwenyewe kujiuzulu na Mwenyekiti amemkubalia, japo kwa moyo mzito.

Matukio haya mawili, yaani kutenguliwa kwa Nape na January, na kisha kujiuluzu kwa Kinana ingawa hakuna muunganiko wowote wa dhahiri wa moja kwa moja mpaka sasa, historia ya yaliyopata kuwakuta watatu hao kwa pamoja, inaacha maswali mengi sana mitaani. Kwamba kwa nini ni kwa pamoja tena safari hii? Baba mtu, Yusufu Makamba, amempongeza Rais Samia kwa kumtengua mwanaye.

Pengine kauli ya Rais Samia wakati wa uapisho kwamba kila mteule wake ana kazi yake ya kufanya, kauli ambayo aliisisitiza kwa kina zaidi akimzungumzia Balozi Kombo, huku akimtaja Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Shelukindo, kuwa ni mchapa kazi hodari nayo inafikirisha. Je, kama Katibu Mkuu ni hodari, huku Waziri na Manaibu wake wote wakibadilishwa, kuna nini basi katika mahusiano ya kazi pale Wizarani. January ni Waziri wa tatu wa Mambo ya nje anabadilishwa tangu Rais Samia ashike madaraka Machi 2021. Walishapita Dk. Stergomena Lawrence Tax na Balozi Liberata Mulamula. Miaka mitatu na takribani miezi minne, wizara ya Mambo ya Nje imekuwa na sura mpya nne.

Kuna kitu kimoja hakisemwi sana, uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ulipanda mbegu mpya ya siasa za Tanzania, ambazo ndani ya kipindi cha miaka mitano ya utawala wa Magufuli, hadi 2020, CCM kama chama tawala kilipitia mabadilko mengi magumu. Kinana, Nape, Makamba na January kwa kiasi fulani, wanaaminika kuwa na mikono yao katika kile kilichotokea mwaka 2015, ambacho kilimfanya aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM wakati huo, kuwa na majina ya wagombea wake wa urais mfukoni. Kilichotokea dunia inajua. Lakini ile mbegu ya hila, kiburi na kuumizana bado inaendelea kutafuta watu ndani ya chama hicho na hata serikalini.

Suala moja la kujiuliza, Kinana na Yusufu Makamba kwa umri wao wanaweza kuwa wamemaliza kazi yao, je, wawili hawa, Nape na January watarejesha majambia alani, au wataanza mtifuano wa askari wa msituni? Tuvute subira.

spot_img

Latest articles

Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi yaanza kazi, yakaribisha wananchi kutoa maoni

Na Winfrida Mtoi Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi nchini, imesema tayari imeanza...

Urathi wa Mwalimu Nyerere usaidie kukubali kukosolewa

JUMATATU wiki hii Watanzania walikumbuka kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliyefariki...

Nimemsikiliza Gachagua, nikatamani Lowassa 2008 angelipambana vivyo

KWA zaidi ya wiki mbili sasa majirani zetu, Kenya, kumekuwa na siasa za moto....

Kukataa mgombea binafsi ni kukumbatia utumwa

HISTORIA inashuhudia kwamba wapo watumwa walikataa kuwa huru kwa sababu waliamini kwamba pamoja na...

More like this

Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi yaanza kazi, yakaribisha wananchi kutoa maoni

Na Winfrida Mtoi Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi nchini, imesema tayari imeanza...

Urathi wa Mwalimu Nyerere usaidie kukubali kukosolewa

JUMATATU wiki hii Watanzania walikumbuka kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliyefariki...

Nimemsikiliza Gachagua, nikatamani Lowassa 2008 angelipambana vivyo

KWA zaidi ya wiki mbili sasa majirani zetu, Kenya, kumekuwa na siasa za moto....