Wananchi Kipunguni kulipwa fidia mwezi ujao

Na Nora Damian

Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba amesema fidia kwa wakazi wa Mtaa wa Kipunguni wanaotakiwa kuhama kupisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, zitaanza kulipwa Agosti mwaka huu.

Akizungumza leo Julai 8,2024 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Jimbo la Segerea katika viwanja vya Shule ya Sekondari Liwiti, amesema imechelewa kwa sababu ya dharura iliyojitokeza katika mwaka wa fedha uliopita (2023/2024).

Dk. Nchemba alikuwa akizungumza kwa simu baada ya kupigiwa na Katibu Mwenezi wa CCM Taifa, Amos Makala, kutoa majibu ya suala hilo lililoulizwa na wananchi katika mkutano huo.

“Jambo la Kipunguni ninalifahamu vizuri na nilishafika Kipunguni kulielezea, tulitoa kauli ya serikali. Mheshimiwa mbunge (Bonnah) amelifuatilia mara nyingi, amelifikisha kwenye vikao kadhaa vya viongozi wakuu na vyote kauli ya serikali ilikuwa ni kuanza kulipa fidia mara moja.

“Tumechelewa tofauti na tulivyoahidi kwa sababu ya dharura iliyojitokeza katika mwaka wa fedha uliopita, tullikuwa na dharura kubwa ambazo zilikuwa zinalikata taifa vipande vipande yakiwemo mafuriko ya Kusini.

“Leo asubuhi nilikutana na ujumbe wa viongozi 10 kutoka Kipunguni, niliwapa majibu kwamba baada ya kuanza mwaka mpya wa fedha tunatarajia mwezi mmoja utatumika kuweka sawa mifumo mipya ya malipo…tunatarajia kuanzia mwezi wa nane tuanze kulipa wananchi wa Kipunguni,” amesema Dk. Nchemba.

Makala ambaye alikagua utekelezaji wa Ilani katika miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo ujenzi wa shule za sekondari amempongeza Bonnah na kusema ni mchapakazi.

“Bonnah anafanya kazi, mambo ya kusema mnyonge mnyongeni haki yake mpeni…ukishamnyonga haki anaipata wapi…kwahiyo tunakupongeza sana kwa kazi nzuri unayoifanya. Ni kamanda mzuri, yuko na wananchi wake na anawatetea muda wote.

“Kila waziri atakayeteuliwa awe wa ujenzi au uchukuzi anajua kuna swali la Kipunguni, lazima amuulize. Ameliweka vizuri suala hili na sasa yamebaki malipo, mimi shahidi wenu mwezi wa nane wananchi watapata fidia zao,” amesema Makala.

Awali Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli, amesema kwa muda mrefu wananchi wa Kipunguni wamekuwa wakiahidiwa kulipwa fidia bila mafanikio na kuiomba serikali kuharakisha malipo hayo.

spot_img

Latest articles

NESCH MINTEC YAPUNGUZA GHARAMA ZA VIPIMO VYA MADINI KUPITIA MAABARA YA MWANZA

Na Mwandishi Wetu WACHIMBAJI na wafanyabiashara wa madini nchini sasa wana fursa ya kupata...

OTR na IMF zajadili utendaji wa taasisi za umma

Na Mwandishi Wetu MSAJILI wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amekutana na ujumbe wa Shirika la Fedha...

MAAMBUKIZI MAPYA YA VVU YAPUNGUA KUTOKA 98,754 HADI 33,511

Na Tatu Mohamed MAAMBUKIZI mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU) nchini yamepungua kutoka watu 98,754...

MRADI WA UPANUZI WA KITUO CHA KUPOZA UMEME DEGE KUIMARISHA HALI YA UPATIKANAJI WA UMEME KIGAMBONI

📌Wafikia Asilimia 90 katika utekelezaji wake 📌 Kukamilika Mwisho wa Mwezi Disemba 2026 Na Mwandishi Wetu...

More like this

NESCH MINTEC YAPUNGUZA GHARAMA ZA VIPIMO VYA MADINI KUPITIA MAABARA YA MWANZA

Na Mwandishi Wetu WACHIMBAJI na wafanyabiashara wa madini nchini sasa wana fursa ya kupata...

OTR na IMF zajadili utendaji wa taasisi za umma

Na Mwandishi Wetu MSAJILI wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amekutana na ujumbe wa Shirika la Fedha...

MAAMBUKIZI MAPYA YA VVU YAPUNGUA KUTOKA 98,754 HADI 33,511

Na Tatu Mohamed MAAMBUKIZI mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU) nchini yamepungua kutoka watu 98,754...