KATIKA juhudi za kurejesha utawala wa sheria (orderly administration) katika jiji la Dar es Salaam, Serikali ilipata kuivunja Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Uamuzi wa serikali ulifikiwa Juni 28, 1996 baada ya kujiridhisha pasi na shaka yoyote kwamba halmashauri hiyo ilikuwa imeshindwa kuongoza Jiji hilo. Serikali ilitekeleza uamzi huo kupitia Tangazo la Serikali Namba 110 na 111 la Juni 28, 1996.
Baada kuivunja Halmashauri hiyo, serikali iliunda Tume ya Jiji kama chombo cha mpito, chenye jukumu la kuendesha shughuli zote za jiji na kuandaa mageuzi ya mfumo wa serikali za mitaa. Tume ilifanya kazi kwa takribani miaka minne, hadi mwaka2000, kisha muundo mpya wa Jiji hilo ukawekwa kwa kuunda Manispaa tatu, Ilala, Kinondoni na Temeke, na kisha kukawa na utawala wa Jiji ambao ulijumuisha wawakilishi kutoka halmashauri hizo tatu.
Kushindwa kuiongoza Halmashauri ya Jiji mwaka 1996 kulijidhihirisha vipi? Kwamba ilikuwa imeshindwa kuzoa uchafu. Jiji lilikuwa limetapakaa uchafu uliokithiri. Masoko ya Jiji hilo yalikuwa ni kitovu cha uchafu, hali iliyokuwa inatishia afya za wakazi wake. Wafanyabiashara ndogondogo walikuwa wametapakaa kila mahali. Vibanda vya mbao vilivyotengenezwa ovyoovyo vilikuwa vimetapakaa kila kona ya Jiji. Yaani hata karibu na Ikulu ya Magogoni kulikuwa na vibanda hivi!
Baada ya kuundwa kwa Tume hiyo, serikali ilimteua Mwenyekiti wake, Charles Keenja na makamishna wengine kadhaa. Wakapewa pamoja na majukumu mengine kuongoza Jiji hilo. Ni wakati huo, pengine kuliko wakati mwingine wowote, Jiji la Dar es Salaam iliwezekana kufanyiwa usafi. Iliwezekana kuondoa vibanda vya wafanyabiashara waliokuwa wamezagaa kila mahali bila utaratibu, iliwezekana kukarabati ofisi za Jiji na iliwezekana kutengeneza ‘orderly administration’.
Mpaka inafika mwaka 2000 uchaguzi mkuu unafanyika, Jiji la Dar es Salaam lilikuwa limepangwa likapangika, kulikuwa na utii wa sheria. Uholela ulipotea. Yeyote ambaye alijiingiza katika uholela iwe wa kufanya biashara ya umachinga, au mama ntilie wakati huo, sasa mama lishe, alikula hasara. Tena hasara kubwa.
Leo mwaka 2026, miaka 30 baadaye hali ya jiji la Dar es Salaam ni mbaya zaidi pengine kuliko ilivyokuwa mwaka 1996. Ni mbaya wakati kwa sasa Jiji hilo lina mabaraza matano ya madiwani – Ilala, Kinondoni, Temeke, Kigamboni na Ubungo. Kila baraza lina madiwani na meya wake. Kuna wakurugenzi wa manispaa hizo. Viongozi wa kuchaguliwa na kuteuliwa, leo ni wengi zaidi kuliko waliokuwapo ndani ya Tume kati ya 1996 – 2000 chini ya Tume. Wingi huo, siyo hoja.
Siyo hoja, kwa sababu hali ya Jiji la Dar es Salaam lenye manispaa tano ni mbaya zaidi leo. Ni mbaya kwa sababu kuna watu wameamua kutokutii sheria na taratibu zilizowekwa. Ndiyo maana sasa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameamua kuwa mabaraza ya Madiwani ya Ilala, Kinondoni, Temeke, Kigamboni na Ubungo. Ametangaza operesheni ya kuondoa malori yaliyogeuza sehemu ya barabara za jiji zilizojengwa kwa mabilioni ya fedha za walipa kodi kuwa ni maegesho yao bubu!
Mkuu wa Mkoa huo wiki iliyopita alizitaka kampuni za mabasi ambazo nazo zimekimbia kuegesha mabasi yao Stendi ya Magufuli iliyoko Mbezi Luis, na kuamua kutengeneza stendi bubu popote mtaani, warejee kwenye stendi hiyo. Eneo la Shekilango na Urafiki kandokando ya barabara ya Morogoro, ndiyo sasa limetia fora kwa stendi hizo bubu.
Malori na mabasi haya yalianza kidogo kidogo tabia ya kuegesha kila mahali, kwa fujo, vurugu na kiburi kikubwa, sasa tabia hiyo imeota mizizi na kugeuzwa kuwa haki. Mabasi yanaegeshwa Shekilango, ambako hakuna huduma yoyote. Siyo kibanda cha abiria kupumzika, siyo choo, siyo kioksi cha kununua hata maji ya kunywa. Mvua, jua na vumbi vyote ni halali ya abiria. Wenye mabasi haya kwa kiburi kikubwa hawajali, hawatishwi. Wenye malori hawa na madereva wao, wamegeuza karibia kila upenyo kando ya barabara zote za jiji kuwa maegesho yao. Vurugu mechi kubwa!
Juzi hapa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando akatangaza wamiliki wa mabasi ambao wamechomeka vibanda vyao vya kukata tiketi maeneo ambayo hayajaidhinishwa katika wilaya hiyo, waviondoe mara moja. Hadi sasa, hakuna kilichotokea. Hakuna. Wenye mabasi na malori hawana wa kuwatingisha. Siyo watendaji wa manispaa tano za Jiji la Dar es Salam, siyo Mamlaka ya Usafiri wa Ardhini, siyo Wakala wa Barabara (TANROAD) na hata sasa wamemtoa ofisini Mkuu wa Mkoa Chalamila. Anapambana nao.
Kwamba vurugu mechi hii inayoendelea katika jiji la Dar es Salaam siyo kitu kipya. Haijaanza jana wala juzi. Ilianza kidogo kidogo, na sasa imekuwa sheria. Nani wa kuwatisha wenye malori na mabasi? Nani wa kuwatisha na kuwashurutisha waendesha bodaboda na Bajaji kutii na kufuata sheria za usalama barabarani? Nani wa kuwagusa wamachinga ambao wamevamia kila barabara ya jiji la Dar es Salaam na kufanya wakazi wa jiji hilo waishi kwa stress za kutisha? Nani?
Kila uchao hali ya vurugu katika jiji la Dar es Salaam inazidi kuwa mbaya kwa maana ya uegeshaji wa malori, mabasi na uendeshaji wa bodaboda na bajaji. Hali hii inazidi kuwa mbaya wakati mabilioni ya shilingi yakitumika kuboresha miundombinu – kupanua barabara, kujega madaraja ya juu, kujenga mfumo mpya wa barabara za mwendo kasi. Nguvu kubwa inatumika kuboresha miundombinu hii, lakini bado hali ya msongamano wa magari na vyombo vya moto inazidi kuwa vurugu mechi.
Swali langu la kizushi, ni hili, yaani mabaraza matano ya madiwani yamekata pumzi kiasi kwamba hayawezi kufanya hata robo ya kile kilichofanywa na Tume ya Jiji ya Charles Keenja miaka 30 iliyopita. Ni kwa nini sasa mabaraza haya yaendelee kuwapo? Nani anawapa kiburi wenye malori na mabasi? Ninamkumbuka sana Keenja.


